Ni swali aliloulizwa mfanyakazi mwenzetu
"Sina mpango wa harusi na wala sitaki kusikia Habari hiyo tena?" bwana harusi mtarajiwa aling’aka na kuinuka kutoka nje.
Kila mmoja wetu pale ndani aliduwaa, kwani katika harusi tuliyokuwa tukiisubiria kwa hamu ilikuwa hii, je kulikoni, michango kadi kila kitu kilishaanza! Ushauri wa haraka unahitajika ili kama inawezekana tuiokoe harusi hii au la jamaa ajiandae kivingine.
Jamaa huyu alikuwa akiishi na mdogo wake ambaye alimchukua nyumbani kwao alipomaliza kidato cha nne, na kuamua kumuendeleza. Ilibidi ajinyime, na kujinyima huko ndiko kuliko changia hata achelewe kuoa. Ilibidi akope kazini, kuhakikisha mdogo wake naye anasoma hadi akafikia chuo kikuu, huu ni mwaka wake wa mwisho.
Jamaa akaona sasa naye atafute jiko, kwani umri umekwenda na alichofanya ni kuenda kijijini akampate `kuku wa kienyeji’ ambaye kamaliza kidato cha nne, mrembo kweliweli. Alipomfikisha hapa Dar na kumtambulisha kwa mdogo wake, kuwa huyo ndiye shemeji yake na kwamba watafunga ndoa lakini ameonelea asubiri mdogo mtu amalize chuo ili isimkwaze katika mipangilio yake.
Siku zikaenda na jamaa akawa anasafiri safari za kikazi kwahiyo nyumba inakuwa chini ya mdogo wake ambaye mara kwa mara alikuwa akija kulala hapo kama yupo safari vinginevyo alikuwa akikaa chuoni, sasa inabidi akae na shemejiye.
Siku moja jamaa, akarudi bila taarifa,ndipo yalipompata ambayo hatayasahau maishani, na kuapa kuwa yeye hana mpango wa kuoa tena. Kwani hilo sio tukio la kwanza, alishasalitiwa kabla na rafiki yake mpenzi na hii ya sasa imekuwa kali zaidi kwani aliyemsaliti ni mdogo wake toka nitoke. Aliwakuta `live’
Kumbe huyu binti na mdogo wake walikuwa wapenzi huko kijijini wakiwa shule, yeye yupo vidato binti alikuwa msingi. Na katika ahadi zao ni kuwa jamaa akimaliza shule walianzishe. Siku zilivyokwenda binti akawa anasakamwa na wazazi wake kwani wachumba wengi walishaposa bila mafanikio, ndipo alipokuja huyu jamaa ikawa ni hitimisho.
Uolewe na huyu! lasivyo atakuoa mzee Kijashimo kama mke wa pili. Binti akawa hana jinsi, `hata hivyo jamaa huyu mpya anafaa sana, nimempenda...' binti alisema.
Kwahiyo binti alipoletwa Dar, hakuamini kukutana ma mpenzi wake wa udogoni/utotoni na kisiri wakawa wanajirusha.
Za mwizi arubaini wamefumwa na kubainisha ukweli. Jamaa alishindwa la kufanya kwani kijijini alishakabidhiwa binti wa watu kwa heshima na kiapo na binti alikubali kuwa huyu sasa anafaa(kwa kweli alivutika naye alikiri binti) na alishaamua huyu anafaa kumuoa, hakujua kuwa atakutana na mpenzi wake wa kijijini tena.
Tukirudi kwa mdogo wake ndiye kipenzi cha wazazi wake, kumtelekeza hawezi. Alipoliona tukio hili alizimia kwa muda.
Ujumbe ndio huo tunaomba sana ushauri wenu.
emu-three na wadau wengine hapa kazini.
Jawabu: Hiki kisa kinasikitisha sana lakini sioni sababu ya kumfanyaKijana kususa kufunga ndoa kwa vile tu matukio mawili yaliyotokea. Natambua wazi kuwa atahitaji muda ili kuondokana na kilichojijenga Kisaikolojia na pengine akahitaji wataalamu ili kumsaidia ku-over come hilo.
