Thursday

Mume Mbishi au apenda Changamoto?

Hongera kwa kuokoa Ndoa za walio wengi mimi ni mfuatiliaji wa blog yako kwa muda sasa na ninapenda saaana kazi zako. 

Kiufupi mimi ni mwanamke nimeolewa miaka miwili iliyopita na nimebahatika kuwa na mtoto mmoja. Naomba ushauri ambapo sijui tatizo ni la kwangu au ni la mume wangu au ndio kukosa hisia!

Ni kwamba nahisi Mume wangu hana hisia nami kwa sababu zifuatazo;

1. Huwa hanisikilizi kama zamani na amekuwa mbishi kupindukia anaweza kubishana na hata mtu mzima kumzidi, mimi ndio usiseme.

***********

Dinah anasema: Mumeo amekuwa na huenda Upeo wake umepanuka kwamba anauelewa wa mambo mengi kwa undani kuliko ilivyokuwa awali (mlipokutana).


Kubishana sio tatizo kwani inakusaidia kuweka wazi Mawazo yako wazi kuhusu issue inayozungumziwa, muhimu ni yeye kutoa nafasi ya kukusikiliza na wewe umpe nafasi ya kujieleza(weka mawazo yako wazi).

Kuhusu kubishana na mtu mzima kuliko yeye ni dalili kuwa anajitegemea kiakili na anajua kuwa anahaki ya kusikilizwa na kuweka maoni yake wazi....kuna watu wanapenda "debate"....ni sehemu ya "character" yake kama yeye.

Jaribu kuzungumza nae na kumuambia tabia yake ya kubishana kuhusu kila jambo haikupendezi na inakunyima amani, ni vema mjifunze kuzungumza (kuwasiliana) kama Wenza.
*************

Anaweza kuondoka na asiseme anakwenda wapi kwa kweli mimi huwa ananiudhi inafikia hata kipindi namchukia.

**********


Dinah anasema: Hili pia ni suala la kuzungumza na Mumeo na kumuambia kuwa ni muhimu kuanga na kukuambia anakwenda wapi na kwasababu gani ili kukuondolea hofu na usumbufu wa akili kwani Dunia inamengi na lolote linaweza kutokea muda wowote na wewe usijue kama Victim ni Mumeo au la!
***********


2. Hana shukrani hata upike vizuri kiasi gani, upambe chumba au hata nijipambe mwenyewe hawezi kunisifia sasa huwa sijisikii vizuri pale ninaposifiwa na watu wengine wakati wa kunipa faraja ni yeye....ila utamsikia mmh leo mmmh leo. 

*********

Dinah anasema: Huenda alipata Malezi mabaya, hakufundishwa manners nzuri(na muhimu Maishani) ambazo kila Mzazi anapaswa kumfunza mwanae tangu akiwa Mdogo nazo ni Kushukuru, Kuomba, Kusalimia, Kuaga, Kubisha(Hodi) n.k.


Kwenye kukusifia kuhusu Muonekano wako sio muhimu ailimradi tu mwenyewe unajijua umependeza, lakini kama kwako ni Muhimu na inakufanya ujisikie vizuri au kukufanya ujiamini basi weka wazi kwake mnapozungumza au mkumbushe(kama anajua anapaswa kukusifia ukipendeza).

**************


3. Hanifikishi kama zamani, siku hizi akipiga kimoja hoi ndio nitolee hiyo wakati mwanzo alikua anaenda hata round nne kwa siku na si za masihara ni za ukweli!


**********


Dinah anasema: Jinsi siku zinavyokwenda Mwili wa mwanadamu hubadilika! Hivyo inawezekana mwili wake hauwezi tena au anahitaji "kuhamasishwa" zaidi baada ya hicho kimoja. 

Halafu pia Wanaume wengine huwa Hodari wa Mizunguuko pale mwanzo wa uhusiano ili mwanamke usikimbie....na vile mnaonana mara chache basi "anajitunza" mwenyewe ili akija au ukienda mfanye mapenzi kufidia siku Saba zijazo na Saba zilizopita!

Lakini baada ya ndoa anakuwa na uhakika wa kukupata muda wowote hivyo haitaji ku-show off "uhodari" wake ana-relax a bit. AGAIN....zungumzeni kuhusu hili pia na mkubaliane kurudisha "moto" kwenye uhusiano wenu.
************

4. K yangu ni ndogo sana inanifanya hadi niumie kila wakati hata kama mume wangu ataniandaa kwa masaa matano mwisho wa mchezo naambulia maumivi sasa tatizo sijui nini? 


***********

Dinah anasema: Sasa mrembo walalama Mizunguuko Michache, hapa unasema unaambulia Kuumia, huoni hicho kimoja ni afadhali kuliko viTano eti?!!


Hakuna Uke Mdogo linapokuja suala la kufanya Ngono ailimdari kuna Ute wa kutosha Nje (mwanzo wa Uke) na ndani kusaidia Uume kuingia na Misuli ya Uke ku-relax jinsi anavyoingia taratibu(hatua kwa hatua).

Lakini kutokana na yote uliyoelezea hapo juu ni wazi kuwa unapoteza hamu ya Tendo hivyo hata akikuandaa kwa muda mrefu Misuli ya Uke wako inashindwa ku-relax kwasababu wewe huja-relax akilini kutokana na maudhi ya Mumeo.

Kumbuka kupata Ute sio kielelezo kwamba upo tayari kwa Tendo (kuingiliwa)....jaribu kumaliza issues zenu kwa kuzungumza na kuelewana ili wote kwa pamoja muweze kufurahia Ndoa yenu.
**************

Kiufupi da dinah nampenda sana mume wangu na sitamani kumkosa ila kwa tabia sijui hata nitamrekebisha vipi.

Na nikimkubaria kila kitu anasema simpendi kwa nini niwe namkubalia kila nachosema na nikimkatalia pia  ni hivyo hivyo nifanye nini jamani au mimi ndio namkosea sijui jinsi ya kuishi nae?!!

**********

Dinah anasema: Ahsante Mrembo, shukurani sana kwa ushirikiano.


Nimejitahidi kujibu kila swali papo kwa hapo ili nisikuchanganye.


Hilo la mwisho nitalijibu hivi:- Wanaume wa Kisasa wanapenda Changamoto, hawapendi ile "ndio bwana" kwenye kila jambo kwani haiwasaidiii.


Kama nilivyogusia awali, inaonyesha Mumeo amepanuka kiupeo na ana-enjoy changamoto au anataka kupata Maoni yako kuhusu jambo analokuambia.

Hategemei kukubaliwa au kataliwa moja kwa moja/haraka hali ambayo wewe unadhani ni "umbishi".


Ndoa yenu haina Mawasiliano na inaelekea hamkujipa nafasi ya kujuana zaidi kabla ya Ndoa, matokeo yake kila jambo unaona "jipya".

Kuwa pamoja kwa Muda mrefu kabla ya Ndoa sio kithibitisho cha kujuana zaidi (usichanganye), bali Uwazi kwenye kujieleza kuhusu Malezi yenu, Wepesi wa kuhoji, Uhuru wa kuweka wazi au kuonyesha "good manners" n.k.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Monday

Ushauri wa Kimaisha

Dada Dinah Habari za Kazi? Mimi ni mdada mwenye umri wa miaka 35 nina watoto wawili wenye baba tofauti. Wa kwanza ana miaka 16 na wa pili ana 12.


Hapo nyuma nilikuwa sipo vizuri kimaisha kwani nilikuwa sina kazi. Baada muda nikapata kazi Mkoani, nikafanya kama miaka miwili hivi.


Then nikapata kazi yenye maslahi zaidi ya kule kwa mwanzo Mkoa mwingine, ambako ndio nyumbani kwetu kabisa kwa wazazi wangu.

Nilipokuja kuripoti nikafikia nyumbani hadi hii leo, kwani toka nianze nina
kama miezi sita hivi.

