Thursday

Mume ajali Rakize badala ya Familia yake...

Hongera kwa kazi nzuri rafiki, Naomba ushauri. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30.

Nmeolewa(Bomani) na nina mtoto wa miaka 4(ke) nathubutu kusema tangu nianze kuishi na huyu Mume sina kumbukumbu yeyote ya siku niliyowahi kufurahi nae (kutoka au kushea furaha).


Kutoka ni labda Msiba ukitokea tena upande wake ndio atakuambia kuna Msiba uende ila sio kwetu. Hana habari na ndugu zangu lakini anataka mimi niwahudumie nduguze.


Anawatoto wawili aliozaa na wanawake wawili kabla yangu na wote naishi nao kwasababu Mama zao walikuja kuwabwaga na hawajihusishi na lolote kuhusu watoto wao.


Tukipanga mipango ya maendeleo na kuelewana vizuri lakini hela ikipatikana anabadilika na kukuambia kuna rafiki yangu kaniomba kiasi cha pesa siwezi kumnyima.

Ukiuliza zaidi utaishia kugombana tu. Yeye ni mkali sana ukiuliza kitu kidogo anawaka.

Kunawakati aliniambia kuna dada ambaye ni Yatima anashida sana anaomba aje kukaa kwetu. Nkamwambia hali yetu ni mbaya kiuchumi hatutaweza kumhudumia wakati huo nilikua Chuo na nyumbani tulikua na mdogo wake (Wifi) tukakubaliana.

Siku ya siku akaniambia anaenda kumpokea msichana wa rafiki yake kwani huyo rafikie amemuomba kwani yeye hana nafasi, sikua na wasiwasi. Siku zikazidi kwenda kila nikimuuliza hanipi jibu linaloeleweka.

Wakaanza tabia ya kupiga stori hadi saa tano za usiku, binti akaanza kujiachia nyumbani yaani hafanyi kazi yoyote. Siku nipo Chuo Wifi akanipigia akanambia nimefanya fujo nyumban, huyu binti haeleweki nimemuuliza kaka kama ni mke wa pili aseme tujue lakini hakujibu!

Baada ya fujo za Wifi Mume wangu akamuondoa nyumbani na sijui alikompeleka.


Akaja mdogo wangu kwa lengo la kurudia masomo, tukawa tumekubaliana kumsaidia. Mara nikasafiri na niliporudi Mdogo wangu akanambia hataki kusome tena. Nikamuuliza mume kulikoni? akanijibu mkato achana nae hataki kusoma!!


Siku moja asubuhi akaamka mapema kwenda kuoga, muda ukawa unaenda nikatoka chumbani kimyakimya kujua kulikoni. Nikaenda bafunu, chooni hayupo! Ikabidi nisimame Koridoni kuona atatokea wapi?

Baada ya muda naona anatokea chumbani anakolala mdogo wangu, nikamuuliza kulikoni? akanambia alikuwa anachungulia mwizi?!


Ila moyo wangu ulikosa amani kabisa na tangu nimuulize kuhusu kutoka chumbani kwa mdogo wangu tukagombana sana hadi yule mdogo wangu akaondoka. Hivi ninavyokuambia huwa naomba muda tuongee anajibu kuwa amechoka.

Lakini simu zake hata usiku wa manane zikiita ataamka kupokea wakati mwingine hata mkiwa mnaduu na simu ikaita atakuacha akapokee simu.


Juzi ananiambia anataka watoto wanne, nikamwambia atalea nani?maana huyu mmoja kumtimizia mahitaji yake ni ngumu. Hivi hadi leo Ada hajamlipia tangu mwaka uanze achilia mbali mahitaji mengine na hao watoto wake wawili.


Naumia!! sio kwamba hela haipatikani kabisa, ikipatikana lakini yupo radhi kuvunja makubaliano ya familia yake na hutaiona hela yake. Ukiuliza tatizo, ataishia kununa na majukumu ya kifamilia hatimizi kisa kanuna.


