Friday

Mchumba ananichanganya...

Pole na kazi.
Naomba ushauri juu ya hili lililonitokea. Nina Mchumba na ninasoma nae Chuo kimoja, tumeshapanga mambo mengi lakini nimekuja kugundua amenisaliti kwa kutembea na mtu mwingine.


Nilipomuhoji alilia sana akanambia amepitiwa na muda huo akachukua simu na kumpigia yule Mvulana na kumwambia kwamba hataki mawasiliano nae tena.


Hilo halikuniridhisha, ilipofika asubuhi nikawaita marafiki zake na marafiki zangu na pia nikamwambia amuite yule Mvulana. Nilivyo muhoji yule Mvulana akasema hakuwahi kuwa nae kimahusiano na akakataa kabisa.

Mchumba wangu yeye anakubali ila anasema mbele yetu kwamba ananipenda Mimi na akahaidi kutorudia. Aliona hiyo haitoshi akabadili namba za simu na kila muda anaomba msamaha. Rafiki zetu walitushauri tusameheane ila niendelee kumchunguza.

Je, wewe unanishaurije?

**********


Dinah anasema: Ahsante, shukurani kwa ushirikiano.


Mmechumbiana kienyeji/kimjini-mjini au kwa kufuata taratibu zote za kutambulishana kwenye familia zenu, Umetoa Posa na kutoa sehemu ya Mahari?

Kama mmechumbiana kienyeji hakuna haja ya kuendelea kuwa nae, ikiwa upo nae hapo Pua na Mdomo (Chuoni) ameshindwa kuwa muaminifu kwenye penzi lenu sasa mkiwa mnafanya kazi sehemu mbali-mbali (Mikoa tofauti) si ndio ataolewa kabisa?!!

Kuna issue za kuhusisha marafiki lakini sio hii(mnajitia aibu tu). Kumuweka kati mwenzenu (yule kijana) na marafiki zenu inaogopesha....hata ingekuwa mie ningekana kwa Nguvu zote.

Kubadilisha namba sio kielelezo kuwa hana uhusiano na mwanaume aliekusaliti nae....kumpigia simu na kumuambia hataki mawasiliano nae haina maana anamaanisha kwa huyo kijana.

Kumbuka kuna wake/waume wanafanya affair wakijua kuwa wao ni "wezi" na wanafurahia kuwa wezi....hivyo huelewana na "muibiwa" na kukufanya Fala ili waendelee kuibana....sijui unanielewa?!!.

Umeelezea tukio zima lakini hakuna mahali umeweka wazi hisia zako juu ya Mchumba wako tangu hayo yote yatokee. Wewe kama wewe unajisikiaje? Unataka kufanya nini kuhusu uhusiano wenu.


Fuata Moyo wako lakini usisahau akili yako nyuma....Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Thursday

Ataka Ndoa, mie nasoma.

Mimi nikijana umri wangu miaka 24, ninamchumba wangu ninampenda sana na tumedumu kwenye uhusiano huu ni mwaka wa Nne but hatujawahi kukutana kimwili maana ndivyo alivyo niomba hadi ndoa.

Mimi bado niko Chuo ila mwenzangu hakufanikiwa kuendelea na Masomo sasa yuko nyumbani kwao. Juzi kamtuma rafiki yangu akidai anahitaji kuolewa kwani amechoka kunisubiri.

Kila nikimpigia simu anadai yuko bize yani kiufupi anaona kama ninamsumbua. Ninampenda sana ila mwenzangu ndio kashaanza vituko please nisaidie dada dinah.

*********


Dinah anasema: Unamiaka 24 na uhusiano wenu unamiaka Minne which means mlianza mkiwa watoto....tusema alikuwa 17 na wewe 20.


Well, sidhani kutopokea simu au kusema yupo busy ni vituko. Huenda kweli yupo busy akijipatia "uzoefu" wa maisha baada ya shule. Ila wewe unajishtukia ukidhani unamsumbua (huenda kweli ni msumbufu) sio kila mwanamke anapenda kuwa checked on kila saa.

Katika hali halisi, kama ni Mchumba wako ni wazi kuwa Unajulikana kwao na yeye anajulikana kwenu, umetoa Posa na seheme ya Mahari au Mahari yote si ndio?.


Sioni sababu ya kwanini Mchumba wako kumtuma rafiki yako kukufikishia ujumbe badala ya kutumia Wazazi/Mshenga wako via wazazi wake au kukuambia moja kwa moja. Unless mnaitana Muchumba kufurahisha nafsi zenu kuwa uhusiano wenu ni serious, kwamba hamjakamilisha taratibu za Kuchumbiana.

Binti atakuwa na miaka 24 au mdogo zaidi, akili yake na mtazamo wake na hisia zake hazifanyi kazi kama alivyokuwa miaka 4 iliyopita, amekuwa kwa kiasi fulani, si msichana tena bali ni Mwanamke.

Huenda sasa (since hasomi) anadhani ni wakati muafaka wa yeye kuolewa na tayari kuna "wachumba" wanataka kuoa leo-kesho.


Kutokana na maelezo yako ni wazi anakuambia mfunge Ndoa haraka au umuache aolewe na mtu mwingine kwani amechoka kukusubiri.


Kufunga ndoa kwavile unampenda mtu ni vizuri, lakini hamuwezi kulipa bills na kula penzi lenu, mtahitaji pesa kutimiza hayo.


Kutokana na umri wako na bado unasoma nisingekushauri ufunge Ndoa mpaka ujiweke sawa Kimaisha na Kiuchumi.


Kaeni chini mzungumze tena na ku-review options zenu (kama zipo) kiuchumi sasa na baada ya ndoa(kama mtaamua kufunga)....mkishindwa kuelewana pelekeni issue yenu kwa Wazazi wenu na kama vipi vunjeni Uchumba.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Sunday

Kaikataa Mimba...Mie naitunza!

Shikamoo dada Dinah, hongera na kazi yako nzuri. Samahani dadangu mie ni binti nina miaka 22, nasoma College mwaka wa Tatu nategemea kumaliza Mwezi wa Nane.


Nilikuwa kwenye uhusiano na mwanaume kwa miezi kama mitatu. Siku tuliyosex kwa mara ya kwanza ndio siku nikapata Ujauzito, hiyo ni baada ya kupima ndani ya wiki Mbili.

Shida ni kuwa home Wazazi ni wakali ile mbaya na wakijua kifatacho ni
kunitimua nyumbani na mwanaume huyo ananambia kuwa hayuko tayari kuwa baba kwani hakujipanga.


Mwanzoni niliumia sana lakini nikajitahidi kulichukulia suala langu kawaida ili lisiniathiri katika masomo, hivi sasa nina Mimba ya wiki 4 na kila mara naambiwa kuwa kama ningetoa ingekuwa best.


Mie kutoa sipo tayari sababu naamini kiumbe hakina makosa, wenye makosa ni sisi, naomba mnishauri kitu kimoja kuhusu huyu mwanaume.


Yeye hajaukubali huu Ujauzito na hilo linamuathiri katika kazi zake na anasema mipango yake imevurugika. Nataka nimsaidie Kisaikologia ili aone ni tatizo dogo na aweze kufanya mambo yake hata kama hatonipa support mimi na mtoto.


Naombeni mnisaidie.

*************


Dinah anasema: Marhabaa Binti, Ahsante kwa ushirikiano.

Sasa na wewe ilikuaje ukangonoana na mtu kwa mara ya kwanza Bila kinga ukijua wazi utashika Mimba na hivyo kutimuliwa kwenu?


Ndani ya hiyo miezi mitatu ya "uhusiano" wenu mlikuwa mnafanya nini au mnazungumza kuhusu nini? Maana inaonyesha hamkulizungumzia suala la "je nikishika Mimba tutafanya nini?" na mengine Muhimu mkakimbilia kutiana tu....watoto wa leo MNATIA HASIRA! Anyway....limetokea hatuwezi kubadilisha but I had to say that.

Aliekuambia Mimba ni tatizo dogo alikudanganya. Mimba na baadae Mtoto ni Mabadiliko Makubwa sana kwenye Maisha ya mwanadamu na hakuna "going back".

MOSI....Wacha kupoteza muda na nguvu kumsaidia mwanaume aliekuwa TAYARI kufanya Ngono Bila kinga lakini HAYUPO TAYARI kuwa Baba. The shenzi kabisa.

Mimi pia sitopoteza Muda wangu kukushauri nini cha kufanya ili kumsaidia huyo Kijana wakati wewe ndie uliebeba Mzigo, Nyumbani kuna Utata na ndio utakae zaa kwa Uchungu.


Wachaa ateseke Kisaikolojia na ikiwezekana afukuzwe na kazi ili apate robo ya robo ya Machungu utakayokumbana nayo kama Single mother.

Au unadhani ukimsaidia atajirudi na kukubali Mimba ili muendelee na Uhusiano?! Tunza nguvu zako kwani utazihitaji sana ndani ya Wiki 8 zijazo na siku ya Kujifungua.

Sasa nakupa Ushauri ambao hujauomba! Focus....woman Focus....kama umeamua kuutunza Ujauzito usitegemee sana kuwa huyo Jinga siku moja atarudi na kukuoa (akirudi tutajua then)....kwasasa tengeneza Mazingira Mazuri kwa Wazazi wako na Mtoto utakae mzaa.

Anza na Mama yako na uanze kwa kuomba Msamaha kisha umpe picha kamili....Mama huwa na namna ya kuwaweka sawa Baba so atasaidia kukufikishia ujumbe.

Hakuna Mzazi atamchukia mwanae kwa kukosea (kosa Kubwa na la kijinga)....wazazi wanapokuwa wakali kwetu ni kwasababu wanatutakia Mema, hawataki tuwe na majukumu Magumu kabla ya Umri (chini ya Miaka 25).


Napenda nikuhakikishe, pamoja na ukali wa wazazi wako bado watakukubali na kukupa support(hasa Mama).


Pamoja na kusema hivyo tegemea kufokewa na kupokea kila aina ya matusi kisha huruma au kilio na huruma kisha kufokewa au kutukanwa.


Maliza Masomo yako salama, Lea Mimba yako, Omba Mungu akulinde na ujifungue salama kisha Tafuta kazi/shughuli ya kukuingizia Kipato....lea Mwanao.

Mwanao akikua atamtafuta Baba yake...

Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Thursday

Mume ajali Rakize badala ya Familia yake...

Hongera kwa kazi nzuri rafiki, Naomba ushauri. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30.