Tangu watoto wamezaliwa wamekuwa hapa kwa wazazi hadi hivi leo hii kwani  wazazi wangu hawataki niwachukue
nikakae nao mwenyewe.


Kwa hiyo hadi hii leo wote tupo hapa nyumbani ila najipanga
kuhama.

Swali: kuna vitu viwili ,vinanichanganya nina kahela kangu nawaza je nifungue biashara au nirekebishe nyumba ya wazazi wangu?

Yaani najiuliza sipati jibu kwani nyumba nayo ni ya kizamani sana naomba unishauri dada Dinah nijiongezee kipato kwa kufungua biashara
au nianze na ukarabati wa nyumba yetu?

Yote ni muhimu kwani napenda wazazi wangu wakae kwenye nyumba nzuri, nianze kwanza kukarabati nyumba then biashara ifuate au?


Kumbuka hao watoto mimi ndio baba na ndio mama maana sijaolewa na umri umeenda. Ningependa ufiche email yangu. Asante.

**********


Dinah anasema: Habari ni njema, shukurani kwa ushirikiano.

Najua kuna hisia ya Hatia inakusukuma au kukufanya utake kuanza kukarabati nyumba ya wazazi wako kama shukurani!

Lakini kumbuka ilikuwa chaguo lao kuwachukua watoto, hukuwalazimisha au kuwaomba wakusaidie hivyo huna haja ya kurekebisha nyumba kwasababu ya kuhisi "guilt" na badala yake fanya kitu ambacho una uhakika kitazalisha Pesa ulizonazo.


Biashara itakuwezesha kurekebisha Nyumba yenu, kuwasaidia kujikimu na wakati huohuo kutakuwa na muendelezo wa kipato cha pili kuingia.


Lakini pia, unaweza kufanya yote kwa wakati mmoja, endelea kubaki hapo kwa wazazi ili senti za kulipia Nyumba ya kupanga (kutoka kwenye Mshahara wako) ndio uitumie kurekebisha Nyumba ya Wazazi wako taratibu(kila mwezi). Na hizo pesa za pembeni zikafanye Biashara unayotaka kuifanya.


Nina Imani kuwa maelezo haya yatakupa mwanga zaidi, nafurahi kuwa sehemu ya Maamuzi yako Muhimu ya Kimaisha.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Mchumba Hanipendezeshi...

Shikamoo da Dinah.
Asante kwa kutuelimisha na mungu akubariki sana.

Da dinah naomba ushauri wako kwa hali na mali maana nipo njia panda. Mimi ni mwanamke 27yrs nipo kwenye mahusiano miaka 4 sasa na tumebarikiwa kuwa na mtoto mmoja.

Tunatarajia kufunga ndoa miezi mitatu ijayo na tunaishi pamoja. Tatizo langu ni kwamba mimi nina mpenzi binafsi sana yeye hanifikilii kabisa anajipenda yeye tu.

Mimi nimemaliza Chuo na sina kazi kwa sasa, kwa kipindi cha nyuma kidogo nikiwa mwanafunzi nilikuwa nikijishughulisha na vibiashara vyangu ambavyo vilinisaidia kufanya mambo mengi pamoja na kujiendeleza kielimu na maisha kwa ujumla.


Nilikuwa simwombi huyo mpenzi kitu chochote, lakini mimi kama mwanamke siku zote nimekuwa nikimtekelezea mpenzi wangu anachohitaji kutoka kwangu na kujaribu kuremba penzi letu.

Katika suala la kunipenda naona ananipenda na hawezi kukaa mbali nami hata akisafiri kikazi basi atajitahidi kutekeleza majukumu arudi kabla ya siku  alizotakiwa kukaa huko.

Mawasiliano ni mazuri akiwa hayupo nyumbani hawezi kupitisha masaa mawili bila kunipigia LAKINI akiwa nyumbani ndiyo tunawasiliana vizuri but kuna wakati ana majibu mabaya sana kiasi kwamba hunifanya nipoteze mapenzi kwake.


Nashindwa kumwelewa huyu mpenzi wangu, tangu tumekuwa wapenzi hanijali mimi kama mwanamke wake haninunulii nguo, hanipi pesa ya Saloon hanifanyii kitu chochote kinachonihusu mimi binafsi.

Mimi ni mwanamke ninaejipenda kweli kwa kipindi cha nyuma nilijimudu mwenyewe kama nilivyoeleza hapo mwanzo lakini niliacha kila kitu baada ya kuwa Mjamzito, maana niliumwa sana. Hata baada ya kujifungua afya yangu haikuwa stable mpaka sasa.


Nikimwambia baby naomba pesa nikanunue nguo hizi zimechoka, nguo navaa miaka mitatu hizo hizo out of fashion kama unavyojua sisi wanawake inatakiwa tuwe nadhifu!


Lakini nitaambiwa nitakupa basi inaishia hapo. Cha ajabu yeye binafsi anajipenda sana ni kawaida kununua vitu vyake binafsi kama nguo au viatu kila mwezi tena vya bei ghali laki ngapi huko na saa zingine ataniita dukani mzigo mpya umeingia nimchagulie vitu vizuri lakini mimi mpenzi wake hanifikilii hata siku moja!

Kipato sio tatizo ana huo uwezo nikimwambia ataniahidi tu itaishia hapo nasindwa kuelewa tatizo nini?


Da dinah kuna wakati nahisi hanipendi labda yupo na mimi kwa sababu anajua nitamsaidia kujenga family basi, natamani hata siku moja mpenzi wangu anipe zawadi lakini hakuna!

Mpaka kuna wakati anasema "najinunulia mimi tu ngoja mke wangu usijali nitakupendezesha tu subiri" hapo unakuta anapima nguo kaniona mie mnyonge.

Najisikia vibaya na nahisi kama hana mapenzi ya dhati kwangu sababu tofauti na hayo kuna mambo mengi anayostahili kunisaidia ktk future yangu ( kusaidiana) lakini hakuna kitu.

Mimi nimekuwa nikimpa support kwa kila kitu niwezavyo lakini mwenzangu hapana. Nahisi  sina furaha na nimemchoka sasa natamani hata niachane nae na vikao vya harusi ndio vimeanza naona kama ananitumia kujifurahisha tu.

Niliona aibu siku nimeenda nyumbani kwetu Mama yangu amechukua pesa zake akaenda kuninunulia nguo, pochi na viatu ananiambia mbona nimevaa vitu vya zamani nami ni mke wa mtu hivi they expect to see me shining nilishindwa kumweleza ukweli.

Naomba ushauri wako da dinah nipo taabani.

************


Dinah anasema: Marhabaa Mrembo, shukurani kwa Ushirikiano.


Sasa siku ya Ndoa utavaa nini Mrembo? Usijejikuta unavaa gauni lako la mwaka juzi ambalo haliendani na sherehe husika na yeye anawaka na Suti Mpya!

Kabla sijaingia ndani! Makubaliano yenu yalikuaje? Malezi? Uchumi? Mipango na je mlikubaliana kuzaa au ilikuwa "bahati mbaya"?

Kwasababu mtu huwezi tu kuacha shughuli zako/Elimu ili uzae wakati hujui utakaezaa nae atakuangalia au mtasaidiana vipi (kama ni Mchumba/Mume)?


Mambo ya kushika Mimba kiholela ukitegemea Mwenye Mtoto atakutunza bila mipango ya mbeleni ni Uzamani na husababisha matatizo makuu kwa mwanamke, moja ni kama hili ulilonalo wewe.

Huyu mtarajiwa(mume) sio mbinafsi, angekuwa mbinafsi asingekuwa akiijali familia yake kwa mawasiliano na kukatisha safari zake ili awahi kurudi Nyumbani.

Kwani nani huwa ananunua mahitaji muhimu ya hapo nyumbani? Je huwa Mpenzi wako anakupatia Senti za manunuzi ya kila Siku/Wiki.....je huwezi kuwa unabajeti na ku-save kwa ajili yako?!!

