Sunday

Wifi anachukua nafasi yangu, nifanyeje?-Ushauri

"Nimegundua kuwa watu wanafanikiwa kuokoa mahusiano na ndoa zao kupitia blogu hii na mimi leo nimeona nichangie tatizo langu ili kupata ushauri wa watu wengine na zaidi kutoka kwako Dada Dinah.

Mimi ni mdada mtu mzima tu nimeolewa miaka si chini ya mitano, nina watoto wawili. Nimekuwa nikishindana na wifi yangu ambae ni dada wa damu wa mume wangu, ushindani wetu ni kama mtu na mke mwenzie lakini si hivyo.

Kabla sijaolewa na huyu mwanaume tulikuwa kwenye uhusiano wa mbali kwani mimi nilikuwa nasoma Ireland na yeye alikuwa Tanzania. Kipindi chote hicho hakukuwa na matatizo yeyote kati yangu na dada yake.


Baada ya kumaliza masomo nilihamia England kufanya kazi ambako ndiko tunaishi mpaka sasa. Ndoa yetu ilifungiwa Tanzania na Mume wangu akanifuata huku na baada ya muda tukasaidiana na kumleta dada yake ambaye ndio wifi yangu huyu mwenye vituko kila kukicha ambavyo vinahatarisha ndoa yangu.


Imefikia hatua wifi yangu kuchagua nini kifanyike ndani ya nyumba yangu, aina gani ya vifaa vinunuliwe ikiwa tunafanya marekebisho hapa ndani, wapi tuende au tusiende, tukamtembele nani nalini na kinachonikasirisha zaidi ni kaka mtu kumsikiliza dadake na sio mimi mkewe.


Ikitokea mimi na mume wangu tumejadili jambo la kufanya kwa ajili ya familia yetu ndogo mume wangu anachukua simu na kumwambie kila kitu mdogo wake na kitakachosemwa na mdogo wake basi ndio kitakachofanywa na sio mimi hata kama sehemu ya jambo hilo pesa zangu zinahusika. Yaani imekuwa kama akili ya mume wangu haifanyi kazi basi anatumia ya dada yake kufanya maamuzi.


Kitu kingine kinachoniumiza roho na kunipa donge ni pale ninapotoka kazini jioni au siku za mwisho wa wiki wote tuko nyumbani, badala mume wangu atumie muda huo na mimi yeye atakuwa kwenye simu na dada yake wakiongea maongezi yasiyoisha tena kwa kilugha chao na kucheka.


Nimevumilia sana na nimefanya vikao na ndugu wa pande zote mbili na hata kuzungumza na mume wangu lakini hakuna mabadiliko yeyote, nimekuwa mkiwa ndani ya ndoa yangu na sijui nini cha kufanya, japokuwa nampenda mume wangu lakini kama suluhisho ni kutoka kwenye hii ndoa basi nitatoka ili kutafuta amani na furaha kwingine lakini sio ndani ya ndoa hii.


Wifi yangu huyu ni mkubwa zaidi ya mume wangu, ameolewa na anawatoto kadhaa wote wako Mkoani Kagera Tanzania.
Naombeni ushauri ndugu zangu"

Jawabu:Mmh Dada tatizo unalokabiliana nalo ni zito sana kwa mwanamke yeyote yule ndani ya ndoa. Kwanza kabisa nakupa pongezi kwa kuwa mvumilivu na kwa ushirikiano wa kuchangia tatizo lako mahali hapa.


Nisingependa kuingia ndani sana lakini nashindwa kujizuia kupata hisia kuwa Mumeo na Dada'ke hawajiamini kwa vile umewasaidia kwa namna fulani kujikomboa kimaisha......ndio Ulaya sio mwisho wa matatizo lakini ukweli utabaki pale pale kuwa, kama ukifanikiwa kupata kazi you better off huko kuliko Bongo. Sasa nahisi hawa wanafamilia hawaamini kuwa wewe mwaamke ndio sababu ya wao kuwa huko na hilo linafanya kupoteza ile hali ya kujiamini.


Natambua sio vema kuzungumzia Makabila lakini ni wazi kuwa kuna Makabila mengine hapa Tanzania wanajali sana kuwa juu kwa kila kitu, sasa ikitokea wanakutana na mtu amabe yuko juu kabla yao inakuwa taabu. Ninaamini kabisa kuwa Mumeo hajiamini mbele yako kwa vile inaonyesha umesoma na una kazi nzuri kulingana na Elimu yako, hili ni gumu sana kwa mwanaume yeyote kuishi nalo achilia ukabila wake.