Suala sio Mdogo mtu kuwa kipenzi cha wazazi basi asitelekezwe kama alifanya kosa la kumsaliti kaka yake hakika alikuwa akistahili adhabu kubwa zaidi ya kuterekezwa lakini Mdogo mtu hajafanya kosa na kama ilivyo kwa kaka yake na mpenzi “wao” yeye pia ni “Victim” wa utaratibu wa maisha ktk jamii yetu ya kibongo.
Hakuna mwenye kosa kati yao hao wanandugu wawili na huyo binti, nafikiri jamii iliyokuwa ikiwazunguuka ndio inapaswa kulaumiwa kwani kama kungekuwa na “uhuru” wa jina kutambulishana kwa wazazi kama “marafiki wa karibu” ambao huenda pengine wana hisia za kimapenzi lakini hawako tayari kujihusisha na mwanya gono(inawezekana kabisa).
Hivyo basi kama jamii ya Kibongo ingeachia kidogo ili vijana waweze kurafikiana na badala ya kuwatisha unawaeleza ukweli wa mambo hali ambayo ingesaidia kwa kiasi kikubwa kwa familia ya binti na Mdogo wake kijana muathirika kufahamu ukaribu wa wawili hao na hivyo wasingeruhusu kaka mtu kuchukua jumla.
Kaka mtu anachopaswa kufanya ni kuwaacha wapendanao hao waendelee namapenzi yao kwa ni wao ndio walioanza kupendana na penzi lao lilikuwa asilia ulikinganisha na yeye, pengine huyo mwanamke hana mapenzi na huyo aliyemleta mjini (kaka mtu) lakini alikubali tu kwa vile hakutaka kuolewa kama mke wa pili na Mzee Kijashimo kama alivyotishiwa na Familia yake.
Kwa kifupi basi napenda kusema kuwa haya ndio matokeo ya kuficha ficha pale tunapokuwa na mafariki wa jinsia tofauti ktk umri wa ukuaji. Unajua kile kipindi cha ukuaji kila mmoja wetu huwa na hisia za kuwa na mtu wa karibu ambae mara nyingi huwa tunarafikiana kwa muda mrefu na kupendana bila kujihusisha na ngono.
Lakini tatizo linakuja kwa wazazi, ndugu na jamii kuhisi kuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya “matusi”. Badala ya kuwasaidia na kuwalezea nini cha kufanya kukabiliana na masumbufu ya ukuaji na kuwa huru kumuona rafiki yako wa jinsia nyingine unapigwa marufuku kama sio kuhamishwa na shule kabisa.
Naelewa kuwa jamii, wazazi na ndugu wanajaribu kulinda binti/kijana wao na kuzuia wasiharibu maisha yao ya badae kwa kutiana mimba ktk umri mdogo lakini hapo hapo itambulike kuwa kuna umuhimu wa kujua nani anarafikiana na mtoto wako na urafiki wao ni namna gani hasa.
Ushauri wangu ni kwa Kaka kujipa muda na kufurahia maisha yake badala ya kuhofia lini atapata “jiko” na wapi hasa linapatikana. Akumbuke kuwa Mapenzi hayalazimishwi na vilevile kila linachotokea ktk maisha yetu huwa kuna sababu kwanini hasa kimetokea.
Huyo binti hata kama ungefunga nae ndoa asingekuwa akikupenda kama alivyokuwa akimpenda Yule aliyeujaza moyo wake na kwa vyovyote vila lazima angenda tafuta mapenzi ambayo yasingekuwepo hapo ndani na hivyo ndoa yenu ingeharibika.
Napenda kuwashauri ninyi marafiki zake kumuacha jamaa aishi vile apendavyo kwani kutokana na maisha ya sasa kufunga ndoa ni uamuzi wa mtu pale anapokutana na Yule atakae ujaza moyo wake kwa mapenzi, ila kasumba ya kukimbilia kijijini unapohisi umri wa kuoa umefika sio haki kwako wewe muaji na Yule muolewaji kwani ndoa yenu ita-base kwenye “wajibu” na kila kitu maishani mwenu kitakuwa wajibu na sio mapenzi.
Kila la kheri.
No comments:
Post a Comment