Thursday

Mume wangu hataki tuzae-Ushauri!

"Habari dada dinah na wasomaji wengine, naomba msaada wenu wa ushauri na samahani kwa maelezo marefu. Mimi nina umri wa miaka 28 na mume wangu 37. Tunaishi Europe. Niko kwenye ndoa miaka 2.


Tulikubaliana na mume wangu tusizae kwa muda fulani kwasababu ya gharama tulizopata wakati wa harusi na pia ili tujenge. Muda wa kutozaa unaisha mwezi wa 12 hivyo ikifika muda huo natakiwa kutiana kwa nguvu zote ili nimimbike.


Kuna siku nilimkumbushia mume wangu kuhusu muda wa kupata mimba unakaribia hivyo tuanze kujiandaa, akawa mkali na kuniambia nisahau kitu kuzaa kwasasa kwasababu ana majukumu mengine ya kuwasomesha wadogo zake wawili ambao ni mtoto wa kaka yake na masikini mmoja anamsaidia na mtoto wake alimzaa na mtu mwingine alipokuwa chuoni.


Mimi nikamwambia anaweza kupunguza majuku kwa kuwaachia ndugu zake mdogo wao mmoja na yeye akabaki na mdogo mmoja kwasababu kwao wako 9 na huyo mtoto wa kaka yake amuachie kaka yake amsomeshe mwanae ili na sisi tuzae wa kwetu na tujenge na kufanya mipango mingine akanambia hatofanya hivyo kama siwezi kusubiri majukumu yaishe nitafute mwanaume asiye na majukumu nizae nae.


Ndugu zake wengine wanauwezo wa kawaida mbao yeye ameshawasaidia kwani alishawapa mtaji wabiashara, na kuwajengea nyumba ya familia na pia mambo mengi anawasaidia. Jamani nisaidieni sielewi nifanye nini. Na nimeshaambiwa nitafute mwanaume mwingine, kuzaa nataka na ndoa yangu sitaki ivunjike"

Jawabu:Asante sana kwa barua pepe yako, nadhani mumeo alijibu kwa hasira kwa kufikiria kuwa kwa vile tu amekuoa unataka asahau familia yake (kumbuka umeolewa miaka 2 tu) hivyo majukumu yake aliyonayo aliyaanza kabla yako na hivyo hana buni kuyamaliza. Yeye kama mwanaume tena wa Kibongo haitaji mwanake kumuambia nini cha kufanya hasa linapokuja suala la ndugu zake. Hivyo basi tamko lake la kutafuta mume mwingine usilitilie maanani.


Katika mambo yote kwenye uhusiano wowote wa kimapenzi hata siku moja usiingilie mambo ya familia ya mwenzio, hata kama atakuomba ushauri hakikisha unampa ushauri utakaomsaidia na kwamwe usiponde ndugu zake hata kama wamemuumiza mumeo na badala yake msikilize, mpe matumaini na kumtuliza hata siku moja usijarubu kujiingiza kwenye masuala ambayo wewe hayakuhusu......hujui makubaliano yako kama Familia.


Badala ya kumuambia mumeo apunguze majukumu ulitakiwa kumwambia kuwa "kipato changu" kinatosha kusaidia majukumu mengine yakiongezeka moyoni ukimaanisha kuwa unataka mzae, lakini kama kila kitu ni juu yake inamuuwia vigumu hasa ukizingatia kulea mtoto Ulaya sio lele mama kwa maana ya kiuchumi.

Natambua unavyojisikia na hofu yako ya kuchelewa kuzaa, wewe bado kijana ungekuwa na umri wa miaka 33 na ukawa na hofu hiyo ya kuzaa ningekuelewa, lakini kumbuka unaweza kufurahia maisha yenu ya ndoa bila kuwa na mtoto mpaka pale mtakapokuwa tayari na kuwa na uhakika wa kufanya hivyo.


Najua wanawake wa Kibongo kuzaa wanaona mwisho wa matatizo au njia pekee ya kulinda ndoa kama sio kum-keep mwanaume, yaani wewe kuwa mwanamke basi ni lazima uzae lakini wanasahau kuwa (1) Ni majaaliwa na (2) Ni chaguo la mtu. Kuzaa sio lazima na haijalishi una umri gani kama Mungu alitaka siku moja uwe na familia basi itakuwa hivyo.


Hivyo mdada tulizana, acha kujipa mawazo bila sababu ya msingi, furahia maish ayako ya ndoa, Mpe ushirikiano mumeo ktk kukabiliana na Majukumu uliyomkuta nao ili kumpunguzia stress, fanya bidii kwenye shughuli zako kiuchumi ili kukusanya senti kwa ajili ya mtoto atakae zaliwa, pale mtakapo elewana kufanya hivyo.

Ukimuonyesha mapenzi, ukiwa mwenye furaha, ukijitahidi kumuondolea stress na kushirikiana nae ktk kila jambo bilakujiingiza sana kwenye masuala ya familia yake, hakika mumeo atapata ujumbe na kama ni mtoto ndio unataka basi atakupatia......tumia uanamke wako kupata utakacho.


Pssst! Usikute hana uwezo wa kuzaa ila anashindwa kukuambia, mana'ke wanaume wakikaribia miaka 40 huwa na haraka sana ya kuzaa no matter what kama unahisi the same basi baada ya mwezi wa 12 tumia ila mbinu ya "kumtegeshea" siku za hatari na usiposhika mimba utajua ukweli na ukishika basi utakuwa umepata ulichokitaka.