Nmeolewa(Bomani) na nina mtoto wa miaka 4(ke) nathubutu kusema tangu nianze kuishi na huyu Mume sina kumbukumbu yeyote ya siku niliyowahi kufurahi nae (kutoka au kushea furaha).


Kutoka ni labda Msiba ukitokea tena upande wake ndio atakuambia kuna Msiba uende ila sio kwetu. Hana habari na ndugu zangu lakini anataka mimi niwahudumie nduguze.


Anawatoto wawili aliozaa na wanawake wawili kabla yangu na wote naishi nao kwasababu Mama zao walikuja kuwabwaga na hawajihusishi na lolote kuhusu watoto wao.


Tukipanga mipango ya maendeleo na kuelewana vizuri lakini hela ikipatikana anabadilika na kukuambia kuna rafiki yangu kaniomba kiasi cha pesa siwezi kumnyima.

Ukiuliza zaidi utaishia kugombana tu. Yeye ni mkali sana ukiuliza kitu kidogo anawaka.

Kunawakati aliniambia kuna dada ambaye ni Yatima anashida sana anaomba aje kukaa kwetu. Nkamwambia hali yetu ni mbaya kiuchumi hatutaweza kumhudumia wakati huo nilikua Chuo na nyumbani tulikua na mdogo wake (Wifi) tukakubaliana.

Siku ya siku akaniambia anaenda kumpokea msichana wa rafiki yake kwani huyo rafikie amemuomba kwani yeye hana nafasi, sikua na wasiwasi. Siku zikazidi kwenda kila nikimuuliza hanipi jibu linaloeleweka.

Wakaanza tabia ya kupiga stori hadi saa tano za usiku, binti akaanza kujiachia nyumbani yaani hafanyi kazi yoyote. Siku nipo Chuo Wifi akanipigia akanambia nimefanya fujo nyumban, huyu binti haeleweki nimemuuliza kaka kama ni mke wa pili aseme tujue lakini hakujibu!

Baada ya fujo za Wifi Mume wangu akamuondoa nyumbani na sijui alikompeleka.


Akaja mdogo wangu kwa lengo la kurudia masomo, tukawa tumekubaliana kumsaidia. Mara nikasafiri na niliporudi Mdogo wangu akanambia hataki kusome tena. Nikamuuliza mume kulikoni? akanijibu mkato achana nae hataki kusoma!!


Siku moja asubuhi akaamka mapema kwenda kuoga, muda ukawa unaenda nikatoka chumbani kimyakimya kujua kulikoni. Nikaenda bafunu, chooni hayupo! Ikabidi nisimame Koridoni kuona atatokea wapi?

Baada ya muda naona anatokea chumbani anakolala mdogo wangu, nikamuuliza kulikoni? akanambia alikuwa anachungulia mwizi?!


Ila moyo wangu ulikosa amani kabisa na tangu nimuulize kuhusu kutoka chumbani kwa mdogo wangu tukagombana sana hadi yule mdogo wangu akaondoka. Hivi ninavyokuambia huwa naomba muda tuongee anajibu kuwa amechoka.

Lakini simu zake hata usiku wa manane zikiita ataamka kupokea wakati mwingine hata mkiwa mnaduu na simu ikaita atakuacha akapokee simu.


Juzi ananiambia anataka watoto wanne, nikamwambia atalea nani?maana huyu mmoja kumtimizia mahitaji yake ni ngumu. Hivi hadi leo Ada hajamlipia tangu mwaka uanze achilia mbali mahitaji mengine na hao watoto wake wawili.


Naumia!! sio kwamba hela haipatikani kabisa, ikipatikana lakini yupo radhi kuvunja makubaliano ya familia yake na hutaiona hela yake. Ukiuliza tatizo, ataishia kununa na majukumu ya kifamilia hatimizi kisa kanuna.


Nimkopaji mzuri ila hakushirikishi kwanini anakopa na pesa anazokopa zinakwenda wapi?! Akiba kuweka kwake mwiko, na likitokea tatizo anaanza kupiga simu za kukopa. Marafiki zake wote wamemkimbia hawapokei simu zake.


Ukweli ni kuwa siamini kuwa anaweza kunisaidia kulea watoto wangu anaotaka nizae, hata mimi mwenyewe kunihudumia kama mke hanihudumii achilia mbali mtoto wetu huyu Mmoja.


Sina upendo tena kwake, yaani najilazimisha tu japo kimapenzi ananiridhisha.

Wote niwafanyakazi wa Serikali, Mshahara ukitoka mie nitaleta nyumbani na kama kunamahitaji nimenunua nitamuelekeza lakini wakwake unaishia Mfukoni. Hakwambii chochote zaidi ya nimelipa madeni ambayo sijui alikopa lini na kwanini?

Naomba ushauri ndugu yangu.


************


Dinah anasema: Ahsante na shukurani kwa Ushirikiano.

Jamani!! Ndoa ni uvumilivu kwa maana kuwa unavumilia hali ngumu ya maisha, magonjwa na mabadiliko mengine ya kibinaadamu sio upuuzi kama huo ulioueleza!


Wala tusipoteze muda kujadili uchafu wa tabia na matendo ya Mumeo, hastahili kabisa kuwa Mume wala Baba.

Kwavile huna furaha(hujawahi kufurahia Muungano wenu), huna mapenzi kwake na humuamini tena hakuna sababu wala umuhimu wa wewe kuendelea kubaki kwenye Ndoa ambayo imefikia mwisho.


Miaka 13 uliyoipoteza kwenye Ndoa hiyo inatosha, sasa ni muda wa kuanza kufurahia maisha yako yaliyobaki. Tunafunga Ndoa na watu tuwapendao(most of us) ili kwa pamoja tufurahie Maisha na kujenga Familia na sio kuonewa, kuteswa, kunyanyaswa au kutumiwa.


Ikiwa sasa unamiaka 30 inamaana umekuwa na huyo baba ukiwa mtoto wa miaka 17! No wonder wale ma-ex walikuja kukubwagia watoto na wewe ukakubali. Ungekuwa 30 then sidhani kama ungekubali.


Mie nakushauri utafute namna ya kutoka humo Ndoani. Kwa bahati nzuri una Kipato na inaonekana ni Mwanamke unaejielewa na unaakili, hivyo unaweza kabisa kuendesha maisha yako na mwanao bila yeye.


Kutokana na ukali wake na kukwepa mazungumzo na wewe hakuna haja ya kumuambia kuwa unataka kutengana nae au kumuacha....asije kukutoa roho....maana anajua wazi hakuna mwanamke anaeweza kuvumilia hayo yote aliyokufanyia....achilia mbali kulea,kuhudumia na kusomesha watoto wa wanawake wengine.

Akili kichwani mwako; hakikisha hakuna mtu anajua mpango wako mpaka utakapokamilika na umeisha hamia kwako. Hata mwanao asijue lolote maana miaka minne lazima atakuwa anazungumza vya kutosha....na bila kujua anaweza kuropoka kwa Baba yake ikawa vita.


Kila kitu kikienda sawia, uamuzi ni wako ama kumtaliki huyo "Mfano wa mwanaume" kupitia Mahakama au ukauchuna tu. Ila kumbuka Ndoa ya Bomani ni Ndoa inayotambulika Kisheria hivyo asije akaitumia hiyo baadae kukuharibia uhusiano Mpya.


Kwenye kila jambo unalolifanya hakikisha unakuwa Muangalifu, maana huwezi kujua akilini mwake kuna "madudu" gani.


Sasa anaenda kuwa Baba wa watoto 3 kutoka Mama 3 tofauti, what a mess!! Fanya yote lakini usimuachie/msusie mwanao.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Wednesday

D'hicious leo ni Mwaka wa Saba!

Hongera na Ahasnte kwa kuichagua Blog hii siku ya leo ambapo inatimiza Miaka Saba.









Napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe Msomaji, Mtembeleaji, Mchangiaji na zaidi ni wewe unaenitumia Mwaswali kwa kuamini kuwa nitakupatia Ushauri ambao kwa namna moja au nyingine utasaidia kupanua mawazo yako na hivyo kufanya uamuzi sahihi.











Kwa dhati kutoka Moyoni nasema ahsante sana kwa kunipa nguvu ya kukaa chini na kufikiria nikupe ushauri gani na Changamoto ya nikushauri vipi?











Kuna Baadhi ya Watu hunipa Changamoto kweli kweli, wakati mwingine nashindwa ku-switch off "kichwani" swali/maelezo husika na hivyo kabla usingizi haujanipitia naanza kufikiria namna ya kujibu/shauri.











Kumbuka tu kuwa Ushauri unaotolewa kwenye D'hicious sio sheria, hivyo ni hiari yako kufuata yote, kuacha yote au kuchukua unayodhani yatakusaida kwenye kutatua issues zako.











Mwisho kabisa napenda kusema ahsante kwa my little ones kwa kulala mapema so that I can write this Post.









Mungu aendelee kutupa afya njema, atupe akili na upeo wa kuweza kuona na kukabiliana na issues kwenye Ndoa/Mahusiano yetu ili tuishi kwa Amani na furaha.





Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Mwili unafanya nisijiamini...

Dada/Mama shkamoo mimi ni kijana umri wa kwenye early 20s urefu 6ft  naitwa junior naishi arusha nimekuwa nikiambiwa na my friends kuwa mimi ni handsome na vitu vingine ila sijui tatizo liko wapi.

Nashkuru sana kwa Blog yako ambayo nimekuwa nikijifunza mambo mengi kuhusiana na Mahusiano na vitu vingine vingi.


Nilikuwa naomba ushauri sana sana kutokana na tatizo langu la kutokuwa na self confidence na sometimes nakuwa insecure about my body.


Wakati wa kum-face msichana naeza nkamuona msichana 4 the 1st time na kupenda kujuana nae ama kumuomba no zake lakini nashindwa.

Mimi ni mkimya na mara nyingi huwa naogopa sana kutoswa na msichana kuhofia aibu na pia ninapokuwa katika approaching phase huwa najiona kama sina quality za msichana kunikubalia sababu maybe kwa ajili ya body yangu ama other negative reasons na kwamba siwezi kukubaliwa.

So kutokana na mimi kufikiria hivyo nimekuwa si-participate kwenye relationships meaning I don't care, no feelings no emotions stuffs like that.


Naomba sana ushauri wako kwa kuniambia tatizo langu hasa ni nini? na unanishaurije? Asante.
 
***********

Dinah anasema: Aiii Mama tena?!! Mwanangu mkubwa anamiaka 3 sio 20+....Mdogo wangu wa mwisho anamiaka 21 so yeah I am your Dada hehehehe nani ataka uzee hapa! Ahsante sana na shukurani kwa Ushirikiano wako.


