"Mimi ni mama wa kitanzania ninaeishi na familia yangu UK, nimeolewa miaka 12 iliyopita na ndoa yetu imejaaliwa watoto wa wiwili na mwingine wa tatu yuko njiani. Mimi nilikuja UK kwa ajili ya masomo na kumuacha mpenzi wangu ambae sasa ndio mume wangu nyumbani Bongo.
Wakati naondoka tulikubaliana kuwa nikikaa kwa muda nimfanyie mpango ili na yeye aje huku kusoma, lakini kutokana na ugumu wa maisha kwangu kama mwanafunzi niliekuwa chini ya wazazi sikuweza kufanikisha hilo na yeye hakuwa na pesa za kutoshana kumleta huku. Basi tukaamua kusitisha suala la kusoma na kwavile tulikuwa tunapendana tukaamua kuwa yeye aje huku kama mwenza wangu na hivyo mimi nitaendelea na shule wakati yeye akifanya kazi ili kumudu maisha yetu.
Baada ya mimi kumaliza na kufanikiwa kupata kazi kwenye Bank na tukafunga ndoa mwaka uliofuata, maisha yakawa mazuri, mapenzi motomoto kama mke na mume na baada ya mwaka mmoja tangu tufunge ndoa nikajifungua mtoto wetu wa kwanza.
Baada ya kumaliza likizo ya uzazi mume wangu akaamua kuacha kazi bila sababu ya msingi, mimi haikunisumbua kwa vile kazi yangu ilitosha kutufanya tuishi maisha ya kawaida. Mtoto wa pili akaja, nikaamua kukaa chini na mume wangu ili tujadili maisha yetu ya mbeleni kwani familia inakua, mume wangu akaahidi kurudi kazini. Lakini hakufanya hivyo na sasa mtoto wa tatu yuko njiani.
Mume wangu amekuwa mvivu, hajali, hana umpendo na asie na ubinaadamu kabisa, natoka nyumbani asubuhi na mapema kwenda kazini, narudi jioni nikiwa nimechoka si unajua tena ujauzioto! nikifika nyumbani kitu pekee nahitaji ni kupumzika, lakini wakati napumzika utasikia mume wangu anauliza "leo hatuli humu ndani?" wakati yeye anatazama TV. Kwavile nakuwa nimechoka na sitaki ukorofi mwanamke nainuka naenda jikoni na kuanza kuandaa chochote cha haraka haraka ili nipate muda wa kupumzika.
Siku moja nikaamua kuzungumza na mume wangu na kumwambia jinsi ninavyojisikia kuhusiana na suala zima la ujauzito, masaa mengi kazini na kumuomba tusaidiane shughuli za ndani ili kuepusha matatizo kwangu na kwa mtoto alie tumboni.
Sikuamini masikio yangu pale mume wangu aliposema kuwa " wewe ni mwanamke wa kiafrika ni lazima uhakikishe nyumba safi, chakula kinapikwa na kuangalia watoto. Kwani kuwa na mimba ni ugonjwa? wangapi wanakuwa na mimba zinatoka na wanapona alafu wanashika nyingine na wanazaa? ikitoka hiyo utapata nyingine".
Dinah ghafla nikajisikia sina nguvu, nikanyanyuka taratibu bila kusema kitu nikaenda zangu kupumzika. Tangu siku hiyo nikaamua kuwa kila Juma Pili nitakuwa napika chakula/kuandaa chakula kingi kwa ajili ya wiki nzima ili watoto wangu na baba yao wasishinde njaa.
Sasa ndugu zangu nauliza hivi, kama hali imefikia hivi na watoto wetu hawajafikia umri mkubwa kuishi na mzazi mmoja nitakuwa nakosea kama nikimvumilia mpaka watoto wakuekue kidogo ndio nitafute ustaarabu wangu au nitengane nae sasa ili nisimpatie matatizo mtoto alie tumboni?.
Mimi binafsi hisia za mapenzi kwa mume wangu hazipo tangu aliponiambia kuwa mimba sio ugonjwa na mameno mengine yote, yaani namuona kama mtu tu pale asie na umuhimu wowote kwangu. Sina uhakika kama hali hii nikutokana na ujauzito, hasira au mapenzi yameisha?
naombeni msaada wenu wa kimawazo.
Mdau wa UK"
No comments:
Post a Comment