Ikiwa unatumia aina yeyote ya dawa za kuzuia mimba basi ni wakati wa kuacha na kutumia njia asilia au Condoms ili kujiweka sawa kushika mimba hapo baadae.

Kila la kheri.

Monday

Nikirudi Bongo ndio itakuwa basi?-Ushauri

"Dada dinah pole na kazi, naomba niingie moja kwa moja na kile kilichi nileta hapa.
Dinah nina mpenzi ambaye tumeahidiana kuoana ingawa wote tuko shule mimi niko mwaka wa mwisho yeye bado kama miaka miwili hivi, na wakati wote huo tuko karibu sana kama mke na mume na tuko ughaibuni.


Tatizo ni kwamba tumekua tukigombana mara kwa mara na tunapatana wenyewe bila kumshilikisha mtu na kibaya zaidi huyu mwenzangu hua hajui kusema samahani hata kama anajua amekukosea, kiasi kwamba mtu unapata hasira.Mtu amekukosea halafu haombi msamahaa.


Siku zingine hua tunapigana kabisa kutokana kwamba yeye hataki kujishusha na mimi kama mwanaume sipendi kudharaulika mwisho wa siku tunaanza kupigana, Mbali na hayo inaonyesha kila mtu anampenda mwenzie kiasi kwamba hayuko tayari kumuacha.


Na kingine ni kwamba huyu mpenzi wangu ameumbika kidogo mungu kamjaalia.Na kipindi chote hiki nilichokua nae kweli tumefurahia mapenzi ingawa kuna ugomvi wa hapa na pale. Wanaume wengi wamemtaka lakini wote huishia kugonga patupu na wengi wanasubiri mimi niondoke baada ya kumaliza shule ndo wamtake kwani wanamwambia laivu ku wanasubiri niondoke.


Hapo ndio ninapoingiwa na wasiwasi je nikiondoka ataweza kuvumilia kweli?au ndo ahadi yetu itakua imekufa? pamoja na hayo namwamini sana lakini najua kuna kutereza, na mimi sipendi kuchangia hasa ukizingatia tumekuwa pamoja kwa muda wa miaka miwili na miezi sita sasa na baadhi ya ndugu wanajua uhusiano wetu.


Kipindi chote hicho wote tumekua sio watu wa kujirusha sana na wala hatutumii any alchohol. JE DADA DINAH NIWE NA MATUMAINI AU NDIO BAI BAI MAANA NATAKA KUJUA ILI NISIPOTEZE MUDA.

Naomba ushauri dinah na wadau wengine wa blog hii
thanx".

Jawabu:Asante sana kwa pole zako kwani zimefika wakati muafanya kwa vilemajukumu yameniandama sana tangu mwaka huu uanze lakini najaribu kujigawa kimtindo.

Sasa jamani mapenzi gani hayo ya kupigana magumi kwa vile mmoja hataki kudharauliwa na mwingine hataki kuwa chini? Hata siku moja haiwezekani mtu ajiweke chini kwani akifanya hivyo utamdharau kama ambavyo wewe hutaki. Kwanini wewe usiwe mstaarabu ukakaa kimya wakati yeye analalamika na akimaliza mpe jibu zuri, kwa upole na upendo badala ya kuinua mkono na kumdunda mwenzio ambae ni mwanake?.....tuliache hilo.


Suala la wewe kutaka kujua kama ni kweheri au usubiri unapaswa kumuuliza yeye mpenzi wako. Zungumzzeni kuhusiana na maisha yenu ya baadae na mipango yenu kama wapenzi. Weka wazi hofu na wasiwasi ulionao juu yake pale utakapokuwa unarudi Nyumbani na kumuacha yeye huko.

Mawasiliano ndio njia pekee ya kujua umesimama wai kwenye uhusiano wenu, mazungumzo yenu yakina yatakusaidia kufanya maamuzi ya busara iwe ni kusubiri au kuendelea namaisha yako kivyako.

Kuwa na mpenzi au kuwa kwenye uhusiano hakuzuii watu wengine kukutamani, kama mzuri anavutia na amejaaliwa umbile zuri kwanini asitamaniwe?!! Kutamaniwa haina maana kuwa mpenzi wako atatereza na kila atakae mtamani.....jivunie uzuri wa mpenzi wako ambao unavutia watu wengine.
Kila la kheri!

Hivi tutafunga ndoa au? Mawasiliano Sufuri...

"Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 25 ninamchumba ambaye tuna miaka 2 katika uhusiano wetu, anasema kuwa anatarajia kunioa ila sina uhakika kuwa ni kweli. Mimi nipo Arusha na yeye yupo Dar, ila sina uhakika maana naona siku hizi kapunguza mawasiliano na mimi sio kama mwanzo. Naombeni ushauri wenu kama kweli ananipenda au ananidanganya tu.
Ester."


Jawabu: Ester, asante sana kwa ushirikiano wako. Mchumba wako ndio amesema kuwa anatarajia kukuoa sio kwamba mmepanga (yeye na wewe) kuoana hivyo kufanya nyote wawili kutarajia kufunga ndoa na kuishi pamoja mpaka kifo kiwatenganishe?

Natambua kuwa ni kawaida au asili kwa mwanamke kusubiri mwanaume atangaze ndoa au atake kuoa lakini ktk hali halisi ndoa ni makubaliano ya watu wawili wanaopendana na wenye nia moja ya kwenda kuishi maisha yao pamoja, japokuwa kwenye baadhi ya Jamii wazazi wako ndio wanakubaliana na sio ninyi mpendanao.

