"Habari dada Dinah,
Hongera kwa kazi kubwa unayoifanya ya kutuelimisha, ubarikiwe sana. Mimi nina umri wa miaka 28, ni mama wa mtoto mmoja na kwa sasa ni mjamzito.
Dada Dinah ninapitia kwenye kipindi kigumu kwani baba mtoto hanijali kabisa yaani hajishughulishi kunisaidia kitu chochote na anapachukia nyumbani. Hana mapenzi na mimi na nimeacha kazi baada ya manyanyaso kazini.
Maisha yangu yamekuwa na huzuni kubwa, najiona nina bahati mbaya nasijui nifanyeje? Mume wangu hana muda wa kuongea na mimi, nashindwa hata kula chakula vizuri. Naombeani msaada wa mawazo na namna ya kumfanya mume wangu anijali na kunionyesha mapenzi kipindi hiki cha ujauzito."
Dinah anasema: Pole sana, kwakweli ni kipindi kigumu kwani sasa najua mtu unavyojisikia unapokuwa mjamzito. Ni ngumu kuamini mume anaweza kumfanyia mkewe vitendo hivyo.
Nashindwa kujizuia kuuliza maswali hili:-
Kabla hujashika Ujauzito huu wa pili mliwahi kujadili suala la kuzaa mtoto wa pili au mimba imetokea tu bila kupanga?
Mimi nakushauri uzungumze na Mama mkwe wako kuhusu tabia/vitendo vya mume wako na yeye anaweza kuzungumza na mwanae (lazima atamsikiliza mama yake) na wakati huohuo zungumza na mama yako mzazi wa ndugu yeyote wa karibu kutoka upande wako na wote kwa pamoja wanaweza kuitisha mkutano/kikao.
Ikiwa mumeo ataendelea na tabia yake baada ya kikao cha familia zote mbili, usilazimishe sana na badala yake wewe tafuta namna ya kurudi nyumbani kwenu/kwa wakwe (inategemea na taratibu za huko uliko olewa) kwajili ya mapumziko mpaka utakapojifungua.
Ujitahidi kula vizuri na kujitahidi kuondoa mawazo ili usiharibu afya yako na ya mtoto tumboni. Baada ya kujifungua utakuwa na nguvu ya kukabliana na mumeo uso kwa uso na kujaribu kurekebisha tofauti zenu.
Sasa hivi jitahidi ku-focus kwenye afya yako na afya ya mtoto alafu hayo mengine yafuate baadae. Mungu akutie nguvu, akupe amani na ujasili ili uweze kujifungua salama.
Kila la kheri!
No comments:
Post a Comment