"Shikamoo dada Dinah, pole na majukumu.Mimi nimfuatiliaji mzuri wa blog yako na nimeona niombe ushauri kupitia blog yako. Naitwa Angel nina miaka 23, ni mwalimu wa Seköndari moja hapa Mbeya.
Stori yangu inaanzia hapa; Mwaka 2007 Septemba nikiwa nasoma Diploma ya Ualimu huko Dodoma, kunakaka mmoja alikosea namba kwa kutuma vocha kwenye namba yangu. Mimi bila hiana nikamrudishia ile vocha na kumpigia kumwambia kaka umekosea namba.
Basi kwa kuwa nilikuwa mstaarabu kwake, kesho yake alinipigia akaniomba niwe dada yake kwani watu hufahamiana kwa njia tofauti. Nilimkubalia natukaanza mawasiliano kama kaka na dada. Yeye alikuwa Mwanza.
Baadae 2009 mwanzoni akaniomba tuwe wapenzi na kwa kuwa nilikuwa sina boyfriend kwa kipindi hicho nikamkubalia, tukawa wapenzi ingawa badohatujaonana. Nikawa naongea na ndugu zake kama shemeji yao nae akawaanaongea na ndugu zangu.
Tuliahidiana mambo mengi sana ambayo tulipanga kuyafanya mara baada ya kuonana. Mara nyingi nilipenda kumuuliza je atanipenda the way nilivyokwa kuwa mimi kwani ni mnene na wanaume wengi hupenda wanawake wembamba akawa akinijibu alichompa Mola hawezi kukikataa kwani ameamua yeye hivyo hakuna kitakachotutenganisha.
Hatimaye mwaka huu mwezi wa Nne nilienda kwake Musoma alikohamishiwa kikazi. Nampenda zaidi ya mwanzo kabla sijamuona, siku mbili za mwanzo niliienjoy kuwa nae. Tatizo likaja akawabusy sana na simu yake akichat na wanawake tofauti tofauti, sms za mapenzi na nilipokuwa nikishika simu yake alikuwa mkali kweli akidai kuwa eti namchunguza.
Usiku akilala ndio nachukua simu na kusoma zile sms,asubuhi akienda kuoga akawa anaficha simu yake. Baada ya wiki kuisha nikaongea nae kumwambia anavyofanya sivyo kabisa na kama hanipendi aseme tu kwani tulishakubaliana kuwa endapo mmoja watu hajaridhika na mwenzie aseme tu kwa uwazi.
Akasema hayo ya kutonipenda nayasema mimi yeye hana mawazo hayo kabisa, kwa kweli hatukufikia muafaka tuligombana kweli usiku ule na nikamuomba kesho yake akanikatie ticket niondoke.
Kweli baada ya siku mbili niliondoka, Nilivyofika Mbeya siku mbili za mwanzo tuliwasiliana vizuri kabisa, baadae nikawa nikimtumia sms hajibu na nikimuuliza kama kuna tatizo anadai hakuna na anaomba tuache kuwasiliana kwa muda then atanitafuta. Nikamwambia kama anataka tuachane aseme tu , lakini hakujibu na alikata simu.
Kitendo hicho kiliniumiza sana kwani nashindwa kabisa kufundisha wanafunzi kwangu kila nikiwaza promise tulizopeana mwanzo na vituko anavyonifanyia sasa nashindwa kabisa ku-concentrate na kazi zangu.
Nampenda saaana tu ila nashindwa nifanyaje ili nijue anawaza nini kuhusu mimi na hisia zake kwangu zikoje?naomba ushauri.
Asante, Madam Angel-Mbeya"
Dinah anasema: Angel asante sana kwa ushirikiano, ni matmaini yangu kuwa maelezo kutoka kwa wachangiaji yatakuwa yamesaidia kwa kiasi fulani kujua nini cha kufanya ili kupana amani na hivyo iwe rahisi kuendelea na maisha yako.
Huyo mwanaume (kutokana na maelezo yako) hana mapenzi na wewe alitaka kukutumia kama anavyotumia hao wanawake wengine, na usikute anatumia mtindo huo wa kutuma sms kwenye simu za wanawake ili kuwapata kiurahisi kama alivyofanikiwa kwako.