Kwenye hili, naona mambo mawili ambayo yanaweza kusababisha hofu yako juu ya u-serious wa mpenzi wako kwako. Mosi, huenda yeye haamini kama kweli unataka kufunga nae ndoa kwani maelezo yako hayajaonyesha wewe kutaka au kutaraji akufanya hivyo bali yeye ndio anatarajia kukuoa.

Pili, umbali kati yenu na gharama za maisha hasa linapokuja suala la mawasiliano inazweza kuwa sababu kubwa ya ninyi kutokuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kama ilivyokuwa huko mwanzo, pia kunauwezekano mkubwa kuwa unasubiri yeye ndio awasiliane na wewe na sio kuwa mnawasiliana kwa maana ya wewe una-check nae na yeye anafanya hivyo. Inaonyesha yeye ndio mtendaji mkuu kwenye uhusiano wenu hali inayoweza kusababisha uchovu na yeye kuhisi kuwa anafanya too much na wewe kazi yako ni kusubiri tu.

Uhusiano wowote wa kimapenzi unajengwa/boreshwa kwa kuzingatia nguzo kuu tano na moja kati ya hizo ni kushirikiana, ninaposema kushirikiana ninamaanisha kiuchumi, kihisia, kimwili, kimawazo na maamuzi. Nasikitikakusema kuwa kutokana na maelezo yako hakuna dalili ya ushirikiano kwenye uhusiano wenu na vile vile mawasiliano sio mazuri sana kutokana na umbali kati yenu.

Kitu muhimu cha kufanya ili ujue kuwa jamaa hakudangaji juu ya suala la kufunga ndoa na wewe, ni wewe kujitahidi na make an effort kwenye uhusiano wenu hasa linapokuja suala la mawasiliano, zungumza nae kuhusiana na ahadi yake na sasa ifanye iwe ahadi yenu kwamba mnaahidiana kufunga ndoa na hakikisha unamshawishi afanye kweli kwa kuchumbia kwenu na sio kuishia kusema tu "nitakuoa", "lazima nikuoe", "natarajiakukuoa" au "wewe mchumba wangu".

Suala la yeye kukupenda au kukudanganya nadhani itakuwa ngumu kwangu mimi na wasomaji wangu kujua kwani hujatueleza kwa undani na kwa uwazi zaidi, wewe Ester ndio mtu pekee unaeweza kujua kama Mchumba wako anakupenda kwa kuzisoma hisia zake, ukaribu wake kwako, anavyoku-treat n.k.

Tafadhali zingatia hayo machache niliyokueleza na mengine kutoka kwa wachangiaji wangu na ujaribu kuyafanyia kazi ili kufanikisha kile ukitakacho kutoka kwenye uhusiano wako. Kwa case yako ni ndoa basi hakikisha unafanyia kazi uhusiano wako ili kupata hiyo ndoa....kwa mbinu zaidi kama utahitaji basi unaweza kurudi tena mahali hapa.

Kila la kheri!

Sunday

Wifi anachukua nafasi yangu, nifanyeje?-Ushauri

"Nimegundua kuwa watu wanafanikiwa kuokoa mahusiano na ndoa zao kupitia blogu hii na mimi leo nimeona nichangie tatizo langu ili kupata ushauri wa watu wengine na zaidi kutoka kwako Dada Dinah.

Mimi ni mdada mtu mzima tu nimeolewa miaka si chini ya mitano, nina watoto wawili. Nimekuwa nikishindana na wifi yangu ambae ni dada wa damu wa mume wangu, ushindani wetu ni kama mtu na mke mwenzie lakini si hivyo.

Kabla sijaolewa na huyu mwanaume tulikuwa kwenye uhusiano wa mbali kwani mimi nilikuwa nasoma Ireland na yeye alikuwa Tanzania. Kipindi chote hicho hakukuwa na matatizo yeyote kati yangu na dada yake.


Baada ya kumaliza masomo nilihamia England kufanya kazi ambako ndiko tunaishi mpaka sasa. Ndoa yetu ilifungiwa Tanzania na Mume wangu akanifuata huku na baada ya muda tukasaidiana na kumleta dada yake ambaye ndio wifi yangu huyu mwenye vituko kila kukicha ambavyo vinahatarisha ndoa yangu.


Imefikia hatua wifi yangu kuchagua nini kifanyike ndani ya nyumba yangu, aina gani ya vifaa vinunuliwe ikiwa tunafanya marekebisho hapa ndani, wapi tuende au tusiende, tukamtembele nani nalini na kinachonikasirisha zaidi ni kaka mtu kumsikiliza dadake na sio mimi mkewe.


Ikitokea mimi na mume wangu tumejadili jambo la kufanya kwa ajili ya familia yetu ndogo mume wangu anachukua simu na kumwambie kila kitu mdogo wake na kitakachosemwa na mdogo wake basi ndio kitakachofanywa na sio mimi hata kama sehemu ya jambo hilo pesa zangu zinahusika. Yaani imekuwa kama akili ya mume wangu haifanyi kazi basi anatumia ya dada yake kufanya maamuzi.


Kitu kingine kinachoniumiza roho na kunipa donge ni pale ninapotoka kazini jioni au siku za mwisho wa wiki wote tuko nyumbani, badala mume wangu atumie muda huo na mimi yeye atakuwa kwenye simu na dada yake wakiongea maongezi yasiyoisha tena kwa kilugha chao na kucheka.