Kama Mwanaume umekuwa "programed" ku-handle kukataliwa bila aibu wala nini....piga kifua jiambie umejiamini na umeweza kutongoza (Baba yako anapaswa kukusaida kwenye hili, mie mkimama hata sijui mambo yenu wakibaba).

Kwenye Maisha yako utakataliwa mara nyingi zaidi kuliko kukubaliwa....ili kupunguza uwezekano wa kukataliwa unapaswa kuwa na uhakika kuwa msichana husika anapendezwa na wewe angalau kwa mbaaali. Jaribu kutengeneza mazingira ya kirafiki zaidi kuliko Mapenzi.

Kuna u-handsome ambao ni Universal (Kama yule Lil Romeo wa MasterP) kwamba kila mtu anakuona "handisamu" alafu kuna ule u-handsome unaotokana au kutegemea na mtazamaji au jinsi mhusika anavyojiweka/jibeba.

U-handsome universal sio kigezo cha kupendwa au kukimbiliwa na wanawake, u-handsome can be boring kwamba mhusika haweki effort maeneo mengine kwavile anajijua yeye yupo "fresh" maeneo ya Usoni.


Alafu kuna wale watu ka' Ali Kiba kwa mfano(I just like the Kid)....sio handsome lakini ni attractive(which can be handsome kwa mtazamaji husika lakini sio kwa kila mtu).


...anajua "kujibeba"....anajua mwili wake ulivyo, anautunza ubaki vile ulivyo na anajua kuuvika/Pendezesha.....anaweza kutoka bila kuchana nywele na kavaa Ndala bado akavutia....haitaji huge effort kuvutia....sijui unanielewa?

Umegusia zaidi ya mara mbili kuwa unadhani tatizo ni mwili wako je, mwili wako ukoje? Urefu wako mbona ni wa kujivunia kabisa!!


Je, unadhani mwili wa aina gani utakufanya ujiamini? Au unadhani wasichana wanavutiwa nao na hivyo kukupa hali ya kujiamini?


Hayo mambo ya Ubora wa kupendwa au kuvutia watu huwa tunajiwekea tu kuvuta muda....Muda ukifika tunajikuta tumedondokea kimapenzi watu tofauti kabisa.....kati ya vibox 10 anaTick kimoja tu hehehehehe Nomaaa! My point is hakuna viwango wala ubora linapokuja suala la Kupenda.

Kuwa na uhusiano wa kimapenzi katika Umri wako sio muhimu kiviiile hivyo badala ya kupoteza muda kutafuta namna ya kuwa na Msichana ni vema kuwekeza Muda wako kwenye kujifunza kujipenda, kujikubali ili upate hali ya kujiamini.

Usipojipenda wewe mwenyewe na kujiweka katika hali ya kuvutia ni vingumu kwa watu wengine kukupenda ama kuvutiwa nawe.

Sote huwa tunavitu viwili-vitatu ambavyo huwa tunakuwa insecure about, haijalishi ni Mzuri kiasi gani, unapesa kiasi gani, akili (academically) kiasi gani au umeumbika vizuri kiasi gani lazima kuna siku utahisi some sort of insecurity. Nadhani ni sehemu ya Ubinaadamu (hakuna aliekamilika).

Utapata vipi hali ya kujiamini?

Tuanze na tatizo kuu hapa ambalo ni "body"....iwe ni mwembamba au Mnene, mazoezi ni muhimu. Mwembamba unahitaji kujaza Misuli na Mnene unahitaji kupunguza Mwili (fat) na kujaza Misuli hivyo fanya mazoezi kulingana na Mahitaji yako.

Kujaza Misuli sio kama Mabaunsa hapana, hiyo wala sio attractive....Misuli kiasi tu ili upate ile V-shape ambayo ukitupia kafulana size ya kati kanakaa vizuri maeneo ya mabegani na kifuani....sio inateremka ka' Blauzi.

Nadhani kuna Blog ya Kibongo
kuhusiana na Mazoezi inaitwa Bryan or something au yeyote unayodhani itasaidia kukupa maelezo muhimu kuhusu Mazoezi kulingana na mahitaji yako.

Muonekano; Hakikisha kichwani ni kusafi....kama ni nywele ndefu basi zipunguze kiasi. Sijui wanawake wangapi wanavutiwa na mwanaume kusuka au rasta....kama unasuka au una rasta hebu badilisha hilo(new start eti).

Mavazi: Badilisha mtindo wa uvaaji wako(style), nenda zaidi kwenye mavazi ya kawaida (casual) lakini yanavutia....achana na trends (Dar combine a.k.a Midosho sort of things). Usivae ili kupata attention(na wewe umo kwenye fashion), vaa ili kuwa Msafi, Uvutie na uwe comfortable.

Vaa Suruali ya kitambaa (nyepesi) only kama unaenda kwenye Mahojiano ya kazi/masomo/kuchumbia vinginevyo wekeza kwenye Suruali "nzito".

Mie sio mtaalam wa Mavazi, nikikushauri kuhusu hilo hapa nitakuwa nakuambia uvae nipendavyo mimi kitu ambacho sio sahihi.

Sasa zoezi hili la kupata hali ya kujiamini likikamilika na ukaanza kujipenda na kuvutiwa na muonekano wako then njoo tuangalie namna ya kunasa wasichana.

Unasoma au kufanya kazi? Kama upo upo tu mtaani basi tafuta mahali pa kujishikiza ili kipato au kujitolea(kusaidia) lakini muhimu ni kupata uzoefu na kuongeza hali ya kujiamini kutokana na kukutana na watu wapya/tofauti na wale uliowazoea kwenye mzunguuko wako (ndugu, jamaa na marafiki).


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Tuesday

Mzito kufunga Ndoa...

Habari Dada Dinah, pole na hongera kwa kazi ya kujitolea unayofanya kuelimisha jamii na kutoa ushauri huru hasa kwa vijana wanaotaraji na walio kwenye mahusiano.

Mimi ni Baba wa watoto wawili niliozaa na mwanamke ninayeishi nae sasa. Tulianza mahusiano toka mwishoni mwa mwaka 2008 baada ya mimi kumaliza Chuo Kikuu na kuanza Kazi ilihali yeye alikua anamalizia masomo yake ya A'level (form six).

Mwaka 2009, alipata Ujauzito wa mtoto wetu wa kwanza hivyo ilinilazimu kwenda kwao kufanya Utambulisho rasmi na kuona nini "way forward". Wazazi wake walinipokea vizuri na wakahitaji tulipe baadhi ya "mali" na tukafanya hivyo na kulipa Mahari kwa kama asilimia 85 hivi.

Kwa sababu alikua amefanya vizuri katika Mitihani yake ya Kidato cha Sita, alipangiwa chuo cha Ardhi hapo Dar es salaam, Wazazi wake walisema hawataruhusu tufunge hadi amalize Masomo ya Chuo Kikuu.

Uamuzi wa Wazazi wake uliniumiza sana. Hata hivyo walimruhusu aishi kwangu bila Ndoa na wakatoa sharti la kuhakikisha anaendelea na masomo bila kuyakatisha. Kwa sababu hata mimi nilipenda asome,niliwaahidi wazazi wake kwamba sitamkatisha masomo.


Wakati akiwa masomoni huku analea mtoto wetu, Nilijitahidi kuona anapata huduma za msingi kumuwezesha kusoma vyema. Hivyo nilimpangia chumba karibu na Chuo, nikampatia Msichana wa kazi na mahitaji mengine muhimu ikiwa ni pamoja na kumtembelea kila mwisho wa mwezi nikitokea Arusha.


Hata hivyo baada ya mwaka wa kwanza, niligundua kuwa alianza Mahusiano ya Kimapenzi na kijana ambaye alikua ni mwanafunzi wa Chuo hicho wa mwaka uliotangulia. Niliumia sana kwa sababu sikujua kwanini anafanya hivo ilihali yeye ni mpenzi wangu na ninajitahidi kumtimizia mahitaji yake kwa kadiri nilivyoweza


Muda wa kufanya field (2010) aliomba na akapangiwa huko kwao Bukoba, hivyo alienda huko kwa ajili ya Field na mwanetu na mdada wa kazi. Nilimshauri aombe mafunzo hayo aje kufanyia Arusha akadai amesha-omba so haiwezekani kubadilishwa.

Masikini kumbe yeye na huyo kijana walikua wamepanga wakafanye Field pamoja ili wapate muda wa kua wote kwa kipindi chote cha Field huko.

Niliona mabadiliko kwenye mawasiliano na ikanibidi kumtumia rafiki yangu wa huko Bukoba ndipo akanieleza kwamba anamuona na huyo kijana most of time.


Fied ilipoisha alikuja Arusha, huku mtoto akiwa na hali mbaya sana na msichana wa kazi aliondoka bila kuaga na aliacha barua kwa moja ya marafiki zangu akiniasa niwe makini na mke wangu kwa maana sio muaminifu na ameondoka kwa sababu hajapenda kuishi na familia yenye hali ya udanganyifu.

Kwa sababu sikujua ameenda wapi yule binti na hakuacha namba ya simu hivyo sikuweza kumpata hadi leo.

Ilibidi nimuweke chini nimuulize kuhusu yale yote na baada ya kum-bana sana alikiri kuwa na rafiki ambae ni mwanafunzi mwenzake lakini alikataa kabisa kwamba hakuwa na Mahusiano naye ya kimapenzi.

Akadai huyo kijana anatabia ya kujikweza anapokua na urafiki na msichana basi yeye anatangazia watu wengine kwamba yupo nae kimapenzi. Aliomba msamaaa na kusisitiza yaishe na ameelewa amekosea nini so atajirekebisha na kwamba hatakua na ukaribu wala mawasiliano na yule kijana tena.

Dada Dinah, mwaka wa Tatu (2012) kama kawaida nilienda kumtembelea mwezi wa kumi na mbili. Nilienda na ajenda ya kumuomba tufunge ndoa ya Serekali ili nipate attachments kwa ajili ya Records zangu kwani nilikua nimetoka Private na kuingia katika ajiara ya Serekali.

Mpenzi wangu alikataa kabisa na kusema anahitaji muda afikirie na awashirikishe Wazazi wake. Hivyo nilimuacha atafakari kwanza.


Nilipokuwa huko nilimnunulia simu mpya na tukakubaliana ile simu yake tumpe zawadi Mama yangu mzazi hata hivyo nilipoondoka nikawa nimeisahau kwa hiyo akaituma Arusha kama Parcel.