Nimkopaji mzuri ila hakushirikishi kwanini anakopa na pesa anazokopa zinakwenda wapi?! Akiba kuweka kwake mwiko, na likitokea tatizo anaanza kupiga simu za kukopa. Marafiki zake wote wamemkimbia hawapokei simu zake.


Ukweli ni kuwa siamini kuwa anaweza kunisaidia kulea watoto wangu anaotaka nizae, hata mimi mwenyewe kunihudumia kama mke hanihudumii achilia mbali mtoto wetu huyu Mmoja.


Sina upendo tena kwake, yaani najilazimisha tu japo kimapenzi ananiridhisha.

Wote niwafanyakazi wa Serikali, Mshahara ukitoka mie nitaleta nyumbani na kama kunamahitaji nimenunua nitamuelekeza lakini wakwake unaishia Mfukoni. Hakwambii chochote zaidi ya nimelipa madeni ambayo sijui alikopa lini na kwanini?

Naomba ushauri ndugu yangu.


************


Dinah anasema: Ahsante na shukurani kwa Ushirikiano.

Jamani!! Ndoa ni uvumilivu kwa maana kuwa unavumilia hali ngumu ya maisha, magonjwa na mabadiliko mengine ya kibinaadamu sio upuuzi kama huo ulioueleza!


Wala tusipoteze muda kujadili uchafu wa tabia na matendo ya Mumeo, hastahili kabisa kuwa Mume wala Baba.

Kwavile huna furaha(hujawahi kufurahia Muungano wenu), huna mapenzi kwake na humuamini tena hakuna sababu wala umuhimu wa wewe kuendelea kubaki kwenye Ndoa ambayo imefikia mwisho.


Miaka 13 uliyoipoteza kwenye Ndoa hiyo inatosha, sasa ni muda wa kuanza kufurahia maisha yako yaliyobaki. Tunafunga Ndoa na watu tuwapendao(most of us) ili kwa pamoja tufurahie Maisha na kujenga Familia na sio kuonewa, kuteswa, kunyanyaswa au kutumiwa.


Ikiwa sasa unamiaka 30 inamaana umekuwa na huyo baba ukiwa mtoto wa miaka 17! No wonder wale ma-ex walikuja kukubwagia watoto na wewe ukakubali. Ungekuwa 30 then sidhani kama ungekubali.


Mie nakushauri utafute namna ya kutoka humo Ndoani. Kwa bahati nzuri una Kipato na inaonekana ni Mwanamke unaejielewa na unaakili, hivyo unaweza kabisa kuendesha maisha yako na mwanao bila yeye.


Kutokana na ukali wake na kukwepa mazungumzo na wewe hakuna haja ya kumuambia kuwa unataka kutengana nae au kumuacha....asije kukutoa roho....maana anajua wazi hakuna mwanamke anaeweza kuvumilia hayo yote aliyokufanyia....achilia mbali kulea,kuhudumia na kusomesha watoto wa wanawake wengine.

Akili kichwani mwako; hakikisha hakuna mtu anajua mpango wako mpaka utakapokamilika na umeisha hamia kwako. Hata mwanao asijue lolote maana miaka minne lazima atakuwa anazungumza vya kutosha....na bila kujua anaweza kuropoka kwa Baba yake ikawa vita.


Kila kitu kikienda sawia, uamuzi ni wako ama kumtaliki huyo "Mfano wa mwanaume" kupitia Mahakama au ukauchuna tu. Ila kumbuka Ndoa ya Bomani ni Ndoa inayotambulika Kisheria hivyo asije akaitumia hiyo baadae kukuharibia uhusiano Mpya.


Kwenye kila jambo unalolifanya hakikisha unakuwa Muangalifu, maana huwezi kujua akilini mwake kuna "madudu" gani.


Sasa anaenda kuwa Baba wa watoto 3 kutoka Mama 3 tofauti, what a mess!! Fanya yote lakini usimuachie/msusie mwanao.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

No comments:

Pages