Nimevumilia sana na nimefanya vikao na ndugu wa pande zote mbili na hata kuzungumza na mume wangu lakini hakuna mabadiliko yeyote, nimekuwa mkiwa ndani ya ndoa yangu na sijui nini cha kufanya, japokuwa nampenda mume wangu lakini kama suluhisho ni kutoka kwenye hii ndoa basi nitatoka ili kutafuta amani na furaha kwingine lakini sio ndani ya ndoa hii.


Wifi yangu huyu ni mkubwa zaidi ya mume wangu, ameolewa na anawatoto kadhaa wote wako Mkoani Kagera Tanzania.
Naombeni ushauri ndugu zangu"

Jawabu:Mmh Dada tatizo unalokabiliana nalo ni zito sana kwa mwanamke yeyote yule ndani ya ndoa. Kwanza kabisa nakupa pongezi kwa kuwa mvumilivu na kwa ushirikiano wa kuchangia tatizo lako mahali hapa.


Nisingependa kuingia ndani sana lakini nashindwa kujizuia kupata hisia kuwa Mumeo na Dada'ke hawajiamini kwa vile umewasaidia kwa namna fulani kujikomboa kimaisha......ndio Ulaya sio mwisho wa matatizo lakini ukweli utabaki pale pale kuwa, kama ukifanikiwa kupata kazi you better off huko kuliko Bongo. Sasa nahisi hawa wanafamilia hawaamini kuwa wewe mwaamke ndio sababu ya wao kuwa huko na hilo linafanya kupoteza ile hali ya kujiamini.


Natambua sio vema kuzungumzia Makabila lakini ni wazi kuwa kuna Makabila mengine hapa Tanzania wanajali sana kuwa juu kwa kila kitu, sasa ikitokea wanakutana na mtu amabe yuko juu kabla yao inakuwa taabu. Ninaamini kabisa kuwa Mumeo hajiamini mbele yako kwa vile inaonyesha umesoma na una kazi nzuri kulingana na Elimu yako, hili ni gumu sana kwa mwanaume yeyote kuishi nalo achilia ukabila wake.


Hili linalotokea kwenye uhusiano wako huenda ni matokeo ya u-bully wa dada mtu kwa mdogo wake ambae ndio mume (lazima kutakuwa na walakini kwenye udada-kaka wao) pia inawezekana ni mambo ya "Ego" tu, Sasa kwa vile mumeo ni mdogo (kutoka na maelezo yako) inawezekana huwa anasikitika au kulalamika kwa dada yake kutokana na kutojiamini kwake, Mf-Unafanya vitu vikubwa ambavyo ktk hali halisi yeye kama mwanaume anadhani ni jukumu lake n.k


Umesema (kwenye maelezo yako) kuwa umezungumza na mumeo kuhusu tabia yake na ile ya dada yake lakini hakukuwa na mabadiliko, inawezekana kabisa namna unavyo wasiliana na mumeo ni tofauti na unavyopaswa kufanya.


Linapotoke tatizo kama lako ambalo linahusu ndugu wa mumeo unatakiwa kuongea na mumeo kwa upendo na mapenzi lakini wakati huohuo unakuwa "firm". Ukiwakilisha hoja zako kwa mumeo ktk mtindo wa kulalamika na kunung'unika mumeo hatochukulia umwambiayo "serious" na badala yake atadhania kuwa wewe unawalakini na dada'ke na unajaribu kuwatenganisha kama ndugu.


Nini cha kufanya: Jitahidi kujiweka kwenye "mood" nzuri yaani kuwa mwenye furaha (hii itakusaidia kumuonyesha mumeo kuwa huna chuki na dada'ke na wala huna hasira nae mumeo). Zungumza na mumeo kwa mapenzi na kwa uwazi kabisa bila kuficha kitu.........na anza kwa kuelezea hisia zako za kimapenzi juu yake, mueleze ni namna gani unafuraha kuwa mke wake na kuchangia kila kitu kwenye maisha yenu, mwambie ni namna gani wakati mwingine unajisikia mpwekwe pale anapojisahau na kutumia muda wake mwingi peke yake (usigusie kuhusu dada'ke).


Mkumbushie namna gani uhusiano wenu ulivyokuwa hapo awali (kabla Dada'ke hajaungana nanyi huko Ughaibuni lakini usimtaje wala kugusia ujio wake), onyesha ni namna gani mlikuwa mnatumia muda mwingi pamoja sio tu kama mke na mume bali wapenzi na marafiki. Muonyeshe ni namna gani ulikuwa unafurahia ukaribu wenu na unaweza kuongezea jinsi uhusiano wenu kingono ulivyokuwa then.


....wakati unaongea yote haya hakikisha hakuna umbali kati yenu na umuonyeshe mapenzi ya hisia ambayo hujawahi kumuonyesha kwa muda mrefu au hujawahi tangu mkutane, usisahau kutabasamu na ku-flirt kimtindo na mumeo huku unamuangalia moja kwa moja kwenye macho yake, mwambie hufikirii hata siku moja kuishi bila yeye na utafanya kila uwezalo kuhakikisha uhusiano wenu unakuwa bora, uliotawaliwa na mapenzi......(hapa atakuwa tayari kupokea "kibomu").

Malizia kwa kusema kuwa, ungetaka uhusiano wenu uwe kama ulivyokuwa mwanzo kwani hivi sasa hauna furaha, amani wala raha ndani ya ndoa yenu kama ilivyokuwa awali na ungependa mabadiliko.....ondoka na nenda kufanya hsughuli zako.