Nadhani ama ulimzoesha kwa kujifanyia kila kitu mwenyewe bila kumshirikisha(ile twende shopping na kununua vitu pamoja) pale uhusiano wenu ulipoanza na wewe ukiwa unajitegemea Kiuchumi.

Wengi wainachanga hii "kujitegemea kiuchumi"....mwanamke kujitegemea kiuchumi haina maana anachukua "jukumu la mwanaume" kwenye familia/uhusiano au Jamii!

Au Mbahili....maana kuna aina mbili za Wabahili....(1)-Hawataki kutumia pesa zao kabisa (2) wana-prefer kuzitumia kwa ajili yao kuliko wenzao.


Pamoja na kusema hivyo inaonyesha wazi uhusiano wenu unakosa Nguzo kuu mbili ambazo ni Mawasiliano(sio kupigiana simu na kujuliana hali) bali kuzungumza kama Wenza na Ushirikiano.

Wenza huzungumzia mengi kuhusu maisha yaliyopo na yale yajayo, kupanga Mipango....Mipango ikiwa ni pamoja na "shopping" ya chakula na Mavazi sio kujenga na kufanya miradi.

Wenza hushirikiana kwenye kila kitu bila kujali nani anaingiza Pesa na nani hana Kipato.


Kabla hujakubali kuzaa nae au kufanya mapenzi bila KUJIKINGA dhidi ya Mimba ulipaswa kuzungumzia na kukubaliana "future" yenu kama wapenzi.....mtafanya nini kuhusu malezi ya Mtoto ikiwa mtazaa?.....utakapojifungua hutorudi kwenye shughuli zako, je mtasaidiana vipi mpaka utakapo kuwa tayari kurudi "job"? N.k.

Hii ni 2000s sio 80s Mrembo, hakuna kuacha kazi inayokuingizia Kipato na kuchanua Miguu bila Kinga wakati hujui kilicho mbele!!

Sasa fanya hivi; Mkiwa mmekaa vizuri na hakikisha anakusikiliza, anza....Mpenzi (Tumuite Paul) Paul hivi unajua kabla sijakutana na wewe/sijazaa nilikuwa najipenda sana?!! Ningewa kama nilivyo hivi sasa walahi usingevutiwa na mimi na tusingekuwa pamoja!

Mwanamke nimechakaa mpaka najichukia....navaa nguo za Miaka 3 iliyopita lakini Mume wangu unag'aa mpaka napata aibu!

Kila nikiomba senti za Shopping, mwenzangu unanipa ahadi zisizotekelezwa.....sasa mpenzi kama hutaki kunipendezesha Mkeo basi naomba Mtaji ili nifanye Biashara na ikilipa nitakurudishia.

Pia inabidi tutafute Msaidizi (Nanny) au tumpeleke mtoto Chekechea maana sitokuwa na Muda wa Kumuangalia hapa Nyumani.


Msikilize atakujibu nini?.....akikupa ahadi! Demand muda maalum kwani hutaki kupoteza muda!


Akilalama kuwa mtoto bado ni Mdogo na anahitaji Mama zaidi ya Msaidizi (kama mtoto ni chini ya miaka 4) basi Jaribu kumuelewesha(wanaume wengine hawajui) na mkumkumbushe jukumu lake kama Mumeo na Baba bila kufoka wala hasira ila kuwa firm(serious)!

Wanaume wengine walilelewa ovyo, kwamba wao ni majina na Maumbile tu, lakini hawajui majukumu yao mpaka wakumbushwe au kushikwa mkono na kuelekezwa.

Suala la yeye kuwa na majibu ya hovyo ambayo yanakufanya upoteze "mapenzi" itakuwa ngumu kwangu kusema lolote kwani hukuwa wazi kwa kueleza Majibu yake hayo hutokana na maswali ya aina gani kutoka kwako?

Siku nyingine (baada ya hili la kurembwa kupita na kufanikiwa)....rudini kwenye Nguzo ya mawasiliano tena, na mzungumze kuhusu hilo.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Friday

Chuki ya Mzazi kwa Mpenzi...

Dada habari za wakati huu mimi ni kijana wa kati nina mpenzi wangu ambae tunapendana sana pia tumefikia hatua ya kukubaliana kuoana.











Uhusiano wetu sasa una mwaka na nusu tatizo limetokea upande wangu ambapo mzazi wangu anaonesha hali ya kutompenda huyu nimpendae.











Halafu mara nyingi humuonesha Mpenzi wangu na sio mimi yaani hajaniambia hamtaki sasa mpenzi wangu anaumia coz tunapendana kweli nae anaogopa baadae inaweza kutokea akajateseka.











Sasa hii imeleta hofu ya kuishi na mimi na sijui nifanye nini maana amekata tamaa kiukweli, naumia sababu sihitaji kumkosa kwani nampenda sana.







***********



Dinah anasema: Habari ni nzuri kabisa, ahsante na shukurani kwa ushirikiano.









Issue yako ni ngumu kuhakiki na sio vema kwenda kumuuliza Mzazi wako kwanini anaonyesha kumchukia mpenzi wako wakati huna uhakika.









Pia huwezi kumkatalia Mpenzio kuwa anachosema au kukiona kutoka kwa Mzazi wako ni Uogo!











Mapenzi ni ya wawili hivyo mwambie mpenzio kuwa wewe ndio umechagua kuishi nae na unampenda. Kuwa na wewe sio kuwa/kuishi na Mzazi wako kwazi Mzazi wako alikuwa na maisha ya yake ya Ujana na mpenzi wake na yamepita, haya ya sasa ni yako wewe na yeye.









Baada ya kumhakikishia mpenzi wako Msimamo wako na hisia zako kwake, anza kuweka "ukuta" baina yao....yaani Mpenzio na Mzazi wako.











Hakuna haja ya Mpenzi wako kwenda kwa Mzazi wako.....yeye anakupenda wewe na sio lazima ampende Mzazi wako au Mzazi wako ampende huyo Binti(Upendo haulazimishwi).











Suala muhimu kwao hao wawili ni heshima, so long mpenzi wako anamuheshimu Mazazi wako na Mzazi wako anamheshimu mpenzio inatosha.











Ni kawaida kwa Wake(hasa wanawake) kudhani kuwa wana nguvu sana kwenye maamuzi ya kimapenzi ya watoto wao kwa sababu tu waliwazaa.











Baada ya kuweka "ukuta" kati yao(hawaonani) fanya uchunguzi kivyako ili ugundue ukweli kuhusu Chuki ya Mzazi wako kwa Mpenzio au Mpenzio kwa Mzazi wako....maana baadhi ya wanawake huwa na yao!





Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Thursday

Hanitaki kwake kisa Ex ni rafiki wa Dada'ke!

Habari za kazi pia pole na majukumu, hongera kwa kazi nzuri ya kutushauri wadau, mimi nikiwa mmoja wao!

Dada dinahicious mimi ni mwanamke umri wangu ni miaka 30 kwanza napenda kukufahamisha kuwa nimepitia mahusiano kadhaa ingawa sio mengi kihivo!

Tatizo langu linalo nisumbua sasa kwa huyu bwana niliyenae ni hili, nimeanza mahusiano nae ya kimapenzi mwezi wa Kwanza mwaka huu 2014 hadi leo hii tarehe 18.8.2014 ninavyoandika mail hii tuna miezi 7 na wiki kadhaa ingawa tumefahamiana tangu mwaka 2009.


Mwenzangu ana umri wa miaka 38, wakati tunaanza mahusiano alinieleza kuwa alikua na mke na akabahatika kuzaa nae watoto 2. Waliacha kutokana na sababu zao ambazo alinieleza nikaridhia ingawa kwa maelezo yake ni kwamba sababu za kuachana ni Usaliti wa mkewe.