Kabla sijampa mama niliweka laini yangu ili niweze kufuta some text na kurestore settings ili isimpe shida mama kuitumia. Hapo nikakuta text za mapenzi na appointments zisizopungua 20 na nilipochunguza niligundua ni namba ya yule kijana.


Nilimpigia simu kumuuliza akashindwa kunikjibu, akadai zilikua ni za zamani sana na hata hivyo hana mawasiliano na huyo kaka siku hizi. Nilimpigia yule kijana kwa hali ya utulivu alinipokea simu yangu na kunitambua kabisa kama Baba____. Nilipoongea nae kwa kirefu akasema ni kweli alikua na mahusiano nae japo mwanzoni hakujua kama ana mwamaume because aliwahi kumwambia haishi na mwanaume.


Yule kijana alikiri kwa sasa hana mahusiano nae kimapenzi bali ni marafiki na yeye ameshamaliza Chuo na ameoa. Tuligombana sana lakini kwa kuwa ulikua ugomvi wa simu, niliona ni busara nimpe nafasi afanye mitihani yake ..then tutayaongea vyema baadae.

Mwaka Jana mwezi wa 8 alimaliza Chuo na ku-Graduate rasmi Novemba 2013 na akaja Arusha tukaanza kuishi pamoja. Nilitafuta muda nikamtoa ili nimuulize kuhusiana na yule kijana. Akasema hana mahusiano nae na zile meseji zilikua za zamani.

Nikamuonesha na tarehe na zille meseji zilivo, akasema hazikua za tarehe hizo, kwa sababu alizimove kwenye phone baada ya Sim Card kujaa so zimerecord tarehe ambazo zilikua moved.

Baada ya hapo ameanza kutaka tufunge Ndoa na ananikera sana na jambo hilo japo nimeshamwambia mie kwa sasa sipo tayari lakini bado ni msumbufu mno.

Wazazi wake wananiuliza pia kuhusu Ndoa? lakini ukweli ni kuwa Moyo wangu unakua mzito mno na naogopa kula kiapo na huyu mwanamke. Nimepoteza hata hamu ya tendo la ndoa kwake..

Dada Dinah naomba ushauri Tafadhali.


**************

Dinah anasema: Habari ni njema sana namshukuru Mungu, ahsante kwa ushirikiano.


Pole kwa yote uliyokabiliana nayo kwa miaka yote wakati Mwenza wako yupo Masomi. Huyo mwanamke nae mchafu wa tabia, hana utu wala shukurani.


Kutokana na matendo yake maovu ya kusaliti uhusiano wenu bila kujali hisia zako wala za watoto wenu ni wazi kuwa humuamini tena.


Uaminifu unapotoweka kwa mtu unaempenda kunakuwa hakuna umuhimu au faida ya kuwa na uhusiano mpaka Uaminifu urudi.


Kwa kawaida aliesababisha Uaminifu kupotea (asiaminiwe tena) ndio hupaswa kufanya jitihada za kurudisha uaminifu huo. Kurudisha uaminifu sio rahisi kama vile "najua nimekosa, sitorudia tena na sitofanya mawasiliano na whoever".


Baada ya hayo yote wala asingekuja kifua mbele kulazimisha Ndoa ambayo awali aliikataa. Nadhani anajua "udhaifu" wako ambayo nahisi ni Upole na huenda unashindwa kumconfront ukiwa firm kutokana na ushahidi ulionao....anacheza na Saikoloji yako.

Anafikiri kuwa amekupata, kwamba anakudanganya na unaamini Uongo wake na ndio maana baada tu ya kurudi kakimbilia kutaka kuolewa.


Nini cha kufanya: Ifanye issue uliyonayo iwe yenu na SIO yako, kwamba kaa na mwezio na uzungumze nae kwa uwazi jinsi unavyojisikia.

Mwambie kwa mf; "kwavile nanyamaza au kukubaliana na Uongo wako haina maana kuwa mimi ni mjinga na sijui nini kilikuwa kinaendelea".

Ongeza; "Kabla ya ushahidi niliokuonyesha unaodai kuwa ni wazamani which inaonyesha usaliti wako kwangu pia kuna watu walikuwa wananipa habari zako".


Mwambie..."Hayo yote yamenifanya nijiulize mara nyingi kama kweli unafaa kuwa mke wangu au la!"......Hayo yote yamenifanya nisikuamini tena na wala sitamani tendo na wewe, nahisi kinyaa...nikikuangalia na-imagine wewe na yule Kijana mnafanya mapenzi, so inani-put off".

Endele; "Nahitaji muda kukuamini tena na wewe unahitaji kunithibitishia kuwa na tabia njema na mapenzi ya dhati juu yangu ili nirudishe hali ya kukuamini na kuvutiwa nawe tena"

Malizia "Kila kitu kikienda vizuri na uaminifu kurudi basi tutaangalia uwezekano wa kufunga ndoa, lakini kwa sasa sipo tayari".


Weka kila kitu cheupe ili ajue unavyojisikia.....aache kujionda bingwa wa kudanganya na kuficha siri kumbe wee unaugulia na ukweli unaujua.

Wazazi wakiuliza kuhusu Ndoa, waambie kuwa wewe na huyo Bibie mna issue zenu mnajaribu kuzitafutia ufumbuzi kabla hamjafunga ndoa.

Wakitaka kujua ni issues gani then waeleze moja kwa moja au via Mshenga(hakikisha ni ana kwa ana, sio simu).


Tangu ulitoa Mali na sehemu ya Mahari na sasa mnawatoto wawili, hakika una haki kuwakilisha issue yenu kwa Wazazi kama wanandoa, japo sio rasmi..

Vyovyote mtakavyoamua kumbukeni kuna maisha ya watoto wawili ambao wanahitaji Mapenzi yenu kama wazazi. Umoja wenu usipofanikiwa basi hakikisheni watoto wenu hawateseki.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Monday

Ubora na Viwango vya Mpenzi!

Hi dada dinah, i have been your follower for quite some time now, though ukaja potea kidogo, naona umerudi and you are doing a good job. I would like to congratulate you for that.


Nina umri wa miaka 26 single and lonely, naomba ushuri kwa hili, nimekua napata shida sana kuanzisha mahusiano ya kimapenzi.


Am not sure whether my standards are very high or else. Currently nakaribia kumaliza my Masters Degree probably this december. Nina kikazi though hakilipi vizuri lakini siku zinaenda.

Natamani kuwa na mahusiano ya kimapenzi ambayo ni serious. Am not very outgoing person, ni mkimya sio muongeaji sana labda hiki ndicho kinachonifanya nisipate ninachokitaka.


Natumaini utanisaidia njia rahisi ninazoweza kutumia ili kuwa interactive mostly with girls. Hope you can keep my email private, thanks for your time.


***********

Dinah anasema: Ahsante sana na shukurani kwa ushirikiano (for being my follower....najihisi ka' Yesu vile hihihihi natania). Yeah nilipotea kwa muda mrefu sana, sikuwa na Muda wa ziada wa ku-blog.

Inawezekana standard zako zipo sky high lakini kutokana na maelezo yako nahisi kama vile ulikuwa/upo busy na Masomo + Kazi. Sasa unakaribia kumaliza unahisi presha imepungua na unaona umuhimu wa kuwa na mtu maishani mwako.

Wengi wetu kwenye umri huo kushuka chini huwa tunajiwekea "standard" na "quality" za watu ambao tungependa wawe wapenzi wetu.

Hivyo "Viwango" na "Ubora" hutusaidia kuvuta muda bila kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi.....kwasababu kila unaekutana nae unahisi hafikii Viwango na Ubora unaoutaka kwa Mpenzi.

Basi unaendelea kusubiri au kungojea hali inayosaidia kuzingatia Masomo/Kazi au chochote unachokifanya kwa wakati huo bila "Can we meet tonight, I miss you" sort of usumbufu.

Lakini katika hali halisi(in reality) mambo hayaendi hivyo unless otherwise uumbe mwanamke/mwanaume wako vile utakavyo nje na ndani.

Sasa unapofikia umri fulani kuanzia miaka 25(kwa wanawake) hivi unaanza ku-settle kiakili unagudua kuwa Viwango na Ubora unaoutaka hauwezi kupatikana kwa mtu mmoja hivyo unaanza kushusha/kupunguza.

Wengine hugoma kushusha/punguza na badala yake hufikia mahali wanakata tamaa(muda umeenda) na kuwa desperate na hivyo kujitolea Mhanga na kujiambia "liwalo na liwe".....ndio maana unaweza kukuta mtu kafunga Ndoa au kazaa na mtu ambae hawaendani kabisa au hawapendani ila desperation imepelekea iwe hivyo....which is sad really!

Anyway....Muhimu ni kupunguza Ubora na kushusha Viwango utakavyo (ulivyojiwekea) kutoka kwa mpenzi mtarajiwa kwani huwezi kuvipata vyote....unaweza kupata 5 out of 12 au 3 out of 8.


Wakati mwingine unapata Viwango au Ubora ambao wewe hukuufikiria mara baada ya kujenga Mahusiano au kuishi pamoja na Mpenzi husika.


Muonekano ni muhimu na kama anatick vibox 2 nje ya 5 sio mbaya vingine utakutana navyo huko huko na kujifunza kuvizoea au kumsaidia kubadilika.


Badili mtazamo kisha ujiulize ni nini hasa unataka au unadhani ni muhimu kutoka kwa Mpenzi....orodhesha vitu vitatu, Mf; (1)Iwe kwenye Muonekano (2)Iwe kwenye Mazingira na (3)iwe kweny Elimu.


Na je wewe uta-offer nini kwake na kwenye uhusiano wenu kwa ujumla ikiwa mtafikia hatua hiyo?.


Je unadhani ni kitu gani unacho(in terms of knowledge) na ukitumie hicho kukamata attention ya mwanamke husika.

Zingatia mazingira uliyokutana na mwanamke husika, anza kwa kupiga stori za kawaida tu bila kuhusisha mambo ya "kisomi"....unless mwanamke mwenyewe aanzishe.


Jaribu kuwa interesting, iwe kwa kucheza, mavazi, simulizi, tabasamu, unavyojiweka n.k.... inategemea na mazingira uliyopo na aina ya watu waliokuzunguuka.


Inaonyesha huna issue ya kujiamini (hivyo unaweza kushawishi mwanamke).....Upole/Ukimya, sio tatizo ni sehemu ya Character yako, inakufanya wewe kuwa wewe(tofauti na wengine).

Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Friday

Kisirani sehemu ya Pili

Acha Uvivu: Kabla hujalala panga kwa kuandika nini kinatakiwa kufanywa siku inayofuata.


Kitu cha kwanza kiwe Mazoezi, natambua sio utaratibu wengi lakini amini nakwambia....Mazoezi huondoa Uvivu/Uchovu, huitaji kwenda Gym, hapo hapo chumbani kwako kunatosha kabisa kuruka-ruka na kufanya push-ups na sit-ups. Kwavile huna mtoto itakuwa rahisi kwako.

Kwa kufuata mpangilio wa vitu ulivyoandika chini jitahidi uvifanye vyote kwa muda uliojiwekea....Mf; kabla ya saa Sita Mchana usafi uwe umemalizika.

Huna mtoto na wala huna ajira hivyo sidhani kama unahitaji Msaidizi, kama uanae muachishe kazi ili ufanye kazi zote humo ndani kama "ajira" yako.


Kisirani/Hasira/Ukali:

Jifunze kujizuia, unaweza kujizuia kwa aina nyingi....ila hizi hutoa matokeo mazuri. Ikiwa kama unamuaini Mungu, Ongea nae, Muombe akupe Amani Moyoni kwani hutaki kujisikia unavyojisikia.


Jifunze kusikiliza na kufikiria kwa wakati mmoja hali itakayokuzuia ku-snap na kutoa majibu kwa hasira.....kama hasira zimekukamata jizuie na utoe jibu fupi bila kufoka au kuonyesha hasira Usoni...

Kama issue inahitaji maelezo marefu, omba muda kujibu, nenda chumbani na ufikirie kilichosemwa kisha rudi na ujaribu kutoa jibu bila kufoka au kukasirika.

Au kila unapohisi hasira zikianza kuja bana/Uma Meno au kunja ngumi, huku umefumba macho na ujikakamue bila ku-move wala kuongea......au hit something kama ukuta au meza....ukiumia utajiona mjinga so hutorudia tena.



Au kila unapokuwa na kisirani, usikae na kuanza kujionea huruma....inuka na hasira zako, nenda kachukue Masufuria masafi na uyasugue kwa kutumia Mchanga mpaka yang'ae.


Ukimaliza bila kupumzika....safisha nyumba yako na hakikisha ni safi na imependeza. Nyumba ikiwa safi kutokana na jasho lako hakika utapata Amani Moyoni na utatabasamu(kisirani nje).


Tamaa/Wivu:

Ni hisia ambayo hujificha au mhusika mwenyewe huificha kwa vile ni aibu kusema kuwa unamuonea wivu (as in envy) au tamani maisha ya rafiki yako/ndugu yako/jirani n.k.


Wengi huificha hisia hii kwa kujifanya marafiki, kwa kuonyesha furaha kwa mafanikio yako lakini kumbe Moyoni wanatamani wangekuwa wao (wanajenga chuki).

"Envy" inasababishwa na kutoridhika kwako na maisha uliyonayo au chochote ulicho nacho unadhani hakitoshi na unataka zaidi.....unapoteza Muda mwingi kufananisha maisha yako na ya watu wengine....unafuatilia maisha ya watu au mtu alafu unaishia kuumia au kukasirika/chukia.

Ifunze nafsi yako kuridhika na ulichonacho.....Kila unapoamka asubuhi ukiwa na afya njema, jione kuwa unabahati kwani wenzako muda huo ndio wanavuta Pumzi ya mwisho.


Thamini maisha uliyonayo na yaone kuwa ni unique na hayapaswi kufanana na maisha ya watu wengine kwani wewe na wao ni watu tofauti na muhimu hawana umuhimu kwako.


Andika vitu au mambo uliyonayo maishani mwako ambayo unadhani ulitamani kuwa navyo na sasa unavyo.


Mf:Afya njema (huna magonjwa), Elimu, Ndoa, Mahali pa kuishi n.k. kisha jiulize...ulifanya nini kufanikisha yote hayo na je ni Muhimu kwako?

Kisha andika vitu ambavyo unatamani kuwa navyo sasa na kwanini? Je ni kwasababu unataka kuwa sawa na fulani au kumshinda?.....unapata faida gani kujilinganisha au kushindana na huyo fulani? Je, ni muhimu kwako kuliko Ndoa yako?


Kujiamini; Uzuri hauna uhusiano na kujiamini au kutojiamini. Mimi si Mzuri lakini najiamini asikuambie mtu hihihihihihi. Anyway....


Kujiamini kunatokana au kunasababishwa na malezi ambayo yalikuwa Chanya kutoka kwa wazazi au walezi.

Kama watu hao walikuwa ni watu wa kukukandamiza, simanga au kukufanya ujihisi huna umuhimu au "not good enough" kwenye lolote then hali ya kujiamini hupotea kwa sababu umeaminishwa kuwa wewe si "good enough".


Sasa ukiendelea na Kisirani/Hasira, Uvivu na mengineyo hata mumeo atakuona kuwa si "good enough" kama mke....hivyo ni muhimu kurekebisha hayo hapo juu ili kupata au kurudisha hali ya kujiamini.

Anza kuwa Chanya (Positive) na fikiria kitu cha kufanya kila siku ili uhisi kufanikiwa. Mf; jitolee kusaidia wengine....tembelea Hospitali/Wodi ya watoto na Usaidie kwa lolote linalohitajika na wewe unauwezo wa kufanikisha.

Sio lazima usaidie Wodi nzima, unaweza saidia mtoto mmoja kwa kitu kidogo kama Dawa ya kupunguza maumivu.....utakuwa umefanikiwa kufanya jambo "chanya" la kuondoa maumivu ya mtoto husika....ni mfano tu.

Itumie Elimu yako kusaidia wengine, umesema hufanyi kazi, Unaonaje kama ukiitumia Elimu yako kujitolea kufundisha watoto kusoma vitabu(soma nao).....watoto hao wakijenga utamaduni wa kujisomea Vitabu utakuwa umefanikisha jambo ambalo ni Chanya.

Kufanya hivyo pia kutakupa nafasi ya kukutana na watu mbalimbali na hivyo taratibu kuanza kujenga hali ya kujiamini na kuondoa Uoga/Aibu ya kukutana au kuwa mbele ya Watu.

Kila unapopata Changamoto, usikasirike au kujiona kuwa umeangushwa na badala yake tafuta namna ya kukabiliana na changamoto hiyo ili ushinde ki chanya zaidi.


Toka na mumeo mara kwa mara bila kujumuika na Marafiki bali ninyi wawili kama wapenzi, hakikisha mnakaa mahali ambapo sio "romantic" yaani penye mwanga mdogo.


Kaeni mahali ambapo watu wengine wanawaona kwa uwazi....sina maana kuwa ujionyeshe la hasha! Bali utakuwa mbele za watu wengine na hiyo itasaidia kukujengea hali ya kujiamini.

Ngoja niachie wengine wajazilizie niliporuka au kosea.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Kisirani sehemu ya Kwanza!

Shikamoo dada Dinah, Pole  na majukumu dada na asante sana kwa kutuelimisha kupitia blog yako hii.
    

Mimi ni msichana mwenye miaka 25 sasa nimeolewa miezi kadhaa imepita bado hatujapata mtoto, naifurahia sana ndoa yangu.
 


Tatizo dada Dinah ni mimi mwenyewe Mume wangu hana shida kabisa. Yaani sijielewi nimekuwaje maana  nina  katabia ka Kisirani.


Nakasirika bila sababu mume wangu anaweza akanisemesha kitu namjibu kwa hasira mpaka ananishangaa. Sio kwamba simpendi nampenda sana.


Sometimes nina Kisirani hadi kwa ndugu zangu, nanuna bila sababu sina furaha Moyoni sijui ni Wivu au ni nini?


Natamani kuacha hii tabia lakini najikuta nairudia tu. Halafu nina hasira za haraka sana mume akiniudhi tu kidogo nakuwa mkali sana.

Halafu uvivu usiseme kuamka asubuhi ni shida nashindwa kabisa na sina kazi nipo tu nyumbani nahisi nina mkera sana ila hasemi.


Nataka niishi kwa furaha kama wanawake wengine wanaojiamini maana mimi sijiamini kabisa kwa lolote then ni muoga sana hata kupita au kukaa mbele za watu ni shida.


Mume wangu ananishangaa sana kwa uoga nilionao natamani nibadilike lakini nashindwa. Naomba unishauri dada Dinah nianze wapi niachane na hizi tabia kwani zinamkera mume wangu sana.


Halafu msimamo ndio kabisa sina kabisa nipo nipo tu.Nashindwa kujisimamia mie mwenyewe nabaki kuiga na kutamani mambo ya watu.


Msaada wako dada Dinah utaokoa ndoa yangu changa kabisa na pia utanifanya niishi kwa amani bila mateso moyoni mwangu kwani ni mtu ninaetamani kubadilika.
    

Kusoma nimesoma na nina Elimu nzuri kabisa. Namshukuru Mungu kwa kweli mimi ni mrembo sijisifii ila ni ukweli hivyo tabia kama hizi mfano za wivu, chuki zisizo na sababu, pia kujali mambo ya watu sijui vinatoka wapi.

Ahsante dada Dinah.


**********


Dinah anasema: Marhabaa Binti, shukurani kwa ushirikiano.

Nahisi kama vile unatatizo la Kisaikolojia linalonifanya nipate maswali haya.....Je, umewahi kunyanyaswa/teswa kwa aina yeyote ile ulipokuwa Mtoto/Shuleni?

Je, uliwahi kuugua sana enzi za utoto wako?

Je, umelelewa na wazazi wako wote wawili au ulikulia/lelewa kwa ndugu au Mzazi mmoja ambae sio wa Damu?


Wewe ni wa ngapi/mmezaliwa wangapi ulipata attention sawa na wadogo/wakubwa zako au unahisi wao walipendelewa? Hebu rejea nyuma na ujitahidi kukumbuka kisha rudi tena kwangu.


Yote uliyoeleza ni tabia ambazo husababishwa na hisia zenye maumivu kutokana na maisha yako ya nyuma, kuna uwezekano mkubwa kabisa hukujua kama uliumizwa/umia na ulichukulia au bado unachukulia ilikuwa hali halisi.


Ukali na Kisirani ni dalili ya "kujilinda" kabla hujawa attacked.....Mf; ukiamka tu umenuna ni wazi kwamba Mumeo hatotaka kukuudhi kwani tayari umeudhika....hivyo kama alitaka kuzungumza na wewe kuhusu jambo lililopelekea "kisirani" chako, hapati nafasi hiyo.