Hili linalotokea kwenye uhusiano wako huenda ni matokeo ya u-bully wa dada mtu kwa mdogo wake ambae ndio mume (lazima kutakuwa na walakini kwenye udada-kaka wao) pia inawezekana ni mambo ya "Ego" tu, Sasa kwa vile mumeo ni mdogo (kutoka na maelezo yako) inawezekana huwa anasikitika au kulalamika kwa dada yake kutokana na kutojiamini kwake, Mf-Unafanya vitu vikubwa ambavyo ktk hali halisi yeye kama mwanaume anadhani ni jukumu lake n.k


Umesema (kwenye maelezo yako) kuwa umezungumza na mumeo kuhusu tabia yake na ile ya dada yake lakini hakukuwa na mabadiliko, inawezekana kabisa namna unavyo wasiliana na mumeo ni tofauti na unavyopaswa kufanya.


Linapotoke tatizo kama lako ambalo linahusu ndugu wa mumeo unatakiwa kuongea na mumeo kwa upendo na mapenzi lakini wakati huohuo unakuwa "firm". Ukiwakilisha hoja zako kwa mumeo ktk mtindo wa kulalamika na kunung'unika mumeo hatochukulia umwambiayo "serious" na badala yake atadhania kuwa wewe unawalakini na dada'ke na unajaribu kuwatenganisha kama ndugu.


Nini cha kufanya: Jitahidi kujiweka kwenye "mood" nzuri yaani kuwa mwenye furaha (hii itakusaidia kumuonyesha mumeo kuwa huna chuki na dada'ke na wala huna hasira nae mumeo). Zungumza na mumeo kwa mapenzi na kwa uwazi kabisa bila kuficha kitu.........na anza kwa kuelezea hisia zako za kimapenzi juu yake, mueleze ni namna gani unafuraha kuwa mke wake na kuchangia kila kitu kwenye maisha yenu, mwambie ni namna gani wakati mwingine unajisikia mpwekwe pale anapojisahau na kutumia muda wake mwingi peke yake (usigusie kuhusu dada'ke).


Mkumbushie namna gani uhusiano wenu ulivyokuwa hapo awali (kabla Dada'ke hajaungana nanyi huko Ughaibuni lakini usimtaje wala kugusia ujio wake), onyesha ni namna gani mlikuwa mnatumia muda mwingi pamoja sio tu kama mke na mume bali wapenzi na marafiki. Muonyeshe ni namna gani ulikuwa unafurahia ukaribu wenu na unaweza kuongezea jinsi uhusiano wenu kingono ulivyokuwa then.


....wakati unaongea yote haya hakikisha hakuna umbali kati yenu na umuonyeshe mapenzi ya hisia ambayo hujawahi kumuonyesha kwa muda mrefu au hujawahi tangu mkutane, usisahau kutabasamu na ku-flirt kimtindo na mumeo huku unamuangalia moja kwa moja kwenye macho yake, mwambie hufikirii hata siku moja kuishi bila yeye na utafanya kila uwezalo kuhakikisha uhusiano wenu unakuwa bora, uliotawaliwa na mapenzi......(hapa atakuwa tayari kupokea "kibomu").

Malizia kwa kusema kuwa, ungetaka uhusiano wenu uwe kama ulivyokuwa mwanzo kwani hivi sasa hauna furaha, amani wala raha ndani ya ndoa yenu kama ilivyokuwa awali na ungependa mabadiliko.....ondoka na nenda kufanya hsughuli zako.

Hapa atakuita/kufuata akitaka kujua nini hasa unamaanisha au atabaki kimya akitafakari uliyomueleza.....usitegemee jibu au mabadiliko siku hiyo hiyo hivyo basi mpe muda na endelea kumuonyesha "mood" nzuri na kama vipi muda wa kitandani ukifika mpe mambo matamu bila kinyongo.

Wakati unaendelea kusubiri mabadiliko ya tabia ya mumeo, mtafute wifi yako na ongea nae ana kwa ana (no sms wala simu) na yeye mpe kitu cheupe kwa kifupi bila hasira wala chuki lakini cheza na Saikolojia yake.

Mwambie kuanzia muda leo aache tabia yake ya kuingilia maamuzi ndani ya ndoa yako, mwambie ulivyoolewa hukuolewa na watu wawili bali mume wako pekee ambae unampenda kwa moyo wako wote na hauko tayari kuumiza hisia za mume wako kwa kufanya mambo machafu ambayo kwa kiasi kikubwa yatakuwa yamesababishwa na tabia yake chafu (hii kisaikolojia itamfanya ahofie kaka yake kuumizwa na wewe na bila shaka atakimbia kwenda kumuambia).

Sasa kwa vile ulimpa mumeo mambo hadimu usiku uliopita alafu leo dada mtu anakuja na issue ya wewe kutopenda kumuumiza hisia hakika itafanya kazi vema kabisa.

Endelea kusubiri mabadiliko ambayo yatajitokeza ndani ya wiki chache hasa kama mumeo anakupenda lakini ikitokea vinginevyo na wanaendelea na tabia yao mbaya basi siombaya kama utatafuta ustaarabu mwingine......lakini nakuhakikishia kabisa kuwa mbinu hizi zitafanya maajabu kwenye uhusiano wako.

Kila lililo jema Mdada.

No comments:

Pages