Kabla ya kuanzisha mahusiano na mimi tulika tukiheshimiana sana mwisho wa siku tukaamua kuwa wapenzi kwa kifupi historia yake ni hiyo na hakunieleza kitu kingine zaidi ya suala la kuachana na aliyekua mke na mama wa watoto wake.


Nami pia nilikua nimeachana na mpenzi wangu takribani mwaka na miezi kadhaa nilikua naishi mwenyewe, ila tatizo linalonisumbua ni kutopajua anapoishi hadi hivi ninavyo andika email hii kwako!

Tulienda na hali hiyo baada kufikisha miezi 2 nilishindwa kuvumilia maana nilistaajabu kuona hakuna siku aliyoniambia karibu nyumbani kwangu na hali yeye anafika nyumbani kwangu na yupo huru sana.


Nikamwambia naomba nipajue unapoishi akasema utapajua usiwe na shaka na akaniambia kupajua anapoishi sio defence ya mahusiano yetu natakiwa kuangalia moyo wangu unasema nini kwake na moyo wake unasema nini kwangu na kusisitiza kua ananipenda na anamalengo.


Baada ya hapo alinifahamisha jambo linalomfanya ashindwe kunipeleka kuwa baada ya kuachana na mkewe alijikuta anaanzisha mahusiano na msichana ambaye hakutaraji pia hakua na malengo nae msichana huyo.

Aliniomba msamaha kwa kutonifahamisha hilo, alinisihi sana nisimwache pia akaniomba nitulie anitengenezee mazingira salama na akadai pale nyumbani anaishi yeye na wadogo zake 2 moja wa kiume na mwingine ni wakike hivyo binti aliyeanzisha mahusiano nae anaurafiki sana na mdogo wake wa kike hivyo mara nyingi huyo binti amekua akipendelea kwenda pale nyumbani kwa sababu hawakai mbali sana.

Yeye kuishi na wadogo zake aliniambia mapema pia akasema anawaheshimu wadogo zake hivyo nimpe muda asitishe mahusiano na yule bila kutumia nguvu nyingi.


Kiukweli nilimwelewa sikuendelea tena kumuhoji kuhusu hilo, tumeendelea na mapenzi hadi mwanzoni mwa mwezi wa 8 mwaka huu nikaona suala hili linaniumiza sana kichwa pia nimejikuta natawaliwa na hasira sana wakati mwingine.


Nikamkumbushia tena kuhusu kupajua anapoishi bado akanisihi niwe na subra na kwamba amejitolea kua nami hakuisha maneno akaniambia mapenzi ni ghalama na amejitoa sadaka kwangu na kauli hiyo alikua anapenda kuitumia toka tunaanza mahusiano mara ya kwanza nilikua simwelewi mara nyingi alikua akiniambia unajua nimejitoa sadaka kwako kwa lolote.


Wakati mwingine ananiambia unajua mapenzi ni ghalama sana kwa siku hizo nilikua simuelewi ila nikaja kumuelewa alichokua akimaanisha kiukweli inaniuma sana na nimekua nikitawaliwa na hasira kila ninapolifikiria suala hili. Nimekua nikijiuliza maswali mengi sipati majibu.


Ingawa nakiri kwa kipindi chooote ambacho nipo nae kama mpenzi wangu amekua karibu na mimi sana ananijali na haijawahi pita siku bila kuonana usiku kabla ya kulala tunawasiliana.

Yeye ni mtu ambae amejiari anaofisi yake na mimi pia ninafanya kazi katika kampuni moja ambayo haipo mbali sana na ofisi yake hivyo kwa kipindi chote hicho nimekua nikitoka ofisini kwangu napitia ofisini kwake nakaa then naondoka zangu pia huwa hasiti kunitambulisha kwa watu wake wa karibu hususani marafiki zake.


Huwa tunatoka mara nyingi hasa siku za Jumamosi na Jumapili baada ya kutoka Ibadani kuanzia saa 3 huwa tunakua pamoja hadi usiku saa 5 ndio ananiaga anaenda zake kwake.

Ananipa treatment kama mke na kila anaponiona nimebadilika na kua na hasira hua haishi kunisihi nimvumilie hatanitenda kama nilivyo kueleza hapo juu kua suala la kutopajua anapoishi linaniuma hivyo nimejikuta nikiwa mtu wa kutawaliwa na hasira hasira hasa nikikumbuka.


Tafadhali naomba ushauri wako dada dinahicious pamoja na wadau kulingana na jinsi nilivyo jieleza kichwa kinaniuma stress tupuuu,


Samahani kwa maelezo marefu.


***********


Dinah anasema: Habari ni njema, ahsante na shukurani kwa Ushirikiano.


Ni rahisi sana kwa mwanaume (mume) kusema "nimeachana na mke wangu kwasababu alinitenda" lakini ukweli ukawa yeye ndio Msaliti mkuu na wewe ndio unaefanikisha Usaliti huo....Kwamba hajaachana na mkewe as in kupeana Talaka.

Ndoa yake ni ya Kikristo? Ndoa za Kikristo huwa hazivunjiki kutokana na "Maandiko" yao hivyo utakuta Mke/Mume anaendelea kuishi tu na Mume/Mke ambaye ni Msaliti.

Sioni umuhimu wala sababu ya wewe kupata hasira kwasababu hukujui nyumbani kwake....,adhani ungepata hasira kwanini yule binti (ex) bado anauhusiano na Jamaa na anaendelea kwenda kwake kwa kisingizio cha Urafiki na Mdogo wake!!

Tena kakuambia kabisa anataka "kumalizana" nae taratibu na wewe ukamuelewa REALLY?!!! Moja haku-declare kuwa na ka-ex (baada ya Mke) THEN I mean pili anakuambia "anataka kumuacha tataribu" kwa kigezo cha " "uwifi" kati ya mdogo wake na ex.


Kuna mawili nayaona hapa: Mosi, hajaachana na Mkewe ila anampango huo(wana issues zao kwenye Ndoa yao). Anashindwa kukupeleka kwake kwasababu hataki Ugomvi na Mkewe na hataki kuwachanganya na kuwaumiza watoto wake kihisia.


Hivyo anatafuta visingizio kila leo kwani hataki kuwa mkweli kuhusu familia yake, hasa watoto wake kwako kwasababu anahofia kuachwa. Ukimuacha wakati hana maelewano na Mkewe atakuwa kakosa kote.

Ujue, kuna baadhi ya wanaume waoga sana kuachwa hivyo akiona dalili za kuachwa na Mke, huwa anatafuta mtu pembeni just in case..... Ndoa ikibuma anaendeleza huko nje bila ku experience upweke(sijui unanielewa?).

Pili, anauhusiano na huyo Binti rafiki wa dada yake na wakati huohuo anauhusiano na wewe.....aka Malaya!


Suala la kukaa na wewe mpaka Late usiku na kuondoka sio kielelezo cha Upendo au Uaminifu! Anaweza kutoka kwako muda huo na kwenda kwa Mkewe au yule rafiki wa dada yake pale Nyumbani kwake.


Kuwa treated kama Mke ndio kukoje kwani? Ikiwa Mkewe anam-treat kwa kutokuwa nae muda wote anapokuwa na wewe....utasemaje anaku-treat kama Mke?

Sasa Mwanamke, ili kujua ukweli wa nini ni nini hasa ni vema kufanya Uchunguzi bila yeye kujua.

Mfuatilie nyendo zake anapokwenda kwake ili ujue nyumbani kwake ni wapi hasa, kisha kuwa Detective.... Siku nenda pale kwako ukijua hayupo na ukajitambulishe kama Mfanya biashara mwenzie au rafiki yake na una-deals au mmepanga kukutana hapo kwake!

Ukipata nafasi (ukikaribishwa ndani) au hata kwa nje, jaribu kuwa Mcheshi na kuhoji uliowakuta kiujanja....Mf: kama kuna binti na kijana unaweza kusema "wewe na huyu nani Mkubwa?"...."Baba yenu anapenda sana kuwazungumzia, anajivunia sana watoto wake"

Maelezo hayo (sio lazima yale kama yalivyo, tafuta ujanja wako mwenyewe wa kupata ukweli) yatawafanya au kumfanya mwenyeji wako kuwa comfortable na wewe.


