Wednesday

Nimegundua Mpenzi alizaa kabla, sina amani-Ushauri

"habari dada dinah na pole kwa kazi ngumu ya kuelimisha jamii, mimi nimekuwa mfatiliaji wa hii blog yako kwa muda mrefu na leo nina swali , Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 21 sijaolewa ila nina mchumba ambae ana malengo mazuri na mimi lakini dada nina tatizo moja.

Mchumba wangu huyu tangu niwe na uhusiano nae ni mwaka umepita sasa, kwa kweli ananipenda na mimi nampenda tena sana tu na ananihudumia kwa kila nitakacho yani kama mke wake. Huwa hanifichi kitu! lakini nimekuja kugudua kuwa yeye ana mtoto mmoja wa kike na ni mkubwa, kwanza alikataa kuniambia kwa kudai ni mapema mno baada ya kumbana akaniambia kweli kuwa anamtoto ambaye alizaa na mwanamke mmoja kabla ya kuwa na uhusiano na mimi.

Alidai kuwa anamuhudumia yule mwanamke sababu wazazi wa yule binti wamembana ahudumie, pia amesema yeye anampenda mtoto tu na sio mama yake kwani hakutaka kuzaa nae ila ilikuwa bahati mbaya!

Sasa dada mimi Moyo wangu umeingia chuki sana baada ya kusikia hivyo lakini mwenyewe anadai anampenda sana mtoto wake kuliko kitu kingine, mimi hapo ndio sielewi je anampenda kuliko mimi?

Dada naomba ushauri, huyu mwanaume nampenda na ndiye anayenisomesha Chuo mpaka sasa na huduma zote ananipa ila tatizo ni chuki iliyoniingia ghafla nashindwa kuelewa ni kwa nini naomba msaada wako! kwani nataka nafsi iwe na amani."

Dinah anasema: Asante sana kwa mail na uwazi wako, Habari ni njema sana tu namshukuru Mungu. Vipi wewe? pole kwa kutokuwa na Amani moyoni. Kuna mchangiaji kafafanua vema kuwa hisia hizo sio chuki bali wivu nami nakubaliana nae kani ni ukweli.


Hiyo ni hali ya kawaida kabisa kwa mwanamke/mwanaume yeyote mwenye mapenzi, unapogundua mpenzi wako anazungumza na Ex wake na siku zote huwa tunawakataza wapenzi wasiwasiliane na Exes.....sasa ndioitakuwa Ex ambae wametengeneza mtoto pamoja kama sehemu ya mapenzi yao....mmh?!! Ni ngumu sana tusichukulie juu-juu tu.

Mchumba wako ni Kaka mwema, ni kweli anakupenda na amedhihirisha hilo kwa kutokuambia mapema kuwa anamtoto ili asikupoteze, muda ulipofika kaweka wazi kila kitu na hata kusema kuwa anahudumia mama mtoto wake. Hii yote inaonyesha kuwa Mchumba wako ni mmoja kati ya wanaume wachache waaminifu, wakweli na wawazi.....Mshukuru Mungu kwa hilo.

Nadhani kinachokuumiza zaidi ni Mchumba wako kumhudumia mama mtoto wake na sio mtoto, kama Mchumba wako hana uhusiano na mwanamke huyo ni wazi hapaswi kumpa huduma yeyote yule mwanamke bali mtoto wake tu.

Mtoto huyo ametengenezwa na watu wawili, yaani yeye na huyo mwanamke hivyo wote kwa pamoja wanatakiwa kukusanya nguvu na kumhudumia mtoto wako sio Mchumba wako kumhudumia mwanamke huyo kwa kisingizio cha mtoto kwani mwanamke huyo hamhusu kwa sasa.


Wazazi wa yule Binti wanachokifanya sio haki na kisheria hakitambuliki, Mchumba wako anatakiwa kuhudumia mtoto wake tu na si vinginevyo. Ukipenda unaweza kuongea na Mchumba wako sasa au kusubiri mpaka mtakapo funga ndoa wewe na mume wako (waakati huo) itabidi mjipange na kwenda kuonana na wanasheria wanaojihusisha na masuala ya watoto na familia (zamani walikwa pale Mnazi mmoja) huko watampa ushauri na nyaraka zinazoelezea haki yake kwenye maisha ya mtoto wake na sio mama wa mtoto huyo.


Alafu mchumba wakoa naweza kuwakilisha ishu hiyo Mahakamani (Mahakama ya Wilaya na omba kuonana na Hakimu moja kwa moja, Hawana matatizo kabisa) na ajieleze huku akiwakilisha yote aliyopewa kule kwenye kitengo cha Sheria kinachojihusiaha na maswala ya watoto na familia ili wazazi na huyo mama mtoto waambiwe kuwa kisheria Baba mtoto (mchumba wako) anatakiwa kuhudumia mtoto wake tu na kwanini, pia Hakimu atasema wazi ni kiasi gani kitatolewa na baba kwa mwezi kwa ajili ya mtoto.


