Thursday

Mchumba anipenda mie Moyo mzito-Ushauri!

"Dear dinah, Natumaini hujambo na mwenyezi Mungu anazidi kukuongezea nguvu katika kazi yako ya kudumisha mahusiano ya watanzania wenzako. Dinah mpenzi mimi ni binti mwenye umri wa miaka 24.

Tatizo langu linalo nileta hapa leo ni ukosefu wa mapenzi kutoka kwangu mimi kwenda kwa mwenzangu. Labda nikuelezee scenario ya mapenzi yangu. Mimi na kijana mmoja tulikuwa majirani enzi za utoto wetu na tukaenda shule moja ya msingi, ila tulivokuwa wakubwa wakati tunaingia sekondari wazazi wa mwenzangu walihama mkoa tuliokuwepo na kuhamia mkoa mwingine.


Tukaja kukutana high school moja tena tukawa marafiki wa kawaida tu kwa sababu tulikuwa tukijuana kabla. Baada ya hapo kwa sababu mwenzangu kwao walikuwa na uwezo akaenda kusoma chuo kikuu nje ya nchi mimi nikabaki chuo kikuu hapa Tz.


Akiwa huko hatukuwahi kuwa na mawasiliano hata siku moja. Ikatokea siku nikapokea simu kutoka kwake akisema alinikumbuka na anataka kunisalimia tu hii ilikuwa mwaka mmoja kabla hajarudi nchini. Tangu hapo akawa anakawaida ya kunipigia simu kila siku.


Kikafikia kipindi akaniuliza kama nina mpenzi nikasema sina naye akasema hana tukaanza kuwa wapenzi kwa simu tu kama ilivyo kawaida ya wapenzi wa mbali. Tukaanza kuahidiana tutaoana akawa amejenga mawazo anamchumba Tz na mimi nikajua yeye ndiye mchumba wangu.


Lakini hapa katikati takribani miezi sita imebaki ili yeye mwenzangu arudi toka shule nikapata mtu (intruder) ambaye tulipendana ile ya mhemko kwa kuonana kwa mara ya kwanza.Wakati naanza mahusiano ya mapenzi na huyo intruder nilijitahidi kumfuta huyo rafiki yangu wa mbali katika mawazo yangu na nikafanikiwa.


Nilikuwa naona mapenzi ya simu ni kudanganyana tu hamna lolote. Ikafikia kwamba nikawa sina uhakika tena kama nampenda huyo rafiki wa nje(Ambaye tunapigiana simu) ama la. Mara nayo mahusiano yangu na intruder yakawa ya muda mfupi sana na wao walihama nchi kabisaa, kwani baba yake alikuwa Balozi nchini Tz kutoka nchi fulani ya nje.


Ilimbidi aondoke awafate wazazi wake na akawa amepata na shule ya masters huko huko kwa hiyo asingeweza kubaki Tz hata kama angependa, akanishawishi twende wote na wazazi wake watanitafutia shule nikakataa kwenda. Baadae nikashtuka na kuona kwamba huyu mtu atanipotezea wakati kwani sioni future kati yangu na yeye japokuwa mawasiliano yetu yalikuwa mazuri tu.


Sikuwa na la kufanya ikanibidi nimuache mwezi mmoja tu baada ya yeye kuondoka chini. Japokuwa kilikuwa kitu kigumu sana kufanya kwa wakati huo ukizingatia nimeshaharibu mahusiano na mchumba wangu wa nje.


Miezi miwili baada ya intruder kuondoka mwenzangu naye akarudi Tz. Na aliporudi alikuwa na higher expectations kuhusu mimi akataka sana kuniona nikawa namkimbia. Kijana wa watu haku give up na alikuwa akinifuatilia kila pahala, Sikuweza kumkimbia tena ikabidi sasa nimpe nafasi aweze kuonana na mimi.


Tukaanza kuzoeana kidogo kidogo. Ikafika siku tukaelezana story za maisha na nini kilipita hapo kati na kwanini nilikuwa sitaki kumuona, sikumficha nikamwambia ukweli kwani alikuwa na haki ya kuamua lolote na isingekuwa vizuri kuwa na siri kati yetu kama nimeamua kujitosa kuwa naye.


Mungu akasaidia hakuniacha na akanisamehe kwa sababu alikuwa akinipenda kwa dhati. Miezi mitatu baadae mpenzi huyu akapropose nami nikakubali. Lakini kusema ukweli ndani ya nafsi yangu nilikuwa nimeshamfuta wakati tunakutana ikawa najilazimisha kuwa naye na sikujua hata kwanini nilikubali hiyo proposal yake.


Siku zilivozidi kwenda ikawa nazidi kuona simpendi ikafikia hatua kila kitu akikifanya mie nakiona kibaya. Sasa nashindwa kuelewa what is happening to me. Mwenzangu ananipenda sana na anajionesha dhahiri kama ananipenda lakini mimi nimeshidwa kurudisha mapenzi, harusi bado miezi mitatu na bwana harusi simpendi nifanye?


Labda nimuelezee kidogo jinsi yeye alivo kitabia.. Ni mtaratibu anaongea kwa adabu, nimsikivu na anamapenzi kwa ndugu zake na ndugu zangu pia. Mapenzi anayajua vilivyo. Zaidi ya yote kusema ukweli kaka wa watu ni mzuri anamvuto wa haja, anapesa za kutosha hatuwezi kulala njaa.