Hapa atakuita/kufuata akitaka kujua nini hasa unamaanisha au atabaki kimya akitafakari uliyomueleza.....usitegemee jibu au mabadiliko siku hiyo hiyo hivyo basi mpe muda na endelea kumuonyesha "mood" nzuri na kama vipi muda wa kitandani ukifika mpe mambo matamu bila kinyongo.

Wakati unaendelea kusubiri mabadiliko ya tabia ya mumeo, mtafute wifi yako na ongea nae ana kwa ana (no sms wala simu) na yeye mpe kitu cheupe kwa kifupi bila hasira wala chuki lakini cheza na Saikolojia yake.

Mwambie kuanzia muda leo aache tabia yake ya kuingilia maamuzi ndani ya ndoa yako, mwambie ulivyoolewa hukuolewa na watu wawili bali mume wako pekee ambae unampenda kwa moyo wako wote na hauko tayari kuumiza hisia za mume wako kwa kufanya mambo machafu ambayo kwa kiasi kikubwa yatakuwa yamesababishwa na tabia yake chafu (hii kisaikolojia itamfanya ahofie kaka yake kuumizwa na wewe na bila shaka atakimbia kwenda kumuambia).

Sasa kwa vile ulimpa mumeo mambo hadimu usiku uliopita alafu leo dada mtu anakuja na issue ya wewe kutopenda kumuumiza hisia hakika itafanya kazi vema kabisa.

Endelea kusubiri mabadiliko ambayo yatajitokeza ndani ya wiki chache hasa kama mumeo anakupenda lakini ikitokea vinginevyo na wanaendelea na tabia yao mbaya basi siombaya kama utatafuta ustaarabu mwingine......lakini nakuhakikishia kabisa kuwa mbinu hizi zitafanya maajabu kwenye uhusiano wako.

Kila lililo jema Mdada.

Friday

Anataka kuacha wake kuja kwangu-Ushauri

"Mambo vipi.
Mimi nilikuwa na mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwenye mahusiano kwa
miaka minne. Mwaka jana tuliachana kwa sababu kadhaa, na moja wapo ni kuwa eti
alikuwa anahisi ninamchezea hivyo sitamuoa. Pia alitaka nibadili dhehebu kutoka
Lutheran na kuwa Roman Catholic.



Kwa kweli tuligombana sana kwa sababu sikuona haja ya kubadili Dini wakati Dini ni kati yangu na mungu. Sasa wakati tunagombana alikuwa akiniambia maneno kuwa sitapata msichana
atakayenipenda kama yeye.


Tumeachana kama miezi sita hivi. Mimi niliendelea kivyangu nikachukua mwanamke
mwingine na yeye pia akapata bwana wake. Sasa cha ajabu amekuja kwangu na
kuniomba turudiane. Eti huko alikoenda hakupenda kama anavyonipenda mimi.
Eti anajuta kwa makosa aliyofanya na kudhani she can replace me.


Pia anasema amegundua kuwa jamaa ni player tu. Ingawa alimuahidi kumuoa. Sasa ameniambia
kuwa ameamua kumuacha hata kama mimi sitakubali kurudiana nae. Sasa wadau
nishaurini.



Hivi kweli huyu amedhamiria kujirekebisha na kuwa nami tu au ndio
anaona noma mambo yamwekwenda vibaya kwake? Nimchukue tena?


Halafu kitu kingine ameniambia kuwa yuko radhi kufanya mapenzi na mimi kama nitakubali coz the way I do it makes her feel good. Hata alipokuwa nae jamaa alimueleza kuwa bado nipo
kichwani kwake ingawa tumeachana."

Jawabu: Mambo poua kabisa hapa, vipi wewe? Miezi sita ni michache sana kwa yeye kukufuta kichwani kwake sio hivyo tu bali hata kuanzisha uhusiano mpya hasa kama mlipendana kwa hati na uhusiano wenu ulikuwa wa muda mrefu kama ulivyokuwa wenu. Hilo mosi.

Pili, inaelekea ninyi wawili mlikuwa mnataka vitu tofauti kwenye maisha yenu ya kimapenzi ukiachilia suala la kubadili Dini (Dini ni imani na sio muhimu sana kama mapenzi), mpenzi wako anataa sana kuolewa lakini wewe ukawa unachelewesha mambo labda hukuwa tayari au vinginevyo.

Inaelekea huyo Ex Mpenzi wako hajui kuwa unampenzi mpya na ndioa maana ameku-offer ngono akidhani kuwa una minyege mpaka kwenye kope, kama angejua sidhani kama angeshupaa kutaka kurudiana na wewe.

Mwanamke yeyote anaefananisha au kumponda mwanaume aliyekwisha kuwa nae sio wa kumuamini kwani yote anayoyasema kwako kuhusu mwanaume mwenzio ndio aliyokuwa akiyasema au atayasema kwa mwanaume wengine atakae kuwa nae kwamba yule jamaa hivi na vile na hajawahi nifikisha kabisa....kwanza ana kibamia n.k

Kutokana na maelezo yako hapa inaonyesha wazi kabisa kuwa unayo nia ya kurudiana nae ikiwa amedhamiria kujirekebisha.....lakini vipi kuhusu mpenzi ulienae hivi sasa?

Angalia wapi moyo wako unaridhia kwa ex mpenzi au kwa huyu wa sasa? Wapi unahisi unafuraha zaidi? Jiulize nini unataka kutoka kwenye uhusiano wako na je unakipata au kuna uwezekano wa kukipata? Lini ulihisi amani zaidi sasa au miezi sita iliyopita? Je uko tayari kufunga ndoa?

