Nilibahatika kupitia mitandao mbalimbali ili kuona maelezo mbalimbali yahusuyo mada hii. Mengi niliyoyakuta ni yaleyale ninayoyafahamu ambayo hata hivyo yameniacha nikiwa na maswali mengi badala ya majibu.
Najua dada Dinah, hata wewe umeliona hilo na kwa uzoefu wako wa kusaidia watu katika nyanja nzima ya maisha na kuridhishana kimaumbile unaweza ukatoa jibu lenye kutosheleza.
Labda nikokotoe maelezo kidogo kwanini nimeuliza hili ili kila mchangiaji aone nini umuhimu wa kufundishana na kuelezana dhana nzima ya neno ndoa, na kwanini kabla ya ndoa kuna vipengele anuai kama `uchumba’ na baada ya ndoa kuna vitu kama `fungate’ na baada ya fungate kuna nini tena?
Wengine hukimbilia `talaka’ au `misukosuko ya ndoa’ ambayo huenda imesababishwa na kutokuelewa zana nzima ya ndoa, na kwanini hii ndoa ikawepo! Wengine wamediriki kusema haina haja ya ndoa, eti kila mtu akijisikia amtafute amtakaye amalize shida zake, lakini hatimaye uzee unapotinga anajuta na anakiri kweli kuna umuhimu wa kumtafuta mwenza, ni kwanini?
Kutokana na hili nikaona kuna haja ya kutafiti kwa undani kwanini kukawa na ndoa. Hii ndoa kwanini iwe na vipengele fulani, vinasaidia nini. Na kawanini ndoa ambayo kiujuujuu tunaiona kuwa ni `raha’ ni `uhalalisho’ wa kutenda yale yaliyokatazwa, ni `kusaidiana’ kwani unaunganisha `jamii’ mbili.
Lakini kwa wengine imekuwa ni kinyume na matarajio, na wengine huishia kusema kuwa `ndoa ni ndoana’ kwani ikikunasa hunasuki. Na wachache waliofanikiwa wamekaa kimya hawataki kuwanasua walinasa kwenye ndoana hii.Tumepata maelezo mengi ya `ngono na kungonoana’ lakini hapa bado tunahitaji maelezo yanaisaidia `ngono!’
Kwani tuelewe kuwa sisi ni binadamu na tuna taratibu zilizokubalika na kututofautisha na viumbe wengine, kuwa tendo hili ni la baraka, na baraka hii haiji kama wanavyofanya wanyama.
Baraka hizi huja kwa taratibu maalumu, nayo ndiyo mchakato mzima wa kuiendea ndoa. Na hata wale waliochepuka na kuishi bila `ndoa’ hujiona hawana baraka hizi, hatimaye huamua na kusema `tunaibariki ndoa’ na ajabu kabisa, wakiamua kuibariki ndoa yao wanaumua kwenda `fungate’!.
Sasa ni kwanini ndoa, na kwanini hawa waliamua kuibariki ndoa yao bado wanakimbilia kufanya fungate na ili hali walishapimana vya kutosha?Hili linahitaji uwanja mpana wa maelezo.
Ninaomba dada Dinah, ulikuze na uliwekee vipengele ili tujifunze, sio sisi tu tulio ndani ya ndoa lakini hasa vijana wetu wanajiandaa kuingia katika uwanja huu mpana wa `mke na mume’, ili wasije wakataabika, na kuishia kuchukiana badala ya `kupendana’ na baya zaidi tunaweza tukapunguza tatizo kubwa la gonjwa la `ukimwi’ kama kweli tutakuwa tumefuatilia kwa namna yake utaratibu huo mzima wa ndoa na kabla na baada.
Kama nimekosea tusahihishane.
Mimi emu-three
No comments:
Post a Comment