Vilevile kwasababu unajijua ulivyo na hupendi kuwa hivyo lakini unashindwa kujizuia. Inaonyesha wazi kwamba unahofia au hutaki kuambiwa na watu wengine kuwa tabia yako ni mbaya....hivyo ili kuwapiga stop....unajihami kwa kuwa Mbogo (Mkali) so hakuna atakae sema chochote.

Suala la kutokuwa na Msimamo sina uhakika unamaana gani! Mf; "Msimamo wangu ni kuzaa baada ya kuolewa"...."Msimamo wetu ni kutotumia ovyo pesa mpaka nyumba iishe"....

Wanawake wengi hawana misimamo au kama wanayo basi huibadilisha mara kwa mara....ndio maana kuna msemo kuwa "I am a woman and I am allowed to change my mind".

Kutokana na maelezo yako ni kwamba unatamaa, unatamani kuishi kama watu wengine au kuwa na vitu kama fulani...!!


Suala la uvivu nikiliunganisha na maelezo yako ya awali nadhani linasababishwa na hali ya kutothamini au ridhika na Maisha uliyonayo.....hivyo huoni sababu au umuhimu wa kujituma na kufanya shughuli yeyote iwe ndogo au kubwa hapo nyumbani.


Pamoja na kusema hivyo haina maana utakuwa hivyo Daima milele. Kwavile upo tayari kubadilika basi itakuwa rahisi. Hautobadilika ndani ya wiki au mwezi lakini utabadilika tu kama nia unayo.


Kitu muhimu ni kutambua kuwa wewe ndio mwenye uwezo na Control ya kumbadilisha Wewe, hakuna mtu atakae control au kubadili msimamo wako, bali wewe.


Hakuna atakae kuondolea Kisirani, bali ni wewe mwenyewe. Hakuna mtu atakaekuondolea hali ya Uvivu bali ni wewe mwenyewe. Hakuna mtu atakaekupa amani Moyoni, bali ni wewe mwenyewe.

Nitarudi na sehemu ya Pili nikushauri ufanye nini ili kuondokana na tabia hiyo.

Mapendo tele kwako...

Monday

Mke wa Pili, hanijali kwa hela wala penzi.

Habari dada Dinah, pole na kazi na hongera kwa kazi unayoifanya.

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka kadhaa, nimeolewa ndoa ya mke wa pili na mume wa kiislamu huu ni mwaka wa pili sasa.


Tumezaa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka minne sasa. Cha kushangaza dada Dinah sitambuliki kwao mume wangu na wala mtoto wangu hajulikani.


Ndoa yetu ilikuwa ya siri hakukuwa na sherehe yoyote zaidi ya Sheikh tu na mashahidi aliokuwa amewatafuta huyo Sheikh.

Hela ya matumizi ni shida na hata haki ya Ndoa kama mke mimi siipati kwasababu halali kwangu na hata kuja ni kwa kubeep tu.

Sasa naomba ushauri huyu mwanaume ana malengo na mimi kweli au ananipotezea wakati na kunizibia rizki mimi.


***********

Dinah anasema: Nashukuru na ahsante kwa ushrikiano.


Sasa mrembo mbona jina lako la Kikristo ilikuaje ukakubali kufunga Ndoa ya Kiislamu achilia mbali kuwa mke wa pili kwa siri!!....Au ulilazimisha ndoa baada ya kuzaa na huyo Mume wa mtu?


Kutokana na maelezo yako nadhani wewe ni Kimada wa huyo Mume wa mtu, sio mke wa pili kwake kama ulivyojiaminisha.


Kufungishwa Ndoa na Shekhe haiweki uhalali wa Ndoa yako ikiwa taratibu nyingine hazikufuatwa. Pia kutokana na Ugumu wa Maisha wengine wala sio Mashekhe bali "wafanya biashara".


Sizijui sheria za Dini ya Kiislamu lakini nadhani kabla ya kufunga Ndoa Mke mkubwa na watoto wa ndoa ya kwanza hupewa taarifa na kuna sheria lazima zifuatwe.


Pia mume mtarajiwa huenda kwa mwanamke kuposa na kufuata taratibu zote muhimu za Uchumba.

Mara nyingi Wake wenza huishi nyumba moja au mahali pamoja, na ikitokea mahali hapatoshi au mke Mkubwa hataki ukae nae basi mke mdogo hutafutiwa mahali pengine.


Mume "wenu" hujigawa "sawa sawa" bila upendeleo kwa wake zake wote. Mke mdogo hujulikana kwenye familia nzima mpaka wale wa ndani ndani kule (wasio na uzito).


Sasa kama mwenzangu hayo yote hayapo na Ndoa ilifungwa kwa SIRI bado unaamini tu kuwa wewe ni Mke wake na sio Kimada?!!


Kwabahati mbaya sidhani kama kuna Sheria inayokulinda ili kupata "matunzo" kwa ajili ya mwanao. Huwezi kwenda Mahakmani wala Ustawi wa jamii kuomba msaada kisheria kwasababu huwezi kuthibitisha uhalali wa Ndoa yako.


Labda kama una Cheti cha Kuzaliwa chenye jina na sahihi ya Baba'ke mtoto, ila mzunguuko wake lazima ukate tamaa (kutokana na nature ya uhusiano wako na Mume wa mtu).


Usijutie kosa lako ila ujifunze kufunga miguu mbele ya wanaume wenye wake na familia zao in the future, Uislamu sio sababu ya kumkubali Mume wa mtu hata kama wanakuahidi Ndoa, kataa.


Kosa kubwa ulilofanya ni kuzaa na huyo mwanaume, matokeo yake mnamtesa mtoto ambae hakuomba kuzaliwa na mume wa mtu ambae sasa ni baba yake au wewe.

Hakupotezei Muda bali ameisha kupotezea Muda wako, hakuzibii rizki (hakuna mwanadamu anaweza kukuzibia rizki), nadhani kagundua familia yake na mkewe wanaumuhimu zaidi yako ndio maana anabeep au kuna Mke wa tatu wa siri huko kwingine.

Hama hapo ulipo, tafuta kazi au shughuli ya kukuingizia kipato.....mwanzo utakuwa Mgumu sana lakini ukisimama kama mwanamke na ukajitahidi utafanikiwa tu.


Baada ya kukaa sawa na mtoto kakua then unaweza anza kutoka tena, zingatia ulichojifunza kutokana na kosa lako la mwanzo.


Utakapo anza kutoka tena na mwanaume hakikisha hana familia na pia usikimbilie kuzaa, tumia kinga kwa faida yako na mtoto wako.

Mtoto akikua atamtafuta baba yake....(Kama atataka hilo litokee).

Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Sunday

Ningependa kuolewa ila naogopa...

Hello Dinah, Pole na majukumu ya kila siku. Samahani usiweke jina langu.

Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 28. Sijaolewa ila niliwahi kuwa na
uhusihano wa kimapenzi ambae alikuwa wa kwanza kwa muda wa miaka 3.

Mimi na Mpenzi tulipanga kufunga Ndoa nikiwa na miaka 25 na alikuwa
amejitambulisha nyumbani lakini kabla ya kufunga Ndoa alitaka
tushiriki tendo, nilikataa nikaomba tufunge Ndoa kwanza.


Chakushangaza alikataa katakata akasema hawezi kuoa mke
ambaye 'hamjui'. Baada ya kunipata ndiyo siku aliyoniacha.


Baada ya mwaka mmoja nilikutana na mwanaume mwingine niliyempenda
sana. Tulipoanza tu mahusiano akawa anataka ngono kwanza lakini Mimi
sikuwa tayari kutokana na mambo yaliyonitokea awali sikumweka wazi
kuwa sitaki ngono kabla ya Ndoa kwani pia tulikuwa na malengo ya kuoana.


Kadri siku zilivyoendelea aliacha kunigusia suala hilo la ngono na kuniambia anaheshimu maamuzi yangu.


Nilizidi kumpenda sana na hakuwahi kunibadilikia hata siku moja. Tukiwa kwenye harakati za kutambulishana, kukawa na send off ya rafiki yangu kwa Bahati nzuri nikakutana na mwanaume wangu akiwa na Mkewe


Tangu kipindi hicho nilichanganyikiwa na kujikuta nachukia wanaume na
sitamani kuolewa tena wala kuchumbiwa.


Nimeshatembelea Hospitali
nakufanyiwa councelling na kutumia dawa za kuondoa stress lakini Moyo
wangu umeshindwa kuamini wanaume tena!


Naomba unisaidie Dada Dinah maana umri unazidi kwenda na hili janga linanizidi kila nikisikia mwanaume anagusia Ndoa kwangu.

**************

Dinah anasema: Hi! Ahsante na shukurani kwa ushirikiano, usitie shaka kwa kawaida huwa sitoi majina.


Sikuwahi kutendwa bali nilikuwa nachukia au niseme NAOGOPA Ndoa.....yaani mtu akigusia tu na Uhusiano unaishia hapo (natoka mbio na siangalii nyuma) nadhani nilikuwa too "academic" a.k.a Msongo....anyway!

Nadhani tatizo hapo ni Muda(Akili/Moyo bado haujapona), ulitoka kwenye uhusiano wa kwanza na ulikuwa wa muda mrefu na mwisho wake ulikuwa wa "kudhalilishwa" na maumivu....in which ulikupa maswali mengi yasiyo na majibu.

Tatizo lingine ni Imani yako juu ya Ndoa na hofu ya kuzeeka bila kuolewa, jiulize; Kwani nini umuhimu wa Ndoa maishani? Na Je hata nikiwa kwenye ndoa siwezi kutendwa ikiwa mume atakaenioa si mwaminifu?


Ndoa sio guarantee ya kufurahia maisha yako.....kwenye maisha kuna mengi ya kufurahia zaidi ya Ndoa, enjoy maisha yako, jiweke sawa Kiuchumi alafu ukifika 30s huko ndio uolewe.

"Maumivu ya Moyo hayapoi kwa Ganzi", maana yake hayahitaji Hospitali wala Dawa za kupunguza stress (ukizoea utakuwa mtumwa wa dawa hizo) na zitakupa wehu.


Unahitaji Muda nje ya mahusiano ya kimapenzi, Familia (watu wakaribu wanaokupenda na kukujali) aka support system.

Pia, Unahitaji kukaa mwenyewe kwa muda mrefu zaidi ya Mwaka mmoja, piga miaka miwili au mitatu ya "single, happy and free", kula na furahia maisha yako kama mwanamke.