Kumbuka kuwa kama ulikuwa na mpenzi kwa miaka kadhaa kisha mkaachana na akaenda kulalwa na mtu mwingine kisha ukarudiana nae ilemiaka mliokuwa pamoja inafutika na mnaaza upya.....sasa je uko tayari kuanza upya na mtu aliyekuacha kwa ajili yamtu mwingine? Kama jibu ni ndio.....vipi kuhusu huyu mpenzi wako wa sasa? Kama yeye angefanya hivyo ungejisikiaje?

Tafakari majibu ya maswali nilikuuliza kisha fanya uamuzi wa busara ambao hutojutia hapo badae. Kila lililo jema!

Tuesday

Miezi 2 tayari ndoa imekuwa ndoano-Ushuhuda!

"Dada Dinah na kushukuru sana kwa kuweka hii blog kweli inatusaidia, ,mimi ni yule dada niliye omba ushauri hapa heading ikiwa miezi miwili tayari ndoa imekua ndoano. Jamani ninawashukuru wote mliochangia mada maana ushauri wenu niliuchukua nakuufanyia kazi kwa kweli nimeona mabandikiko makubwa sana.


Ninasema asante na ninaomba mzipokee shukrani zangu za dhati. Niliongea na mume wangu nikamueleza ukweli kua mwanae nilinaye tmboni ananisababisha nichoke sana na mwili muda wote umelegea legea nikamueleza kua hatamasharti anayonipa yananipa wakati mgumu najikuta nina waza muda wote kwa kweli nashukuru maana sikuamini kama ange-react namna ile kwanza alilia sana nakuomba msamaha kwangu lakini pia alimuomba mwanae pia kama vile anamsikia.


Sikuamini na kuanzia siku ile ananisaidia kupika kama napika ugali basi yeye anapika mboga wakati mwingine nikirudi nakuta kasha pika kipo mezani yani nafurahia kwakweli maana siku akiona sijakaa sawa basi hata kuogeshwa wakati mwingine nikirudi nakuta ameshafua nguo zote kazikunja vizuri.

Kwakweli sikujua kama angeweza kubadilika namna hii, kama siku za weekend yupo off basi saa kumi na moja anakuamsha mama twende tukafue mapema ili upatemda wakupumzika, akiona unafanya kazi sana bila kupumzika ,unashangaa anakuita njoo chumbani ukifika unaambiwa njoo mama nifundishe kuimba huu wimbo au hebu niangalie kuna kipele mgongoni basi tu ili akupe muda upumzike, kweli kilio changu kimegeuka kuwa furaha muda wote .

Dada Dinah ninakushukuru sana kwa ushauri wako na wachangiaji wote mungu awabariki . "

Dinah anasema: Hongera sana kwa kufanikiwa hilo. Tubarikiwe sote!

Saturday

Ndugu wanahatarisha Ndoa yangu-Ushauri

"Habari za kazi dada yetu mpendwa, baada ya kusoma ile stori ya kaka aliyemsaidia mdogoe na kisha kumpindua, nikaona nami niseme yaliyonisibu.

Mimi ni mdada wa 29 umri, nimebahatika kuolewa miaka 8 iliyo pita. Namshukuru mungu nina amani na ndoa yangu. Nia ya kuja hapa ni kutaka kujua hawa ndugu wadogo wa damu, binamu, mashangazi na wengineo tunao wakaribisha majumbani kwetu na kuwaonesha upendo wa juu na baadae kuharibu je tuwafanyaje?


Dinah mimi naweza kusema mume wangu kidogo Mungu kamjalia si sana ila kiasi cha pesa kwa mwezi mshahara unaridhisha. Sisi katika hili nikaona kwanini nisimwendeleze mdogo wangu Juma nimsimamie mpaka atakapo maliza miaka yake 3 au 4 ya chuo bila kuchukua mikopo.

Nikampanga mume wangu naye akaona ok, huruma bado ikaja kwanini huyu Hadija naye nisimtoe, ok kutokana na mambo mengineyo kama mwanamke au matatizo ya kwenu si kila mara unakuwa unamwambia mumeo utacho kwa bure, basi nikawa nafanya siri nikampangia H, chumba pale makumbusho huku akiwa ni waiter kwenye hotel.

Basi ikawa ndio mtindo kodi ikiisha anakimbilia kwa daad, baadae H akajisahau akaamua kuacha Uweitress, ikawa ndio mzigo unaongezeka zaidi kwani pamoja na kumlipia chumba kila mara ilinibidi pia kumpa pesa ya matumizi. Baadae nikasikia anaboyfriend ambaye kula kulala hana kazi ila yeye H ndio anamtake care, sio siri dada, roho iliniuma sana yaani miim nimpe pesa ya matumizi tena akamuonge boyfriend wake wakati wazazi wangu kijijini wanakaa bila matumizi ya kutosha.


Si ikabidi nikae nae chini na kunimuliza H mbona nasikia hivi na hivi, unajua yeye anaongea sana na mtundu mtundu kuliko mimi ila utundu wake si wakimaisha, majibu aliyonipa ni "hee kwani wewe utombwi? unataka nisitombw? wewe ulivyomleta bwana wako nani alikushauri, mume mwenyewe sura mbaya".


Dinah, nilishindwa kuvumilia nikamjibu kwa hasira "sura mbaya mbona pesa zake wazifutafuta?" pia nikamjibu "hao mahandsome nikiwataka ni wapo kibao pesa ninayo nikiamua namchukua napiga pamba anatoka, pamoja na sura mbaya ya mume wangu ila hatulali njaa huyo handsome utakula sura yake huko ndani? kwanza kwa huhandsome gani kiboy friend chenywewe sura mbaya, pesa ya kula hana, wa nini ?" nikamaliza. Basi yakawa malumbano, kitu ambacho kiliniuma sana.