Ana/wanaweza kusema Fulani(mpenzi wako) hana watoto au sisi sio watoto wake au watoto wake wapo blablah...


Kumbuka unachokifanya kinaweza kumpunguzia mpenzi wako Uaminifu kwako lakini unaweza kujitetea kwa kitendo chako (ikitokea umebambwa na alikuwa Mkweli).


Wewe ndio mwenye Mamlaka na furaha yako, mwenye uwezo wa kuchagua aina gani ya maisha unataka kuishi.....kama mtu mwingine anakusababishia usumbufu wa akili na haonyeshi kukuelewa au hamuelewani basi huna haja ya kupoteza Muda.

Wengine wataongezea....
Kila la kheli.

Mapendo tele kwako...

Monday

Nilimuacha, sasa namtaka tena...

Natumaini umzima bukheri wa afya, dada Dinah mimi ni kijana ambae

nilikua na mpenzi na tulipendana sana ila nilimuacha kutokana na

Wivu wangu wa kijinga.













Sasa nina mawazo sana kwasababu bado nampenda kiasi cha kunifanya nisongwe na mawazo mpaka kufikia kuumwa.











Bado namuhitaji mpenzi wangu ila sijui nianzie wapi maana alinivumilia

kwa visa vingi nilivyomtendea na sasa ameamua kunisahau kabisa.









Tafadhali dada dinah naomba unishauri nifanyaje maana naumia sana na

nahitaji turudiane.





***********





Dinah anasema: Namshukuru Mungu, ansante kwa ushirikiano.







Kuna msemo huku unaenda hivi "She will love you, she will cry, she will ask why, she will hate you, she will forgive you, she will love you again.....but one day she'll go and never come back".











Mtu anaweza kuvumilia visa na vituko lakini ipo siku moja akipata "akili" ya kuondoka au kwa bahati nzuri akaachwa kama ulivyofanya wewe inakuwa ngumu sana kurudi(anagundua kuwa alivaba/kosea).....inakuwa lucky escape!











Kwasababu sijui nini hasa kilipelekea wivu wako wa kijinga na hata kumfanyia visa na hatimae kumpiga buti itakuwa ngumu sana kukupa ushauri wa nini cha "kujaribu" kufanya ili umshawishi akubali kurudi kwako.









Kabla hujaanza harakati za kuenda "kumuimbia" misamaha ya kamosa(vile Visa) ni vema kuhakikisha kuwa umebadilika na kujiamini moyoni(na akilini) kuwa hutorudia tena makosa yako kwake (akikubali) au mwanamke mwingine hapo baadae(akikukataa).











Kama unampenda kweli basi pigania penzi lako kwake haraka kabla mwingine hajawahi akamsahaulisha wewe.









Akikataa kubali kuwa sio mwisho wa Maisha yako(huitaji mtu, unahitaji hewa/chakula na maji), ipo siku nyingine utakutana na mwingine na kutokana na ulichojifunza huenda utam-treat vema zaidi huyo Mpenzi Mpya mtarajiwa.







Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Nimesamehe vya kutosha, sasa simuamini tena

Shikamoo dada dinah, pole kwa kazi.
Dada  nahitaji ushauri wako
Nina mpenzi wangu nampenda sana na yeye anaonyesha kama ananijali.

Tangu tuanze mahusiano ni miaka mitatu sasa. Kipindi tunaanza mahusiano aliniambia hana mpenzi na mimi nikamuamini, ila baada ya Wiki kadhaa mwanamke mmoja akanipigia na kudai kuwa huyo niliyenaye ni mpenzi wake!


Nilimuuliza yule mwanaume kuhusu mwanamke yule lakini yeye alikataa ila mwisho wa siku akaadmit kama alikuwa na mahusiano naye ila hamtaki tena akaniomba msamahi basi nikamsamehe.

Mwaka jana nikakuta msg kwenye simu yake anachati na mdada na huyo dada kamtumia picha za uchi nilipomuuliza alidai huyo ni rafiki yake tu, nilimuelewa na kumsamehe.

Ila kama mwezi hivi hatukuwa kwenye mawasiliano mazuri yaani ni ugomvi tu bila sababu. Siku moja nikakuta tena msg anachat na mwanamke na anamahusiano naye nilipomuuliza akasema kweli alianzisha mahusiano naye kutokana na kutoelewana kwetu na akaomba msamah nikamsamehe.


Ila  dada dinah yaani simuamini tena na nahisi bado ana mahusiano na huyo mwanamke. Nampenda sana ila simuamini kabisa na kila nikifikiria aliyonifanyia nakosa hata hamu ya kula.


Dada dinah naomba ushauri wako je nifanyeje??? Nampenda sana ila tabia yake naona inanishinda.


*************

Dinah anasema: Marhabaa mrembo, shukurani kwa ushirikiano.

Mtu kakudanganya mwanzoni kabisa mwa uhusiano utamuamini vipi? Ile ilikuwa dalili ya kwanza kuwa jamaa ni Muongo.....ona sasa umesamehe mpaka kusamehe inapoteza maana eti!

Unahitaji kusamehe mara moja na msamehewa(Mkosaji) kubadilika na kuacha uchafu wake wa tabia....akirudia kosa unanawa Mikono, unaenda kutafuta furaha bila yeye!


Kutokana na maelezo yako ni wazi huyo bwana ni Malaya na ni muoga kuachwa hivyo akiishagundua kuwa mwanamke kajua tabia yake chafu na kuna hatari ya kuachwa....anaanzisha uhusiano mpya wakati bado yupo kwenye uhusiano mwingine uliopo "hati hati".

Sasa akiachwa kwenye uhusiano "hati-hati" anaendeleza ule uhusiano mpya hivyo hatokaa bila mpenzi.

Ndio maana alikuambia kuwa yule alikuwa mpenzi wake lakini hamtaki, hakisema SINA UHUSIANO NAE....."Simataki" ilikupa matumaini na uhakika kuwa wewe ndio unatakiwa na upo peke yako(Kisaikolojia).

Wewe huku unashindwa kula wakati yeye yupo sehemu amekumbatia mwanamke mwingine na anafurahi kama hakuna Kesho!! Bibie umeangushwa, inuka jifute vumbi na uanze kusonga mbele taratibu.

Umevumilia visivyovumilika kwa Miaka mitatu na ameshindwa kukuheshimu wala kukuthamini, haitaji uwepo wako kwenye maisha yake Machafu.


Achana nae, unastahili mwanaume mwema, muaminifu,mwenye mapenzi ya kweli na mwenye kuthamini utu wa mwanamke.

Kumpenda mtu sana sio kigezo wala sababu ya kuendelea kuishi na mwanaume mjinga-mjinga hasa ikiwa anaweka Maisha yako hatarini.

Utaumia, Utajiuliza kwanini? Utalia, Utajutia muda uliopoteza, Utachukia kisha Utakubali kuwa uhusiano haukufai na utasonga mbele kirahisi bila yeye.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Wednesday

Mimi;Nakupena..Yeye;Usijali

Shikamoo dada dinah! Mimi ni mwanamke na nilikuwa ktk mahusiano for 4years but nikaachana na ex wangu sababu alikuwa ananicheat sana.

Sasa kuna mkaka ambaye nilikuwa namjua na tulikuwa tunasoma Chuo kimoja japo yeye alikuwa amenizidi na alikuwa anachukua Masters.


Alikuwa ananifatilia wakati wote huo lakini mimi sikuwahi mkubalia kwasababu nilikuwa kwenye mahusiano na yule Ex, baada ya kuachana nae tukaanza kuwasiliana serious kama mwezi mmoja hivi.