Alafu baada ya hapo anza tena kutoka au kujenga uhusiano wa kimapenzi wa "kurudisha imani"....kwamba mpo serious na penzi lenu na mnafurahia bila kupeana presha za kufunga Ndoa.

Mwaka mmoja kuingia tena kwenye uhusiano "serious" ilikuwa kosa, napengine hukuwa na mapenzi kwa huyo "Mfano wa mume" bali upweke, hali ya kupoteza kujiamini na ulikuwa "vulnerable" kihisia baada ya kuumizwa. Hali hiyo ndio ilikufanya UDHANI anakupenda na wewe unampenda.


Kumbuka sio kosa lako wanaume hao kuwa na tabia walizo nazo, chukulia kuwa wanamatatizo ya akili na wanahitaji matibabu au wamesahau kula dawa zao.


Songa mbele na ufurahie maisha yako bila kuhofia suala la Ndoa, muda ukifika (ukiponyeka) utapenda, utapendwa na mtafunga ndoa. Unamiaka mingine kama 40 hivi kabla hujazeeka.


Kila la kheri Mrembo.

Mapendo tele kwako...

Tuesday

Kiburi na dharau ya Mke...

Habari dada Dinah, hongera kwa majukumu. Mimi ni kijana wa miaka 36 nimeoa na nina watoto wawili.

Wakati naoa dada Dinah nilifurahia sana maisha yangu ya ndoa lakini sasa dunia
imenigeuka, sifurahii hata chemba ndoa yangu.

Tatizo lilianza hivi; mwanzo mke wangu hakuwa Mtumishi wa Serikali hivyo niliamua kumsomesha Sekondari. Baada tu ya kupata kazi alibadilika na kusahau majukumu yake kama Mke.


Kwani inafikia mahali anadai hivi sasa
simbabaishi kwani anamshahara na kazi yake. Sasa Dinah najiuliza je ndoa
zote za Watumishi ndivyo zilivyo au ni hii ya kwangu tu?

Nifanye nini kunusuru ndoa yangu maana nahurumia watoto wangu kwani first born wangu ana miaka 9 tu.Sitaki kushutumu upande mmoja tu pengine hata mimi nina mapungufu lakini nimejaribu kushauriana nae lakini amejawa jeuri na
dharau.


Naomba ushauri wako dada.


********************


Dinah anasema: Hakika nahitaji Hongera ya majukumu maana sio lelemama. Ahsante sana kwa ushirikiano.

Hapana! Sio wanawake wote wanaofanya kazi nje ya nyumbani huwa wajeuri na wenye dharau.

Nadhani uoga wa mwanaume kuwa na mke anaejitegemea kiuchumi na mwenye sauti kwenye maamuzi muhimu kwenye uhusiano humfanya adhani kuwa mkewe ni mjeuri au hamheshimu tena.

Ila mwenzangu maelezo yako yamekaa kibinafsi mno utadhani Mkeo hausiki kwenye Ndoa hiyo, "ndoa yangu"....."Watoto wangu", "first born wangu"....umajaa Umimi ambao unaweza kuwa tatizo kutoka upande wako, jaribu "Ndoa yetu", "Watoto wetu" "firstborn wetu".

Kwaharaka haraka ningesema kuwa tatizo la mkeo ni...ULIMBUKENI. Lakini kutokana na maelezo yako umesema kuwa "anadai sasa hivi humbabaishi kwani anakazi na mshahara wake"......

Hiyo inaonyesha kuwa umewahi kumbabaisha au hata kumnyanyasa kwa vile hakuwa na kipato. Hebu rejea huko nyuma na uangalie matendo yako dhidi yake yalivyokuwa.

Wakati mwingine binadamu tunafanya mambo bila kujua au kutilia maanani kwavile ni madogo (not big deal kwetu) na wenza wetu wakikaa kimya basi ndio limepita hilo(hujui kama ulikosea).

Ukweli ni kuwa huwa yanabaki kwa muda mrefu mpaka mwenza wako atakapo pata namna ya kuliweka mezani ili lizungumzwe na hapo umuhimu wa mawasiliano hujitokeza kwenye uhusiano.

Nirudi kwake sasa; Wanawake wengi wameaminishwa vibaya kuhusu suala la "Usawa" na "kujitegemea" kiuchumi na mkeo ni mmoja kati ya hao wakimama.


Wanawake wengi wanachukulia Mwanaume ni "chombo" kiuchumi na watafanya lolote ili wanaumr waendelee kukidhi mahitaji yao kiuchumi.


Sasa wanawake wa aina hiyo wakifanikiwa kiuchumi inakuwa ni "kulipiza kisasi" kwa wanaume. Badala ya kutumia kipato chao kama sehemu ya umoja kwenye muungano husika(ndoa).

Hali huwa mbaya kama wanaume wamewahi kuwanyanyasa kiuchumi na kuwasimanga kuwa wao ni mama wa nyumbani tu (actually umama wa nyumbani ni kazi, tena ngumu kuliko kwenda ofisini kila siku).

Kaa na mkeo chini na mzungumze sio umwambie au kusema bali kuzungumza.....unaweka hofu zako na kero unazohisi na yeye anaweka zake kisha kwa pamoja mnakubaliana ni hatua gani mzifanye ili kubadilika na kuokoa ndoa yenu.


Umegusia kuwa hafanyi majukumu yake kama Mke.....unamaana Usafi, kupika, kuangalia watoto wakati wewe upo kazini?


Hayo ni majukumu ya "mke" ikiwa tu mkeo ni Mama wa nyumbani (haendi ofisini, anafanya kazi nyumbani).....lakini kwa vile wote mnafanya kazi 'majukumu ya Mke" yanakuwa yenu....mnashirikiana/saidiana.


Ikiwa wewe unachoka na yeye pia akifika nyumbani anakuwa kachoka, huoni ni sahihi kusaidiana au kukubaliana na kuweka Msaidizi.


Kumbuka kuomba radhi kwa makosa ambayo pengine hujawahi kuyafanya (unadhani haikuwa makosa) na hakikisha unasisitiza suala la hisia, usalama na furaha ya Watoto wenu mtakapokuwa mkizungumza.

Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Monday

Atishia kuniacha kisa FB!

Hi dada Dinah natumai hujambo na mzima wa afya. Hongera sana na pole
kwa kazi ya kuelimisha na kuboresha mahusiyano ya jamii.

Nina shida dada yangu, nahitaji wazo lako. Nina b/f wangu wa mwaka na miezi kadhaa anasema anataka kunioa ila simpendi hata kidogo.


Nimekubali kuolewa nae
ikibidi, ila sasa naona anaanza kuwa mkali. Anataka eti nitoe
picha zangu zote facebook na ikiwezekana nifunge kabisa account yangu.


Mimi nimemwambia sintaongeza kuweka picha zingine ila hanielewi na kuhusu kufunga kabisa nimemwambia kuwa siwezi kwasababu inanirahisishia kuongea na ndugu, jamaa na marafiki maana niko nao mbali.

Baada ya kumwambia hayo yeye amenitishia kuniacha.

-Je nitekeleze anayotaka? au nikisha tekeleza ndio ataanza sasa na
maamuzi mengine ya kiajabu-ajabu?


Au niachane nae kama alivyonitishia?
*************

Dinah anasema: Ungekuwa unampenda au mnapendana hakika ningekushauri uzungumze nae tena na kumuelewesha umuhimu wa ubaki na facebook yako kwa sababu kuu ulizozitaja.

Lakini upunguze mazoea ya karibu na namna ya kuwasiliana "rafiki" zako ambao baadhi wanaweza kumfanya jamaa apate wivu au akwazike.


Lakini kwa vile humpendi ni vema kuendelea tu facebook yako na yeye akuache kama navyotaka kuliko kubaki kwenye uhusiano nae wakati humpendi(unampotezea muda na unajipotezea muda pia).

****************

-Je nikiolewa nae na simpendi tutaathirika/nitaathirika kivipi? Au nitamzoea na kupenda jisi siku zinavyokwenda?

**************

Dinah anasema: Hakuna athari mtazipata ikiwa mtafunga ndoa isipokuwa mtakuwa hamna furaha au amani na ni guarantee kwa mmoja wenu au wote kutoka nje ya ndoa kutafuta "kupendwa" au penzi.

Utamzoea lakini kwenye kumpenda siwezi kujua maana kama mmekuwa pamoja zaidi ya Mwaka na bado humpendi "hata kidogo" sidhani hilo litabadilika mkifunga ndoa.


Kama unafikiria kuolewa nae ukiamini utampenda nadhani ni vema kuendelea ku-date kwa muda mrefu zaidi ili uone kama hisia zako za mapenzi zitajitokea kwake.
**************


-Swali lingine, eti ni kweli kutia mabarafu ndani ya uke inapunguza upana wa uke? Nini kazi ya
barafu ukeni?

kila la heri dada dinah.

*************


Dinah anasema: Do'h! Logically...ukiweka barafu itapanua uke kulingana na ukubwa wa barafu hiyo....then barafu itayeyuka na uke kujirudi kama ulivyokuwa awali....Jibu? HAPANA...Barafu haipunguzi uke.


Uke umedizainiwa kupanuka kulingana na kinachoingia na kujirudi tena, hiyo ni kwasababu ya kuruhusu mtoto kuzaliwa.

Ikiwa Misuli ya Uke wako imepanuka kutokana na Mf; kuanza Ngono wakati mwili bado hauja-settle (kabla au wakati wa Balehe au chini ya miaka 21). Utakapozaa, uke utapanuka ku accommodate "safari" ya mtoto Duniani na baada ya hapo uke wako utajirudi kama ulivyokuwa kabla ya Uzazi.


Kwa maana hiyo, kama tayari uke wako ni mpana na baadae ukazaa, utajirudi kwenye "upana" wake na si kuwa mdogo.

Na ikiwa uke wako ni mdogo basi baada ya uzazi utajirudi na kuwa mdogo kama ulivyokuwa kabla ya uzazi.


Ahsante kwa ushirikiano na Kila la kheri!

Mapendo tele kwako...

Sunday

Wivu na kutoaminiwa

Habari da Dinah, Mimi na mke wangu tumekuwa tukiishi maisha ya amani, Furaha na Upendo.


Kwa muda sasa mambo hayapo kama yalivyokuwa miaka ya nyuma. Mke wangu amekuwa na wivu sana na haniamini tena kama alivyokuwa akiniamini zamani.

Siku hizi tunapitisha hata miezi miwili, hajishughulishi wala kuonyesha kutaka kuwa karibu nami.