Ukweli ni kwamba kumuacha sitaki nataka kupewa ushauri vipi nifanye nipate mapenzi nimpende yeye kama yeye. Maana yake sijawahi kupata mtu mwenye mapenzi ya dhati kama aliyo nayo yeye? Lakini moyo wangu umekuwa mzito kwake.

Please Help kuyajenga haya mapenzi na si kuyabomoa. Kwani niliambiwa we can learn to fall in love!
yours Tumaini"

Dinah anasema: Tumaini hadithi yako ni nzuri mpaka raha kuisoma, ulichonifurahisha ni kuwa wazi kw ampenzi wako na kumueleza ukweli ulivyokuwa ni wanawake wachache sana wenye uwezo wa kufanya hivyo, wako radhi kudanganya wapate "kumchuna" mtu kuliko kumpa mtu ukweli na nafasi ya kufanya uamuzi wa busara.


Kutokana na maelezo yako hakika mpenzi wako anakupenda na hata wewe unampenda kwa maana ya "love" lakini humpendi kwa maana ya "dislike", kwasababu kama ungekuwa humpendi kwa maana ya "love" basi usingefikiria kutaka kujenga nae mapenzi wala usingetaka ushauri wa namna ya kumpenda au hata kuhisi mapenzi na badala yake ungeachana nae siku nyingi.


Nadhani umeingia kwenye uhusiano "serious" mapema kabla hujamfuta yule mtoto wa Balozi a.k.a Intruder, sasa kwa vile bado hujaondokana na zile hisia za kimapenzi na yule mtoto wa Balozi itakuwia vigumu kuachiamoyo wako kwa huyu mchumba wako.


Unajua, Enzi zile za Bibi zetu pengine hata Mama zetu, wengi walikuwa wanajifunza kupenda ikiwa wanafungishwa ndoa na wanaume wasiowapenda. Hali kadhalika wanawake hao walikuwa wakitumia mbinu fulani-fulani (sio madawa/uchawi) ili kuwafanya waume zao kuwapenda ikiwa itatokea wameozwa kwa wanaume waliowapenda lakini wao mwanaume hawawapendi na wanaishi nao tu kwa vile wazazi walitaka iwe hivyo.


Kumdondokea mwenzio kimapenzi ni kitu nadra sana (haikupati kama vile hamu ya kula)hivyo basi kudondokewa na mwanaume ambae anakila kitu unachokitaka kwa mwanaume a.k.a "the one" ni sawa na miujiza na unapaswa kushukuru Mungu, kufurahi na kulienzi penzi la huyo mtu aliyekudondokea ambae anavyote utakavyo mwanaume kuwa navyo.


Nini cha kufanya; Msifunge ndoa wakati moyo wako ni mzito juu ya huyo Kijana na badala yake tafuta uwezekano wa kuisogeza mbele tarehe ya kufunga ndoa kwa kushirikiana na Mchumba wako ili upate muda wa kutosha wa kuufungua moyo wako ili kupokea penzi lake kama sio kujifunza namna ya kumpenda mumeo wa baadae.


Kumfanya mtu akupende ni rahisi zaidi kuliko wewe kumpenda yeye hasa kama huna kabisa hisia, lakini kwavile tayari mmekuwa pamoja kwa muda na sasa ni wachumba inamaana kuwa kuna hisia fulani kati yenu, pia kuna vitu umegudua ambavyo vinakufurahisha kuhusu yeye mchumba wako na vingine labda vinakuudhi lakini kubwa zaidi ni kuwa kuna mengi mnafanya kwa kukubaliana, shirikiana na mnafurahia "interest" za aina moja.


Kinachopungua au kukosekana hapo ni wewe kuufungua moyo wako zaidi ya ulivyo ufungua hivi sasa na ili kufanikisha hilo basi fanyia kazi yote haya nitakayokueleza hapa chini, bila kujali mtiririko wake.

1-Kuwa mkweli na nafsi yako ilikujua unataka nini kutoka kwake in terms of mapenzi sio alichonacho.

2-Focus kwenye nini hasa uta-offer kwenye uhusiano wenu.

3-Jifunze kufurahia/kupenda na ku-appriciate kila effort anayoifanya juu ya uhusiano wenu.

4-Mfundishe/mwambie afanye vitu vile unavyopenda/furahia.

5-Jjitahidi ku-share moyo wako wote kwa mwenzio, kamwe usiachie nafasi kwa jaili ya mtu mwingine aliyepita (mtoto wa Barozi) au mabaya aliyokufanyia huyu Mchumba hapo mwanzo.

6-Weka wazi ndoto zako za kimaisha kwa mpenzi wako.

7-Weka wazi uoga wako au vitu unavyohofia kuhusu uhusiano wenu au maisha yenu ya baadae.

8-Tumia muda wako mwingi kuwa na mchumba wako, jinsi utakavyokuwa unamzoea kiukaribu zaidi ndivyo hisia zitakapoibuka.

9-Fanya shughuli pamoja, Mfano; kutoka kwa ajili ya matembezi, chakula, kuona ndugu, jamaa na marafiki, kujichanganya kwenye sehemu ambazo mara nyingi pea/couple huwa pamoja (hii pia itakusaidia kuzalisha hisia zaidi juu yake).

10-Ukipata nafasi ya kuwa pekeyako jaribu kum-fantacise anakufanyia mambo fulani matamu ambayo hajawahi kukufanyia.

Baada ya muda usiozidi miezi miwili utaona au kuhisi tofauti juu ya hisia zako....hilo likitokea au kutotokea basi nitafute tena.

Kila la kheri!

No comments:

Pages