Siku moja akaniambia niende kwake, nilipofka akataka tufanye mapenzi mimi nikamwambia nahitaji kumjua zaidi na japo kucheck afya! Akataka tufanye kwa kutumia Condom but mimi nilikataa.


Sina nia mbaya na yeye ni kweli nampenda halafu dada mimi ni muaminifu sana kwenye mahusiano. Nilivyokataa ku do naye akasema sawa, tulikiss na kunishika shika.

Toka siku ile hapokei simu zangu na msg hajibu. Kuna siku nikamtext kumueleza kuwa nampenda sana akajibu in short akasema usijali!

Kiukweli naumia sana na mimi nampenda huyu kijana sasa simuelewi nimemuomba tuonane tuongee hajajibu chochote.

Dada chonde nisaidie nimekosa raha kabisa sielewi nia yake ni kunichezea au? Na mimi sio kwamba siko tayari kushiriki penzi naye but nahitaji nimjue vizuri then mengine yafuate.
Asante.


******

Dinah anasema: Marhabaa mrembo, ahsante kwa ushirikiano.


Mmeanza kuwasiliana kwa umakini kwa mwezi mmoja....unauhakika kweli unampenda huyo Mr Masters au ume-miss tu kuwa na mpenzi baada ya kuachana na Ex na huyo jamaa akawa easy target kwasababu alionyesha kukutaka?


Miaka minne ni mingi sana kuwa kwenye uhusiano wa Kimapenzi na ku-get over uhusiano wa muda mrefu hivyo huchukua Muda zaidi ya mwaka! Haya ni muda gani umepita tangu umeachana na the cheater one?


Pamoja na kuwa unasababu nzuri sana ya kukataa Ngono (hongera kwa Msimamo Mzuri) bado inaonyesha upo needy na unaharaka ya commitment kwa sababu umemwambia unampenda mapema sana, huwezi mpenda mtu ndani ya mwezi mmoja tena baada ya kutoka kwenye uhusiano wa muda mrefu.


Sio tu inauma kumwambia mtu unampenda alafu yeye anakujibu "usijali" au "ahsante" inakufanya ujihisi aibu mbele yake na pengine kujiamini kunaweza kupungua kimtindo!


Ni wazi kuwa jamaa hajaanza kujisikia "anakupenda" as in "I love you" yaani penzi halijamvaa kama unavyodhani ila anapendezwa au kuvutiwa na wewe as in "I like you a lot".


Kiswahili hakina maneno mbadala ya kuwakilisha hisia kabla, labda napendezwa nawe ilikuwa sahihi zaidi ya "nakupenda".

Tangu kaamua kukuchunia basi ni vema na wewe kuuchuna na kuangalia ustaarabu mwingine.

Kuwa cheated on alafu kujibiwa hivyo hakika inaweza kukukatisha tamaa kabisa na suala zima la Wanaume au unaweza kuamua "liwalo na liwe" kwamba unakubali mwanume yeyote atakaejitokeza ili kujihisi vema moyoni na kujirudishia kujiamini.....(Utajiumiza zaidi).


Unahitaji muda kupumzika kabla ya kuingia tena kwenye mahusiano ya Kimapenzi. Achana na huyo Mr masters.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Tuesday

Mume kapitiliza kwa Kudeka!

Natumaini wewe ni mzima wa afya na family yako pia. Nakushukuru kwa kazi nzuri unayoifanya ya kutuelimisha kwani tunapata vitu vingi sana vya kutujenga kutoka kwako. Ubarikiwe sana.
      


Mimi ni mwanamke wa miaka 25 sasa, Ni mara yangu ya pili kuomba ushauri kwako mara ya kwanza ulinipa ushauri mzuri sana na umenijenga vilivyo na ndio maana nimeamua nirudi tena kwa jambo jingine.


Nimeolewa na mwisho wa mwaka nitatimiza mwaka mmoja wa Ndoa. Mume wangu amenizidi sana kiumri kwani ana miaka 44.

Kutokana na umri wake kunipita watu wanaona nimeolewa na mwanaume aliyenizidi sana wananisema kichinichini nami nazipata habari zao.

Mume wangu mzuri ana mapenzi kwangu na ananiheshimu sana mimi pamoja na familia yangu. Ananipa matunzo vizuri  kwani sijafanikiwa kupata kazi bado na hiyo ni kutokana na kuishi mbali mimi na yeye kwa sababu nitakozokueleza.

Mume wangu na familia yake wanakaa nje ya nchi(Marekani)  ila ni Watanzania waliondoka kitambo kidogo baada ya baba yake kupata uamisho wa kikazi. Aliondoka akiwa mdogo hivyo ana miaka zaidi ya thelathini anaishi huko hivyo ana tabia za kizungu na mambo yake kama wazungu.

Alikuja Tanzania tukakutana tukapendana tukafikia uamuzi wa kuoana. Wazazi wake walikuja ikawa harusi nzuri kweli. Ila mimi bado nipo Tanzania kaniacha huku tukishughulikia mambo ya Visa, ikitick niende.


Anajitahidi kuja mara tatu kwa mwaka  akipata likizo tu anakuja kwani anafanya kazi huko. Mume wangu bado anakaa na wazazi wake huko.

Nawapenda sana wakwe zangu ni watu wazuri, ila kuna tabia siipendi kutoka kwa mume wangu ni mtu flani anapenda kuwataja taja Baba na Mama yake muda mwingi yaani anawataja mno kama mtoto mdogo.

Haiwezi kupita siku bila kuwataja baba yake na mama yake hadi kwenye chakula anacompare akimaanisha cha mama yake kitamu kuliko tunachopika sisi.
      

Muda mwingine tupo na watu tunapiga story yaani lazima atafute sehemu achomekee kitu kuhusu baba na mama yake kama mtoto mdogo na huku kiumri ni mkubwa. Sasa sijui ni sababu ya kukaa na wazazi wake mpaka umri huu.

Nawapenda sana wazazi wake lakini kwa hili sipendi, naona anazidi mpaka sometimes naona kama angeendelea tu kukaa na wazazi wake maana kukaa na mke hakumfai.


Yaani hata akija Tanzania akiongea na wazazi wake kwa simu akimaliza atasema nimewamiss sana wazazi wangu mpaka namuhesabiaga siku ziishe aondoke aende kwa wazazi wake mie nibaki zangu peke yangu.


Unakuta roho hainiumi yeye akiondoka maana naona anapapenda huko zaidi. Kuna muda natamani nisipate Visa mapema maana nikienda huko nitajisikia vibaya zaidi.


Naomba ushauri wako dada yangu kama ni kawaida na nifanyaje ili nizoee hii hali maana naona kama naanza kumchukia na kumuona kama anadeka yaani upendo unaisha kabisa.


Na kumwambia siwezi maana sitaki kuingilia chochote na familia yake. Ahsante sana.
    


**********


Dinah anasema: Mie na familia yangu afya tele, mbio-mbio tu. Ahasnte kwa kujali na shukurani kwa ushirikiano.


Unajua kila Binadamu anamapungufu yake (kasoro), kuna mapungufu ya kimwili (nje au ndani), kitabia, n.k.....Baadhi ya mapungufu huonekana na mengine hayaonekani(utayaona ukianza kuishi na mhusika).

Unapompenda mtu kwa penzi la kweli, mapungufu hayo huwa hayaonekani.....yapo lakini penzi linayaziba hivyo unamchukulia Mpenzi wako kama alivyo.

Unapoyaona mapungufu hayo na ukahisi hayakupendezi na ukahisi unaweza kumsaidia mwenza wako kuacha au "kupona" basi unajitahidi na kujitolea kumsaidia.

Inawezekana Mumeo alidekezwa sana na wazazi wake na hivyo kumfanya ashindwe kujiamini kufanya mambo peke yake kama Mwanaume na hivyo wazazi wakawa tegemezi kuu kwake.