Na mara baada ya kupata alichokitaka ndani ya siku mbili ulipokwenda kumtembelea alihamisha hisia zake kwenye simu yake, Mshukuru Mungu kuwa mwanaume huyo alionyesha wazi tabia yake ilivyo ukiwa nae karibu imagine ni mangapi anafanya ukiwa Mbeya?
Huyu mwanaume kama walivyo Players wote huwa hawataki kuonekana kuwa wao ndio chanzo ya uhusiano kufa ili wakiishiwa huko waliko waweze kurudi kwako na kuomba uhusiano wenu uendelee kwa madai kuwa wewe ndio ulimuacha lakini yeye hakufanya hivyo.
Player yeyote akiona uko serious na uhusiano atakuambia "nitakutafuta" kwa maana nyingine anasema "usinisumbue na nikihitaji huduma yako nitakuambia"......hii inamaana kuwa mwanaume huyo hakufai na ukiendelea kutegemea siku atakutafuta utakuwa unajipotezea muda wako bure na kujipa maumivu ya moyo juu ya mtu ambae hathamini utu wala effort yako kwenye uhusiano husika.
Najua unahisia kali za mapenzi juu yake na hii inaweza kuchangiwa na umri wako kuwa mdogo na hivyo unashindwa kutofautisha hisia za kikware (last) na zile za kimapenzi (love) zote zinafanana sana kwa kuanzia lakini moja hudumu na nyingine huisha....sasa alichokuwa nacho huyo mwanaume juu yako ni Ukware na sio mapenzi.
Vievile nahisi kuwa kutokuwa ulikuwa na matarajio makubwa/mengi juu ya uhusiano wako na mwanaume yeyote kukutaka kwa vile unahisi kuwa umekamilisha mahitaji kimaisha isipokuwa mume, kwamba umemaliza masomo, unajitegemea kwa kufanya kazi na kinachokosekanakwenye maisha yako ni mtu wa ku-share nae maisha yako.
Huna haja ya kujua anawaza nini juu yako kwani amekwisha liweka wazi hilo kuwa hakuna mwanamke yeyote anaemthamini na kila mwanamke kwake ni "sanamu" la kuchezea na fashion ikipita anatupilia mbali na kwenda kununua the latest one.
Badili mawasiliano yako ili asiweze kuwasilianana wewe, pia futilia mbali namba yake ili usishawishike kuwasiliana nae unapojisikia mpweke (we all have those days), jaribu kubadili mtindo wa maisha yako hasa kwa kufanya mazoezi mepesi nakubadili ulaji wako kama unadhani kuwa ukubwa wa mwili wako ni kitu ambacho kinakukwaza.
Kwa kufanya hivyo utakuwa umejiongezea hali ya kujiamini zaidi kama mwanamke mdogo, mrembo, alieenda shule na mwenye kujitegemea kiuchumi. Tumia muda wako mwingi kuongea/kujichanganya na watu wanaokujali nakukupenda (ndugu, jamaa na marafiki).
Hakikisha unajiweka busy na jitahidi ku-focus zaidi kwenye Taaluma yako ili usijepoteza kazi kutokana na utendaji wako mbaya unaosababishwa na mawazo juu ya mtu amabe hana umuhimu wowote kwenye maisha yako.
Mungu atajaalia na siku moja utakutana na kijana mwema, mwenye kuheshimu na kuthamini mwanamke, mwenye upendo wa dhati na kwa pamoja mkapendana na hatimae kufunga ndoa. Yote hayo yanawezekana kwani Angel wewe bado ni mdogo na una muda mwingi wa kujipanga upya na kufurahia maisha yako kama mwanamke anaejitegemea kabla hujajikita kwenye masuala ya kimapenzi na mahusiano nahatimae kuwa Mke na mama kwa watoto wako.
Kumbuka ukiwa mke na mama hutopata muda wa kufurahia maisha yako wewe kama Angel bali mke na mama kwa watoto wako.....maisha yako yatabadilika in good way, lakini itakuwa great kama utakuwa ume-enjoy uanamke wako kabla hujawa na majukumu mengine ya Mke na mama.
Kila lakheri!
No comments:
Post a Comment