Wednesday

Hata sijielewi...

Shikamoo dada dinah, pole kwa kazi na hongera kwa kutuelimisha. Mimi ni
mwanamke mwenye umri wa miaka 26 naomba unipe ushauri kwani mpaka sasa sijielewi.


Mwaka 2005 nikiwa Kidato cha pili
nilijiusisha na mapenzi nikapata Mimba 2006 mwishoni, mwenye mimba
nikamueleza akaikataa. Yeye alikuwa mwanafunzi wa Chuo lakini Mama
wa uyo kijana alinihudumia kipindi nimejifungua mtoto ila kwa bahati mbaya akafariki.

Kwavile nilikuwa nampenda yule Kijana nikamsamehe tukawa pamoja lakini hakuwa mwaminifu na tabia yake ilinishinda nikaachana nae 2010 mwezi wa Tisa.


Nikiwa Chuoni mwaka 2011 nilianzisha uhusiano wa kimapenzi na Kijana mwingine ambae aliniahidi atanioa akanitambulisha kwa ndugu zake na Mwaka 2012 mwezi wa
Sita nikapata mimba.


Akaniambia nitoe Mimba kwani hayuko tayari kulea lakini mimi nikagoma kutoa na kumwambia sitoshindwa kulea mwanangu kwasababu nilikuwa
nafanya kazi. Huyo kijana hafanyi kazi na tulikuwa tunaishi Mikoa tofauti.

Nilikuwa namfata huko aliko, natumia hela zangu kwa mahitaji yake yote na akiwa na shida nilimtumia hela, lakini akanikataa nikalea Mimba lakini nyumban wanahitaji wamjue baba wa mtoto.

Nikakutana na Baba ambae ni Mume wa mtu, huyu baba kanihudumia katika kipindi kigumu nilichopitia naogopa
kumwacha sababu alinitendea mema sana.

Wakati huo huo kuna Kijana mwingine ambae nimejuana nae kwa Miaka Kumi na Mbili. Kwa sasa hana kazi ila anasimamia Miradi ya kwao, nikitumiwa hela na yule Baba(Mume wa mtu) natumia nae lakini hajui inatoka wapi.

Sasa yule Kijana amenambia niendelee na yule Baba kwa kuwa alikukuta nae kwani hawezi kunikataza. Akasema kwa sasa hana hela hawezi kunihudumia ila atapata. Kijana wa watu akalia nami nikalia kwasababu iliniuma.

Nampenda huyo kijana kwani katika hiki kipindi kifupi kanionyesha mapenzi ambayo sijawahi kuyapata. Ananijali, ananiheshimun ananipenda na kunithamini.


Japo nampenda lakini simwamini
sana sababu wadada na wanawake wanamsumbua kwa sms na kumpigia
simu.


Huyu kaka nilikuwa nampenda toka nilipokuwa Primary Miaka 12 iliyopita sasa sijui nifanyeje. Tumeanzisha
mahusiano toka mwezi wa pili mwaka huu ndiye ninae mpenda.

Naomba ushauri dada yangu, pole na
hongera kwa kutuelimisha.

***********


Dinah anasema:Marhabaa! Ahsante na shukurani kwa Ushirikiano.

Ingependeza zaidi kama ungekuwa unafikiria Watoto wako kabla hujafanya maamuzi yako na hao wanaume. Wanao bado ni wadogo na wanahitaji full attention yako...kumbuka Baba zao wamewakataa.

Sio vema kuanza kuwaongezea wanaume holela holela maishani mwao ambao sio baba zao...Kumbuka mtoto anatunza kumbukumbu ambazo humuathiri Kisaikolojia ukubwani kuanzia umri wa miaka Mitatu.

Ni vema ukaachana na huyo Mume wa mtu ambae inaonyesha humpendi ila upo nae kama "malipo" kutokana na wema wake wakati wa matatizo. Mume wa mtu ataongeza "mzigo" wa aibu kwa watoto wako hasa kama jamaa anawatoto.....Hawana baba alafu Mama kazaa na Mume wa mtu(kwa mfano ikitokea unashika Mimba tena).

Ni vigumu kumuamini Mpenzi wako Mpya kutokana na ukaribu wake na wanawake....lakini huna nguvu ya kumuambia aache mazoea hayo wakati wewe ulimkubali ukiwa na Mtu mwingine(mume wa Mtu).

Uwezekano ni Mkubwa akawa anatoka na mwanamke mwingine ili muwe sawa...kwamba yeye anakuiba kutoka kwa Mume wa mtu na wewe unamuiba kutoka kwa mtu mwingine.

Pamoja na kumpenda ni vema ukafanya "jaribio" ili ujue kama mpo kwenye Jahazi moja au anakutumia ili kukidhi mahitaji yake Kiuchumi.

Acha mazoea ya kumpa pesa(kutumia nae) huyo kijana kwani atazoea vibaya....yeye ni Mwanaume anapaswa kutafuta namna ya kuingiza Kipato ili mkichanganya msaidiane. Mpe ushauri ili aombe kulipwa kwenye hiyo Miradi anayosimamia...hata kama ni ya Kifamilia ni vema akapewa "kifutia jasho".

Baada ya "jaribi" na ukagundua jamaa anakupenda pia basi endelezeni uhusiano wenu na muone utakavyokwenda.

Pesa zako zitumie kwa watoto (wekeza kwa watoto), kumbuka yeye hana watoto na wewe unawatoto Wawili ambao hawapati Msaada kutoka kwa Baba zao. Hakikisha watoto wanapata Elimu nzuri, wanakula vizuri, afya njema na wanapata mahitaji mengine Muhimu.

Natambua unamaisha yako kama mwanamke na ungependa kuwa na mpenzi, lakini kwa vile sasa wewe ni Mama badilisha mpangilio wa Maisha yako (priorities)....Watoto kwanza, Kazi pili, kisha Wewe alafu wengine wafuate.

Vyovyote utakavyoamua hakikisha watoto hawawazoei wanaume unaotoka nao, kwasababu wakiwaozoea kisha baadae mkaachana....itaongeza athari kwa watoto Kisaikolojia hapo baadae (wakikua).


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

No comments:

Pages