Pia inategemea na alivyokua kimazingira, ujue mtoto kuhamia na kuishi Nchi za Magharibi unakumbana na mengi Hasi ambayo kwa kawaida watu waishio huko huwa hawayasemi na badala yake wanasema yale Chanya tu.

Sasa huwezijua Mumeo alipitia nini Miaka yote 30na alipokuwa huko hali iliyomfanya ahisi kuwa Baba na Mama yake ndio kila kitu kwake(zaidi ya Wazazi).

Kingine ni kuwa Maisha ya Kimagharibi wakati mwingine yanaweza kuwa ni ya Upweke sana.....hasa kama umetoka kuishi "kiafrika" halafu ukaenda mahali ambapo kila mtu anajifungia kwake (unaita kizungu, mie naita Kimagharibi), utajikuta Mnyonge na watu pekee ni wazazi wako na ndugu zako.

Nadhani hata wazazi wake wanatamani sana Mtoto wao aanze "kujitegemea" wakihofia siku wakifa basi Kijana wao anaweza kuwa Mwehu au hata kujiua na yeye.

Ni mumeo na mnapendana, sasa penye hasi weka Chanya na ujichukulie kuwa wewe ndio muongozo wake, chukulia wewe ndio utamsaidia aanze kujitegemea "kiakili" na "kisosho" (baadhi ya wanaume huchelewa ku-mature).

Anza kumuandaa taratibu kuwa ungependa kuishi mbali na wazazi ila tafuta namna ya kufikisha ujumbe wako ili asijisikie vibaya(usiumize hisia zake).

Unapozungumza nae kuhusu maisha yenu pamoja huko US, jaribu kumuuliza mtakaa wapi kama mke na Mume....akisema kwetu as in kwa Baba na Mama, uliza mtakaa hapo kwa muda gani kabla hamjatafuta kwenu?.

Kumbuka utafika US hautokuwa na Kazi hivyo itakubidi utafute kazi (kama una ujuzi tayari) ama urudi Shule kuongeza/kupata Ujuzi ili uweze kuajiriwa kirahisi huko US.....vinginevyo itakuwa rahisi kwenu kama Pea kujibanza kwao mpaka mtakapojiweka sawa kiuchumi.

Kukutumia senti za matumizi Tz inaweza kukufanya udhani jamaa anamahela....Tsh haina thamani hivyo Dola inalipa (ukibadilisha) lakini utakapokuwa huko US hali inaweza kubadilika kiasi, kwamba matumizi yatakuwa ghali....usilishau hili!


Akiuliza kwanini unahofia kuishi na wazazi wake nyumba Moja....Weka wazi kuwa haupo comfortable kuishi na Wakwe nyumba moja....weka sababu zako za ki-romantic zaidi na kwamba hautokuwa huru ku-romantic-a na yeye (Mumeo).


Wanaume wote wanapenda kufananisha/linganisha Wake zao na Mama zao kwenye Mapishi!

Ni wanawake waliowalea na kuwapikia maisha yao yote ya mwanzo hivyo huwachukua Muda mpaka waje kuzoea mapishi ya watu wengine.

Muhimu ni wewe kuongeza mautundu kwenye kupika na ataanza kusahau ya Mama yake na kusifia ya mkewe kwa Wifi zako (watanuna hao) na marafiki.

Nadhani maelezo haya yatasaidia kukupa mwanga na kutuliza hofu yako.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Monday

Nimpendae anamtoto (Ready made Family)

Habari dada, pole na kazi na asante kwa msaada wa kimawazo ambao
umekua ukitusaidi kuhusiana na mahusiano ya kimahaba.

Nimekuandikia
ili unishauri juu ya tatizo langu kama ifuatavyo. Baada ya kumaliza masomo nilipata Kazi hivyo nikaona ni vyema nitafute mwenzangu.

Nilikumbuka enzi zile nikiwa shule kuna mdada nilimwacha kama madarasa mawili nyuma kwa sasa yupo Chuo, nilimkazia fikra zangu zote
nilikumbuka jinsi alivyokuaga mwema mtulivu.


Tulikua marafiki wa kawaida nilimheshimu sana nikaona she is the best. Nilitafuta mawasiliano yake nikapata tukawa tunaongea na kuchat sana kupitia Simu.


Nilimweleza hisia zangu akakubali akasema hata yeye alikua
akinipenda sana. Tuliendelea kuchat na kupeana ahadi nyingi.


Akasema wakifunga Chuo wakati anaelekea nyumbani atapitia kwangu kuna jambo la kuzunguma na ni vizuri tuonane.

Walipofunga chuo akaja, nilienda kumpokea kwa furaha coz ni muda wa kama 5yrs hutujaonana. Alizidi kuwa mrembo ila mkononi alikua amepakata
katoto kama kamiezi mitano doh!

Tulipo pata nafasi ya kuzungumza alisema tatizo ndio hilo ana mtoto
amezaa na Mume wa mtu na huyo jamaa ni baba wa watoto watatu na walikutana huko Chuoni.


Kwa mujibu wa maelezo yake Jamaa anatoa ushirikiano mzuri tu katika
malezi ya mtoto, matumizi na wanawasiliana.

Nikamuuliza ilikuaje mpaka mimba inamaana walikua hawatumii kinga! akadai ni utoto alikua hajui mambo ya uzazi.

Kweli nampenda natamani tuoane ila hili linakua zito, ahadi na viapo vyangu vinanisuta kumwacha, nifanyeje?

Kinacho niuma zaidi siwezi
kuzuia mawasiliano yao coz ni baba wa mtoto japo anasema hana uhusiano
naye tena. Kiukweli najenga picha mbaya kichwani akiwa huko Chuoni sijui
kinachoendelea.


Naomba msaada wa kimawazo nifanyeje. ASANTE!


************


Dinah anasema: Habari ni njema kabisa, ahsante na shukurani kwa ushirikiano.


Anasingizia utoto, angekuwa mtoto asingechanua miguu kwa Mume wa mtu na Baba wa watoto 3, angelala na kijana mwenye umri unaofanana na wake. Alijua alichokuwa akikifanya. Tangu hukuwa nae kipindi hicho, achana na hilo!

Natambua itakuwa ngumu sana kwako kuwa na amani Moyoni kila wakati Mwanamama huyo anapokuwa Chuoni na "baba mtoto" wake. Watu waliokwisha onana wakiwa Uchi (Exes) achilia mbali ku-share mtoto ni ngumu kuaminika wakiwa peke yao.


Mbaya zaidi huna nguvu kwenye maisha ya huyo Mdada kwasababu uhusiano wenu sio rasmi hivyo huwezi kumshauri/shawishi ahame Chuo ili awe mbali na Baba mtoto wake wala ku-demand mipaka kati yake na Ex wake.


Kama kweli unampenda na unataka ku-share maisha yako nae + mwanae basi anza kuweka "msingi" serious wa uhusiano wenu sasa huku ukiungulia maumivu ya kutomuamini anapokuwa na Ex wake na mtoto wao mbali ya macho yako.


Uhusiano ukikomaa angalau utakuwa na sauti au nguvu ya kumuwekea Mipaka mpenzi wako kuhusu Mawasiliano na Ex wake.


Kwasasa huyo Mdada anasoma which means hana kipato na hivyo hawezi kumtunza mtoto hali inayopelekea yeye kumtegemea huyo Mume wa mtu.

Usijemharibia "utaratibu" wa kujikimu alafu ukaja muacha huko baadae ateseke na mwanae akiwa mwanafunzi (hana kipato).

Kwenye Matunzo ya mtoto kunaweza kukatwa ikiwa wewe utakubali kumhudumia mtoto kipindi ambacho mama yake hana kazi....utakuwa umejipatia "ready made family"


Kwa upande mwingine itakuwa nzuri kipindi hiki mtoto bado mdogo sana so utakuwa kama umemuasili mwanae na hivyo kum-cut off baba yake (akikua mtamwambia ukweli).

