Sunday

Wivu

Mambo vipi!

Hebu leo tulizungumzie hili suala la Wivu, natambua watu wengi wanaamini kuwa Wivu ni chanzo cha kufarakana na kutokuelewana. Baadhi huamua kuficha hisia hizo za wivu kwa vile wanaogopa kuachwa na wenza wao.

Vijana wa sasa ndio wanaongoza kwa kupinga hisia hizi za wivu, lakini tukirudi nyuma enzi zile za Hayati Bibi yangu kumfanya mtu akuonyeshe wivu ilikuwa ni sehemu ya mapenzi na ikiwa mpenzi wako hakuonyeshi wivu ni dalili kuwa humvutii tena (namna ya kumfanya mume awe na wivu ni somo kwenye kufundwa).

Pia wapo wanaopenda kuweka "Wivu" kama ubora wa hali ya chini sana kwenye uhusiano wa kimapenzi na hata ndoa. Ukifuatilia kwa ukaribu utagundua kuwa sehemu kubwa ya watu wanaopinga hisia za Wivu kwenye uhusiano ni ama wanawapenzi zaidi ya mmoja au hawajui Wivu ni nini? kama sio wanachanganya wivu na kuwa "obsessed"(kwa kiswahili ni?).


Inashangaza unapomkuta mtu anataka mpenzi wake awe mlevi wa penzi lake (addicted) lakini hataki mpenzi huyo awe na wivu juu yake....hapo huwa najiuliza ikiwa unamkolezea mwenza wako mapenzi motomoto kiasi kwamba unakuwa "tiba" yake na bila tiba hiyo hajiwezi tena, kwanini asiumie kihisia ikiwa haupo karibu yake au umechelewa kurudii nyumbani?


Wivu ni hisia kama ilivyo penzi, hupangi au kuchagua bali inatokea tu. Wivu mara zote uhusisha mtu wa watatu, inaweza kuwa jirani, rafiki, mfanyakazi, mpenzi wa zamani n.k.

Wivu hauna tafsiri wala sababu kama ilivyo kwenye hisia za kimapenzi, anaekupenda siku zote huwa hana sababu ya kukupenda bali hutokea tu anakupenda, japokuwa kukupenda huko kunaweza kuongezeka siku hadi siku kutokana na matendo mema au mapenzi unayompa n.k basi hata wivu ni hivyo hivyo na huongezeka kutokana na matendo mema na mapenzi unayotoa.

Wivu unaweza kuwa maumivu ya hisia (mtu unakonda tu...lol), hasira, Uoga, hofu, na huzuni. Vilevile wivu unaweza kujionyesha kwa mhusika kuwa mfuatiliaji, muuliza maswali, uhakiki wa muda/mahali au kutaka kujua maisha ya mpenzi wako ya kimapenzi kabla yako.

Wivu unahimarisha uhusiano na kukufanya uhisi/ujue kuwa mwenza wako anakujali, inakufanya wewe mpenzi kuona namna gani unamrusha roho japokuwa mmekuwa pamoja kwa miaka mingi.

Wivu mzuri nii ule unaokwenda sambamba na na mapenzi na kujaribu kumsukuma mtu wa 3 ambae labda humuamini mbele ya mpenzi wako kutokana na mazoea yao.

*Kuna ila hali ya kutomuamini mpenzi kwa vile tayari amewahi kukutenda, au umewahi kumfuma na mtu mwingine "wakidukuana", hali hiyo sio Wivu kama wengi ambavyo huita bali ni kutomuamini mwenza wako.

Pia kuna ila hali ya "umilikishi" kwamba kwa vile tu ni mpenzi wako basi hutaki awe karibu na mtu yeyote....yaani ni marufuku hata kwenda kwao, shughuli zote za kutoka unazifanya wewe kwa vile unahofia watu wengine watamuona na kumtamani....wengi huita wivu, lakini kiukweli sio wivu ni kuwa "obsessed".

Kila la kheri.

*Samahani L inagoma-goma kwani mwanangu kaing'oa hivyo nahitaji kubonyeza kwa nguvu na mie nasahau kutokana na mwendo wa haraka wa kuchapa.....

No comments:

Pages