Wednesday

DL kwenye Umuhimu/faida/hasara ya ndoa.


DL nafurahishwa na michango yako!


"Dear Dinah,
Naomba unipe nafasi nitoe maoni yangu machache kuhusu maudhui ya hapo juu.Siyo rahisi kutoa jibu moja kuhusu tendo la ngono kabla au bada ya Ndoa kama ni sahihi au afadhali au ni vyema au si sahihi au si vyema.


Tatizo kubwa linatokana na mambo mawili: Imani za kidini au miko ya kijamii, kwa upande mmoja, na lengo la wanaotaka kufanya kitendo hicho ni nini hasa, kwa upande wa pili.
Kwa upande wa imani za kidini –na hapa karibu dini zote, hasa Dini Samawiya (Dini za Vitabu Vitakatifu kutoka Mbinguni)- au hata miiko ya kijamii, ngono kabla ya ndoa inakatazwa –haramu- na ni mwiko kwa jamii, yaani marufuku.


Upigwaji marufuku huu unatokana na mtazamo wa kina wa dini na jamii mbali mbali kuhusu madhumuni hasa ya ndoa. Madhumuni ya ndoa, kidini na kijamii, ni kuendeleza na kutunza vizazi vya jamii (re-creation) kupitia ahadi (ndoa), mbele ya mashahidi kwamba ahadi hiyo itaheshimiwa na kutekelezwa chini ya taratibu zilizowekwa, kwa msingi wa upendo, uvumilivu na uungwana, mambo ambayo ndiyo mihimili ya Mapenzi (Love) .


Hivyo, madhumuni makubwa ni kuendeleza na kutunza kizazi; yaani matunda ya ndoa, ambayo ni watoto na familia. Raha na utanashati (recreation) na mapenzi (love), kwa maana hiyo, ni malengo ya pili, au ni matokeo ya lengo kuu la kwanza la ndoa: yaani kuendeleza vizazi.


Kwa mtazamo huo, basi, hapana mjadala kwamba ngono kabla ya ndoa, hata kama inatokana na pendo au mapenzi, haikubaliki; maana inakosa uhalali (leseni) wa jukumu la msingi la kuendeleza kizazi cha jamii (re-creation) mbele ya mashahidi. Raha na starehe (recreation) ni matokeo na natija ya madhumuni hayo halisi.


Ndoa, kwa maana hiyo, ni mapatano ya msingi ya utekelezaji wa ahadi. Kwa maana hiyo, ndoa lazima ije mwanzo kabla ya ngono na si venginevyo. Ukiacha maadili ya kidini na kijamii, na ukayaweka kando, na ukajiuliza je ni afadhali au si afadhali kufanya ngono kabla ya ndoa, basi bado hutaweza kupata jibu la haraka, hata wewe mwenyewe, kama hujajiuliza swali la msingi kabisa, kwanza.


Nalo ni hili: Nini hasa madhumuni ya ngono unayotaka kuifanya? Ni raha na starehe tu au ni raha na starehe pamoja na yanayoweza kutokana na raha hizo na starehe hizo? Ikiwa madhumuni makubwa ni raha na starehe (recreation) inayoweza kupelekea kupeyana ahadi (ndoa) kuhusu kuendeleza na kutunza kizazi basi unaweza kusema kwamba ngono kabla ya ndoa ni jambo la maana; maana inatoa mwanya mzuri wa kupima tabia, uelewano, uvumilivu na hata kiwango cha pendo au mapenzi, kwamba je upo uwezekano wa kufungamana kwa muda mrefu?


Ni pima maji; je unaweza kuyavulia maji nguo na kuyaoga au la? Lakini, na hapa napenda kusisitiza LAKINI laima nyote wawili muwe wakweli; wakweli kwenye nia yenu hiyo na si venginevyo.

Venginevyo mtakuwa, ama nyote wawili mnajidanganya, au mmoja wenu ambaye si mkweli anajidanganya na kumdanganya mwenziwe. Lakini ikiwa madhumuni halisi ni raha na starehe TU, basi ngono ndiyo tendo kuu la kutoa kiu hicho cha raha na starehe hiyo. Ila, kwa nanma ilivyo, ni jibu la muda tu. Suala la ndoa halipo wala halifikiriwi. Hapa wapo watu wa aina mbili.


Kuna wale ambao wanatafuta raha na starehe tu na si jambo jengine. Kila mmoja anatafua kukata kiu chake tu.Wengine ni wale ambao wanatafuta raha na starehe hata kwa kununua au kuuza miili: ambao jamii huwatambua kuwa ni malaya na wahuni. Miongoni mwa wahuni unaweza hata kukuta “wana ndoa”.


Makundi yote haya mawili yanayowinda raha na starehe tu yanachangia sana matatizo ya kusambaza maradhi mbali mbali, miongoni mwao wenyewe kwa wenyewe na miongoni mwa jamii zao na jamii za wengine. Wanaweza hata kuathiri familia zao wenyewe, kwa wale ambao wameshaoa au kuolewa.


Pale lengo la raha na starehe linapokumbana kiajali tu na uja-uzito, au kunogewa na fungamanisho la ngono, basi wana-ngono hao huanza kufikiria njia mojawapo ya ama kujipa majukumu ya matokeo hayo, au ya kuwatangazia wengine kwamba wawili hao ni wao-kwa-wao hawataki mshirika nao. Mojawapo wa njia za lengo hilo ni ndoa.


Nyengine ni Unyumba, au kuishi-kimada na kadhalika. Kwa vizazi vya siku hizi, u-BF-GF au wapendanao, ni mojawapo wa njia hizo. Hawa wa siku hizi, wanasaidiwa sana kufikisha malengo yao hayo na vidonge vya kuzuwiya uzazi. Ngono kwa hawa ni lengo la raha na starehe. Endapo watanogewa na kuelewana basi wanaweza kufunga ndoa.


Venginevyo, kila mmoja anafunga virago vyake na kuelekea kwengine, na kuanza upya. Hivyo, narudia kusema kwamba si rahisi kutoa jibu la mkato au jibu moja, kabla ya kujuwa madhumuni halisi ya tendo hilo la ngono. Ila naweza kusema kwamba ni afadhali sana na ni busara kubwa ndoa kuitangulia ngono na si kinyume chake.


Yaani ni bora kumtafuta wa kuishi naye kwa mapenzi kabla ya kufanya mapenzi yenyewe. Na hapo ndipo penye tofauti kati ya ngono na mapenzi. Ngono inaweza kukata kiu lakini haishibishi. Mapenzi yanakata kiu na yanashibisha. Ngono inatoa raha ya muda.


Mapenzi yanatoa raha ya muda mrefu. Ngono inapapatisha amani na utuilivu wako, na kupoteza vyako, na pengine hata vya wenziwako.Mapenzi yanadumisha amani na utulivu wako, pamoja na kutunza vyako na hata vya wenziwako.

Mwenye akili haambiwi chagua. Mwenye macho haambiwi tazama. Mwenye masikio haambiwi sikia. Kila kitu kiko wazi kama giza la usiku na anga la mchana.
Upo hapo?!!!" DL.

No comments:

Pages