Basada ya muda kupitai tukayasahau hayo yote, akawa na interest ya saloon nikaona njia bora ni kumpatia mtaji wa hicho akipendacho ili azuie kuomba matumizi kwangu. Nikajikaza nikatoa kama milioni 3 anunue vifaa pamoja na kukodi sehemu, kwani baada ya mwaka tena si mkataba ukaisha akawa hana tena pesa ya kurudia kulipia.


Mimi nikauchuna nikamjibu ukitaka funga rudi kwa wazazi kijijini nimechoka. Mwaka ukakata hana chanel nikamwita nikamwambie kasome upendacho ,nikalipa ada ya miezi sita kaenda shule mwezi mmoja tu, nikamuliza kunani? Akasema "ooh mimi sitaki kusoma" kwa sababu alishanunua vifaa vya salooni nikamomba atafute tena frem nitamlipia mwaka na nitampa tena mtaji wa madawa ya saloon, kweli alipata frem sayansi kwa mwaka laki 8 pamoja na bla bla milioni1.2 .

Jamani hata kufungua kinywa na kusema asante, nilibaki naduaa. Kuna siku anakaa na kumsifia ndugu yetu mmoja ambaye alishaolewa miaka 15 iliyopita ee wamejenga, wewe sijui utajenga lini? hao hao wamejisahau kuwa ndio chanzo cha kutokujenga kwangu kuwaangalia wao wamekula nini wamevaa nini watafua na nini, alafu mtu anakuja anakupitia wewe kimafumbo.


Mbaya zaidi huyu ni mdogo wangu wa damu toka nitoke hana udogo wa sana kupishana kwetu miaka 2 tu. Si huyu tu Dinah nimemtaja huyu kwasababu wa damu, nimemseidia binamu, akatoka kunisimanga kwa watu, ni wengi ndugu waliopata msaada wangu ila naambulia kutetwa na kusimangwa.


Hebu nielekezeni niishi vipi na hawa ndugu? Sometimes nasema hili nalifumbia macho ila utakuta roho inanisuta nkuona haifai, pia wanaponizidi nawaeleza mimi si tajiri wa hivyo wanvyofikiria siwezi kusaidia kila mtu, kwani hata Kikwete ana ndugu ambaao hawezi watosheleza itakuwa mimi kapuku?


Kuna baadhi ya Makabila wakiona na unaishi kwenye nyumba kubwa, gari 2, 3 zinapumua garden, basi kila mmoja anataka kuishi kwako.hususani kabila la ........ni hayo tu Dinah na wachangiaji wengine, naomba mnishauri nifanyenini ili dungu wasije haribu ndoa yangu?"


Jawabu:Hihihihi ni kweli kuna Makabila Fulani Fulani akyanani huwa wanaamia na ukishangaa-shangaa na mumeo wanachukua, tena basi wengine hata undugu wenye ulipoanzia wala hujui. Mbaya zaidi hawajali kama umepanga au umejenga, kinachoudhi hata kama unachumba kimoja wako radhi kulala jikoni au kwenye upenyo ilimradi tu wakuharibie uhuru na mumeo.....tuliache hilo!


Shukrani kwa ushirikiano wako na uvumilivu kwa kipindi ambacho nilikuwa nahamisha makazi. Suala lako sio geni miongoni mwetu au niseme kwenye sehemukubwa ya jamii nyingi za kiafrika, ndio kitu pekee kinatufanye tuwe tofauti na jamii nyingine Duniani kitu hicho ni “Family values”.


Ni wazi kabisa kama wewe ni mkubwa kwenye familia yenu unalelewa ktkmazingira ya kuwa mfano kwa wadogo zako, kuwa kiongozi wao na pale unapokuwa mtu mzina na kuanza maisha yako unahisi kuwa na majukumu Fulani juu ya ndugu zako na vilevile kuna kahatia Fulani unahisi ka kusaidia wazazi hasa kama hawana kipato au umri umekimbia (wazee).


Kitu ambacho huwa tunashindwa kukivumbua kama alivyosema mmoja kati ya wachangiaji ni kuwa kuzaliwa tumbo moja kwa maana ya baba na mama moja haina maana kuwa mtakuwa na uwezo wa kufikiri wa aina moja, upendo na kuthamini wengine in the same way.....ndio ni ndugu wa damu lakini tukumbuke sote ni “individuals” na tunafanya mambo “individually”.



Nia na madhumuni yako ilikuwa kumsimamamisha mdogo wako lakini kwa bahati mbaya hana shukurani na wala hathamini jihudi zako za kutaka kumsimamisha kimaisha ili ajitegemee nap engine awe na kidogo kama wewe au kama akiongeza bidii basi afanye makubwa zaidi ili asaidie wengine.


Kuna ndugu ambao huwa na mafanikio lakini huwa wawasaidii wenzo kijikwamua na badala yake huwapa samaki wenzao na sio nyavu kama alivyo gusia mchangiaji mwingine hapo kwenye maoni (nimependa sana msemo wako Kaka uliyesema mpe nyavu akavue samaki na sio kumpa samaki kwani atarudi tena kuomba samaki).