Ni kweli anapenda mtoto wake na upendo huo ni tofauti na alionao kwako, mtoto wake ni damu yake hawezi kuikimbia unless otherwise DNA test iseme vinginevyo. Wewe ni mpenzi wake na anakupenda sana tu pia anampenda mwanae kuliko kitu chochote....hiyo haina maana kuliko wewe.

Mchumba hajui namna gani ya kuwakilisha maelezo kwako ili kukuhakikishia kuwa anakupenda zaidi ya mtu yeyote hapa Duniani lakini pia anampenda mtoto wake kuliko kitu chochote hapa Duniani. Katika hali halisi hawezi kulinganisha upendo wake kwako na kwa mtoto wake kwani ni hisia za upendo za aina mbili tofauti ndani ya moyo wake.

Kama kweli unampenda huyo jamaa na unakwenda kufunga nae ndoa inakubidi ukubali mzigo alionao, kwa maana kubali kuwa kuna mtoto aliezaliwa kabla wewe hujamjua Jamaa na hivyo mtoto huyo ni sehemu ya familia yenu.

Waswahili wanasema ukipenda Boga penda na ua lake, lakini wanasahau kuwa upendo haulazimishwi. Unaweza ukapenda lakini usipendwe hivyo suala muhimu ni kuchukulia mambo kama yalivyo na kujengeana heshima ili kuishi kwa amani.


Huitaji kumpenda wala kumchukia mtoto huyo bali mchukulie kama ambavyo utamchukulia mtoto yeyote utakaekutana nae, hakuna haja ya kujilazimisha au kujipendekeza ili uwe kama "mama yake" kwani kwamwe huwezi kuwa mama yake, hakikisha Mchumba wako hamlazimishi mtoto huyo kukuita wewe "mama" akuite atakavyo yeye as long as hakutukani...MF anawezakukuita jina lako au Antie, lakini ikitokea mtoto kajisikia kukuita mama that will be fine.


Mthamini kama mtoto wa Mchumba wako, mpe ushirikiano wako kila atakapohitaji bila kuwa na hisia zozote mbaya juu ya mama yake as long as Mchumba wako anaweka kila kitu wazi kama anavyofnaya sasa, hakikisha anaendelea kukushirikisha kila anapofanya mawasiliano na mama mtoto wake huyo.

Kamwe tena ni marufuku kumwambia mchumba wako kuwa ni vema mtoto ahamie kwenu kwani siku zote mtoto wa kike anapenda kuwa na mama yake, kitendo cha kumtenganisha na mama yake hata kama ni kwa nia njema bado mtoto anaweza kukichukulia vinginevyo na hivyo mtoto huyo kuathirika.

Ni vema mtoto akaamua mwenyewe kuja kukaa nanyi moja kwa moja au kukaa kwa muda mfupi kila baada ya miezi kadhaa n.k. ili kujenga uhusiano mzuri na pia kupata nafasi ya kufahamiana.

Nini cha kufanya: Kwa vile mchumba wako kaweka kila kitu wazi, unachotakiwa kufanya ni kuacha kuhoji kuhusu upendo wake kwa mtoto wake au hata kujilinganisha kwa kusema kuwa "najua unampenda mtoto wako kuliko mimi", badala yake anapomzungumzia mtoto mpe ushirikiano na ikiwezekana ushauri wa kujenga na sio kubomoa ikitokea kaomba ushauri kutoka kwako. Hiyo Mosi.

Pili, Ondoa shaka juu ya uhusiano wa mchumba wako na mtoto wake, chukulia uhusiano wake huo na mtoto wake ni mfano mzuri kwako kujua yeye ni baba wa namna gani na atawapenda vipi watoto wako mara baada ya kufungandoa.

Tatu, hakikisha unaulizia mtoto mara kwa mara ili kujua anaendeleaje hii itampunguzia mzigo na itampa furaha akijua kuwa wewe pia unajali kuhusu mwanae.

Nne, zingatia masomo yako ili ufanye vema kwenye mitihani yako ambayo ni ndio msingi wa maisha yako ya baadae kama mwanamke anaejitegemea.

Ni matumini yangu kuwa maelezo ya wachangiaji na haya yangu yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa zaidi njisi ya kukabiliana na wivu ulionao kati yako na mama mtoto wa Mchumba wako.

Nakutakia kilala kheri kwenye Masomo yako, Uchumba wenu na maisha yenu ya baadae kama mke na mume.

No comments:

Pages