Ila kumbuka kuwa kufanya uhusiano na mwanamke mwenye mtoto na mwenye connection ya karibu na Ex wake kama huyo wako ni ngumu sana, maisha yako yote yatakuwa ya wasiwasi na hofu kila wakati Baba mtoto anapotaka kumuona mwanae au mtoto (akikua) anataka kumuona Baba yake.

Weka "nampenda sana" na "viapo na ahadi zako kukusuta" pembeni kwanza halafu kaa chini na jiulize tena, katika umri wako ambao ni chini ya miaka 35, upo tayari kweli kulea mtoto wa mwanaume mwenzio?


Je, kweli gharama hizo za maisha (mtoto ni gharama) ndizo ulizokuwa ukizihitaji mara tu baada ya kuanza kazi au ni muhimu kujipa Muda, kujijenga alafu ndio Utafute Mwenza?


Fanya uamuzi kulingana na majibu yako.


Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Tuesday

Pale Mume anapoweka Password kwenye Simu yake....

Hi Dinah,
Kwanza kabisa nikupongeze kwa kazi nzuri. Mie binafsi blog yako imenibamba kweli na imenitowa kimasomaso kwa mambo mengi.


Nimepata elimu na nimnefurahia sana.
Mpendwa naomba kuuliza! Mie ni mwanamke mwenye Ndoa ya miaka Sita. Tulipo oana na mume wangu mwaka wa kwanza wa Ndoa yetu tulikuwa tunakaa Mikoa mbalimbali, yeye akikaa Lindi na mie Dar kwa sababu za kikazi.

Mungu alijalia mwaka wa pili akapata kazi Dar akahamia Dar, tuliishi vizuri na sikuwa na wasiwasi naye maanake niliona kama mwanzo wa maisha mapya kwa pamoja tukiwa chini ya dali moja.

Baada ya miezi kama Sita hivi mume wangu alibadilika na style yake ya maisha ikabadilika ikiwa hata marafiki. Hapo ndipo nilipo anza kutafuta kushika simu yake ili kujua kinachoendelea.

Duh amakweli usilolijua nikama usiku wa giza, nilipoanza kushika simu yake nilikuta ni kiwembe cha kutupa! Alikuwa na mademu wasiopungua 10 wengine amewasave kwa majina ya magari, hotels na kwa majina ya marafiki zake wa kiume.


Dinah niliunia sana nikakaa chini nikaongea naye nikamwambia madhara ya Umalaya ni nini? athali zake kwa watoto wetu akasema atajirekebisha.

Nikampatia muda akabadilisha namba kwa malengo ya kupoteza mawasiliano na wao, ila baada ya muda mfupi hali ile ilijirudia.

Kweli nilipitia kipindi kigumu sana kwa miaka yote hiyo. Mwaka jana nikamwambia kama simfai mie naondika na watoto wetu 2 ili yeye afaidi maisha anayoyataka .

Akapiga magoti akalia akaomba msamaha akasema ni company mbaya za shetani akaahidi ku cut-off marafiki na kubadilika kwa mambo yote niliyo mweleza.

Nikampatia nafasi aniambie kama kuna mapungufu kwangu aniambie nijirekebishe akasema tatizo ni yeye na nimpe muda.


Hivi sasa simu zake zote ameweka password, Airtel na Tigo na ameongeza line nyingine ya Airtel sasa dinah sina amani na simuamini kwani amekosa uaminifu kwa muda mlefu.


Nashindwa elewa kama ana-improve makosa yake kwa sababu ya password kwenye simu na naomba nielimishwe kuhusu matumizi ya simu ya mwenza ni mwiko kushika?


Au anafanya hivyo ili nisione kinachoendelea? Naipenda Ndoa yangu na na muomba sana Mungu anisaidie. Sipendi Talaka na kuachana imani yangu ya Dini hainiruhusu.

Nahitaji elimu jinsi ya ku- overcome haya maumivu na stress.
Natanguliza shukrani.

************


Dinah anasema: Ahsante na shukurani kwa Ushirikiano.


Sometimes watu wanamsingizia Shetani! Hapo Shetani hausiki kabisa ni yeye mwenyewe amejiachia kwa sababu ambazo anazijua mwenyewe.


Sasa hapa mie ndio huwa napata Hasira!!! Mumeo ni Malaya na umethibitisha lakini hutaki kuachana nae bali unataka to overcome Maumivu na stress za Umalaya wake. MWANAMKE mwenzangu!!!! Kweli?!! Kivipi(maana mie sijui)?


Kama Dini yako hairuhusu basi Sheria inaruhusu mkimama....Miaka Sita ya Kunyanyaswa Kihisia, Kimapenzi, Kimwili na Kisaikolojia juu ya Umalaya wa Mumeo kwenye ndoa haijakutosha tu....usije zeeka au kufa bila kujua nini raha ya Maisha.


Huwezi ku-overcome Umalaya wa mtu kwa kuendelea kuishi nae na kumuacha aendeleze Umalaya wake na kum-treat as if wewe ndio mwenye Makosa!


Huyo ni mumeo, sio boyfriend....baada ya kugundua Usaliti wake ungemuweka Chini ukiwa firm (sio unalia-lia), ungempa msimamo wako kwenye Ndoa yenu na unge-Demand kupima afya zenu na mabadiliko ya kudumu haraka sana or else!! Hakuna kumpa Muda.


Kama kweli anakupenda na anaitaka Ndoa basi angekuomba msamaha na angebadilisha tabia yake, SIO kubadilisha namba ya Simu na kuweka password.

Huyo mumeo hafai, hakuheshimu, hakuthamini na wala hakupendi.....yupo na wewe possibly kwasababu ya watoto au mambo mengine lakini sio Mapenzi.


Watu wanakaa kwenye Ndoa kwa sababu za Kikazi (status), wengine kwasaabu ya Miradi n.k.


Sasa usijedhania unapendwa sana na mumeo pale anaposhupaa na kulia kabisa usimuache....usikute analilia "mkate" kwamba Kazi yake inamlazimisha awe na Mke (kazi nyingi za serikalini).


Kuhusu Mumeo kuwa na line nyingi za Simu na kuweka "kiingilio" cha siri ni wazi kuwa anakuficha Mengi ambayo anajua ukiyajua basi utamkimbia.


Unapaswa kuhoji kwanini hasa anakuwa na line nyingi za Simu na kwanini anaweka "neno la siri"?....ni mumeo na unahaki ya kujua kila akifanyacho....hii ni 2014 sio 1994!!


Wengine huweka "neno la Siri" ili simu zao zisitumiwe na watu wengine hasa Makazini, wanaweza kuiba details za kibiashara au hata Picha binafsi na kuzisambaza Mitandaoni.


Hii isikupe matumaini, tayari unajua Mumeo ni Mshenzi hivyo uaminifu haupo so ni vema kupata ukweli kutoka kwake.

Kwa kawaida hakuna mipaka kati ya Mume na Mke linapokuja suala la simu ya Mkononi, kama mna-share kila kitu kama familia kwanini simu ya Mkononi iwe tofauti?!!

Tatizo lako ni kwamba humuamini tena Mumeo na kama hakuna Uaminifu kwenye Ndoa ni wazi hakutakuwa na Amani.

Mumeo anahitaji kubadilika na kukuhakikishia kuwa kabadilika kwa vitendo ili akusaidie kurudisha hali ya kumuamini tena.

Lakini Mumeo hawezi kubadilika ikiwa unam-treat unavyom-treat sasa(kutokana na maelezo yako).....anafanya atakavyo kisha anaomba msamaha....anapewa muda....anarudia tena mzunguuko uleule.

Nasikitika kuwa sina mbinu ya kukushauri ili ku-overcome Umalaya ya mumeo ambao ni very active.....kwamba sio alifanya miaka 2 iliyopita bali nafanya sasa hivi.
Labda wasomaji wasaidie.

Kila la kheri.

Mapendo tele kwako...

Pages