Mabadiliko ya tabia yamenifanya nihisi kuwa labda yeye sio muaminifu na anapata hisia mbaya juu yangu kutokana na Maovu anayoyafanya yeye.


Je, unanishauri nichukue hatua gani ili kuokoa ndoa yetu?

***************


Dinah anasema: Habari ni njema kabisa, ahsante kwa ushirikiano.


Umenikumbusha "ukiona kaanza wivu au hakuamini ujue yeye ndio anafanya maaovu nje ya ndoa na guilt ndio inamfanya ajisikie wivu/asikuamini"....wanaoamini hiyo ni ama wapuuzi....au hawajahi kupenda.


Wivu na Uaminifu ni vitu viwili tofauti lakini kimoja kinasababisha kingine hivyo naweza kusema vinategemeana.


Wivu ni hisia kama ilivyo hisia ya kumpenda mtu. Ikiwa unampenda mtu kimapenzi hutotaka kuona "tishio" la yeye kuwa na mtu mwingine kimapenzi bali wewe na hapo ndio Wivu unapojitokeza.


Kutokumuamini mtu kunatokana na issues za Wivu ambazo hazijafanyiwa kazi(kurekebishwa).

Nitakupa Mfano wa upande wa pili ili unielewe vema na mfano huu utakusaidia kuchukua hatua madhubuti kuokoa Ndoa yako.


Mf; mwenza wako anamazoea ya karibu na wanaume ambao wewe huwajui(marafiki zake) au hata kama unawajua(marafiki zenu).


Inafikia mahali mazoea hayo yanafikia hatua mbaya ya kuitana honey, sweet, Mpenzi, laazizi "kiutani" na kutumiana "visual" hugs, mabusu na emotions nyingine ambazo sio sahihi kwa watu ambao sio wapenzi.


Wao wanakua wa kwanza kusalimiwa asubuhi pale akiamka tu na hupewa "usiku mwema" kiss visually(wewe hupewi, yaani haipo siku hizi kwa sababu haupo kwenye Simu/Tablets).


Mkeo anawatembelea wao na kula nao chakula au kunywa nao (wewe na yeye hamfanyi hivyo siku hizi) kwasababu muda unatofautiana na hata ikitokea mpo pamoja bado hilo halitokei.


Unajaribu kuweka hisia zako wazi kwake kuwa hupendezwi na tabia hiyo ya mkeo, lakini badala ya mkeo kuomba radhi kwa kukuumiza hisia zako na kukuhakikishia mapenzi yake kwako kwa vitendo (sio Ngono bali affection, attention etc). Yeye anakuambia "acha wivu hao ni marafiki tu".


Au badala ya kuahidi kuachana na hao watu (kuwafuta/zuia) kimawasiliano na kuonyesha angalau dalili ya kubadilisha tabia yake hiyo mbaya....anajitetea au anawatetea "watu wake" au ana-justify kwa kusema "mbona wewe na akina blablabla siwaingilii".


Hapo ndipo kutomuamini Mkeo "kutazaliwa"....na kusipokuwa na kuaminiana kwenye uhusiano wowote basi ujue kuna tatizo kubwa na tatizo hilo litaingilia uhusiano wenu wa Kingono na hivyo kuhatarisha Uimara wake.

******Mwisho wa Mfano.

Katika hali halisi hatupaswi kuwaamini wenzetu kwa asilimia zote lakini huwa tunaongeza asilimia kubwa sana ya uaminifu kwa watu tunaowapa Mioyo na miili yetu.


Mkeo alipoanza kuhisi Wivu na kukueleza ulipaswa kuchukua hatua za kurekebisha kama ni tabia au matendo unayoyafanya na kupelekea Mkeo kupata wivu.


Sasa, kwasababu hakuna lililofanyika na labda ukategemea mkeo kuzoea au kuacha wivu bila wewe kutoa ushirikiano lakini haikuwa hivyo na badala yake sasa hakuamini tena.


Wivu hauwezi kuondoka wakati "chanzo" cha wivu bado kipo.....na hapo ndio tatizo la kutoaminiwa na mkeo lilipojitokeza.


Wanawake tunatofautiana na wanaume linapokuja suala la ngono, kwa mwanaume anaweza kuwa na wivu na akaweza kuendelea na tendo la ndoa kama ifuatavyo.


Lakini kwa mwanamke anaekupenda huwa ngumu kiasi kwani kwake tendo hilo ni sehemu ya mapenzi yake kwako na ukaribu wa muungano wenu kama wanandoa....sio ngono ili kumaliza hamu ya mwili.



Hatua gani uchukue: Mawasiliano.....weka issue Mezani na mizungumze kwa upendo, yeye akueleze hofu zake na wewe weka zako (umegusia kuwa unahisi yeye ndio Mkosaji na guilt inamfanya akuhisi wewe) mezani kisha muelewane na Mkubaliane kufanya mabadiliko..

Ushirikiano....badala ya kufananisha au kutetea "chanzo cha Wivu" jiweke kwenye "receiving end" wakati anajieleza ili upate kujua anavyojisikia kisha rekebisha lolote linalosababisha ajisikie anavyojisikia ili muungano wenu uwe na amani.

Kumbuka Ndoa ni safari yenye mabadiliko mengi, hivyo ni vema "kutozoea" mabadiliko au "kuyavumilia" na badala yake kwa pamoja fanyia kazi lolote linalijitokeza ambalo linatishia kuharibu kile mlicho nacho.


Rejeeni nyuma, awali mlikuwa mnafanya nini kama wapenzi? Fanyeni yale na kuongeza mapya na yale ya kati....


Unapofundwa, unaambiwa "usisahau ulikotoka....usiache kilichokufiikisha hapo ulipo"......hivyo kurejea mwanzo kimapenzi husaidia kuwakumbusha ni kiasi gani mnapendana.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Thursday

Ndugu wa Mume wanataka watoto.

Dinah habari za kazi, Mimi ni mama mwenye watoto watatu wenye umri wa Miaka 16, 12 na Tisa.

Mimi na Baba yao tumeachana bila Talaka miaka miwili iliyopita na mwenzangu tayari anamwanamke mwingine kitu ambacho sio tatizo kwangu.

Kinachonisumbua kichwa ni yeye Mume wangu na ndugu zake kung'ang'ania kuchukua watoto. Mimi binasfi sipo tayari kuacha wanangu wakaishi na watu wengine kwa muda mrefu hata kama ni ndugu zao.

Pia naogopa wakienda huko watakataliwa kurudi kwangu na hivyo kuishi maisha ya unyonge na upweke.

Kama ni wewe ungekuwa kwenye viatu vyangu ungefanya nini?


Ushauri wako utanituliza Moyo na akili ili niweze kulea wanangu na kufanya kazi kwa amani. Asante.


**************

Dinah anasema: Njema kabisa, nashukuru kwa ushirikiano.

Hao ndugu nao wanakiherehere kama mama_______! Wakati unanema kuwapata hao watoto walikuwepo? Waambie walee watoto wao, wakuachie ulee wako.

Hakuna mama mwenye akili timamu anaeweza kuruhusu watoto aliowazaa wakakae na watu baki (hata kama ni baba ambae hawajamuona kwa miaka 2 anakuwa "baki" kimtindo).


Sina uhakika na Sheria za Ndoa na Familia za Tanzania zilivyo hivi sasa, ila natambua Mahakama na Ustawi wa Jamii hushirikiana kwenye kutoa msaada.


Kitu muhimu ni wewe kumtaliki Mumeo (kisheria), utaratibu wa sasa siujui ila ukienda Mahakama ya Wilaya hapo ulipo na kuomba kuonana na Hakimu wa masuala ya Familia atakusaidia kwa ushauri na nini cha kufanya (nadhani kuna Fomu unajaza kwanza kabla).


Hakimu anapitia kesi yako (ulivyojieleza kwenye fomu), kwa vile umetangena na Mumeo kwa miaka 2 na tayari anamtu mwingine itakuwa rahisi.

Baada ya hapo nadhani Mumeo atatumiwa Barua ya kuitwa Mahakamani kisha "Kesi" yenu kusikilizwa....weka wazi na kusisitiza kuwa unataka kumtaliki mumeo.


Usiwe na hasira na wala kuongea katika hali yeyote itakayoashiria bado unahisia nae au bado unamaumivu ya kuachwa (ili isionekana unataka kumkomoa).


Baada ya hapo Uamuzi utafanywa na nadhani utashauriwa uende Ustawi wa Jamii kwa ajili ya masuala ya Mgawanyo wa Mali zenu, Matuzo ya watoto....n.k.


Kisheria (kama hawajaibadilisha) kutokana na umri(zaidi ya miaka 6) wa watoto, watoto wana haki ya kuchagua wanataka kuishi na nani kati yako Mama au Baba yao.

Watoto wataulizwa mbele yenu wote(Wazazi) kuwa wanataka kwenda kuishi na nani na Ustawi wa jamii watatoa ripoti yao kuhusu "issue" yako ya watoto wakae na nani, mgawanyo wa mali + matunzo kutoka kwa Baba yao.

Baada ya hapo nadhani utarudi tena Mahakamani na Uamuzi kufanywa na Hakimu Mhusika.


Ndugu huwa hawahusiki kwenye stage hii unless otherwise mmoja wenu afariki Dunia wakati wa process.

Kazi kwako kuwashawishi watoto wagome kwenda kuishi kwa Baba yao, tumbia mbinu zote za chini ya jua(sina maana uchawi, bali ushawishi kama Mama yao) kama unaweza ili wasikubali kwenda kwa Baba yao (ambae atawapeleka kwa Ndugu zake).


Fanya hayo kabla hujaanza shughuli za kupelekana Mahakamani, kwani kibongo-bongo inaweza kuchumua muda mrefu.


Baada ya uamuzi, hakikisha watoto wanauhusiano mzuri na Baba yao, usiwajaze maneno kutokana na hasira zako au hisia zako kwa baba yao ili wamchukie baba yao.


Kama watamchukia iwe kwa vile aliwaacha wao wakiwa wadogo (they will hate him for that naturally) bila wewe kusema lolote kwao.


Hivi hakuna Blog za Wanasheria wa Familia na Watoto za Kibongo? Ingesaidia sana kwa update za sheria hizi muhimu.


Mie sio mtaalamu wa sheria + naishi nje hivyo sizijui sheria za Ndoa na familia za sasa za Tanzania.

Najua hayo niliyoyaelezea kwasababu mtu wangu wa karibu alipitia humo na alifanikiwa. Ni kitambo thought.


Nakutakia kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Pages