Sasa wapo watu wanahisi fahari kuombwa-ombwa kila kukicha na ili kuhakikisha hilo linaendelea watakuwa wanakupa “samaki” badala ya kukupa “nyavu” ukavue Samaki utakao. Wewe dada yangu ulitoa samaki na kisha Nyavu lakini mdogo wako anazidi kukurudisha nyuma kimaendeleo na kuonyesha kuwa hajali anakucheka kuwa unashangaa tu wakati wenzako wana majumba.


Hey, hakuna radhi ya ndugu si ndio?!! Timua huyo mdogo wako asie na heshima, adabu wa shukurani, na sasa “focus” kwenye familia yako, linda ndoa yako kwa kutumia muda mwingi na mumeo badala ya kufikiria hao wanandugu wajinga-wajinga, andaa maisha ya watoto wako ambao ndio wajibu wako na ukishangaa sasa na jambo likatokea ujue hao ndugu zako watasimamnga na kusumbua watoto wako kama wanavyokufanyia wewe hivyo mama changamka na anza kuwarekebishia maish ayao ya baadae hivi sasa.

Huyo mdogo wako ni mtu mzima na anapaswa kuendesha maisha yake kivyake.

Kila lililo jema mdada.

Friday

Kijana utaoa lini?-Ushauri

Ni swali aliloulizwa mfanyakazi mwenzetu
"Sina mpango wa harusi na wala sitaki kusikia Habari hiyo tena?" bwana harusi mtarajiwa aling’aka na kuinuka kutoka nje.

Kila mmoja wetu pale ndani aliduwaa, kwani katika harusi tuliyokuwa tukiisubiria kwa hamu ilikuwa hii, je kulikoni, michango kadi kila kitu kilishaanza! Ushauri wa haraka unahitajika ili kama inawezekana tuiokoe harusi hii au la jamaa ajiandae kivingine.


Jamaa huyu alikuwa akiishi na mdogo wake ambaye alimchukua nyumbani kwao alipomaliza kidato cha nne, na kuamua kumuendeleza. Ilibidi ajinyime, na kujinyima huko ndiko kuliko changia hata achelewe kuoa. Ilibidi akope kazini, kuhakikisha mdogo wake naye anasoma hadi akafikia chuo kikuu, huu ni mwaka wake wa mwisho.


Jamaa akaona sasa naye atafute jiko, kwani umri umekwenda na alichofanya ni kuenda kijijini akampate `kuku wa kienyeji’ ambaye kamaliza kidato cha nne, mrembo kweliweli. Alipomfikisha hapa Dar na kumtambulisha kwa mdogo wake, kuwa huyo ndiye shemeji yake na kwamba watafunga ndoa lakini ameonelea asubiri mdogo mtu amalize chuo ili isimkwaze katika mipangilio yake.


Siku zikaenda na jamaa akawa anasafiri safari za kikazi kwahiyo nyumba inakuwa chini ya mdogo wake ambaye mara kwa mara alikuwa akija kulala hapo kama yupo safari vinginevyo alikuwa akikaa chuoni, sasa inabidi akae na shemejiye.


Siku moja jamaa, akarudi bila taarifa,ndipo yalipompata ambayo hatayasahau maishani, na kuapa kuwa yeye hana mpango wa kuoa tena. Kwani hilo sio tukio la kwanza, alishasalitiwa kabla na rafiki yake mpenzi na hii ya sasa imekuwa kali zaidi kwani aliyemsaliti ni mdogo wake toka nitoke. Aliwakuta `live’


Kumbe huyu binti na mdogo wake walikuwa wapenzi huko kijijini wakiwa shule, yeye yupo vidato binti alikuwa msingi. Na katika ahadi zao ni kuwa jamaa akimaliza shule walianzishe. Siku zilivyokwenda binti akawa anasakamwa na wazazi wake kwani wachumba wengi walishaposa bila mafanikio, ndipo alipokuja huyu jamaa ikawa ni hitimisho.


Uolewe na huyu! lasivyo atakuoa mzee Kijashimo kama mke wa pili. Binti akawa hana jinsi, `hata hivyo jamaa huyu mpya anafaa sana, nimempenda...' binti alisema.
Kwahiyo binti alipoletwa Dar, hakuamini kukutana ma mpenzi wake wa udogoni/utotoni na kisiri wakawa wanajirusha.


Za mwizi arubaini wamefumwa na kubainisha ukweli. Jamaa alishindwa la kufanya kwani kijijini alishakabidhiwa binti wa watu kwa heshima na kiapo na binti alikubali kuwa huyu sasa anafaa(kwa kweli alivutika naye alikiri binti) na alishaamua huyu anafaa kumuoa, hakujua kuwa atakutana na mpenzi wake wa kijijini tena.


Tukirudi kwa mdogo wake ndiye kipenzi cha wazazi wake, kumtelekeza hawezi. Alipoliona tukio hili alizimia kwa muda.

Ujumbe ndio huo tunaomba sana ushauri wenu.

emu-three na wadau wengine hapa kazini.

Jawabu: Hiki kisa kinasikitisha sana lakini sioni sababu ya kumfanyaKijana kususa kufunga ndoa kwa vile tu matukio mawili yaliyotokea. Natambua wazi kuwa atahitaji muda ili kuondokana na kilichojijenga Kisaikolojia na pengine akahitaji wataalamu ili kumsaidia ku-over come hilo.


Suala sio Mdogo mtu kuwa kipenzi cha wazazi basi asitelekezwe kama alifanya kosa la kumsaliti kaka yake hakika alikuwa akistahili adhabu kubwa zaidi ya kuterekezwa lakini Mdogo mtu hajafanya kosa na kama ilivyo kwa kaka yake na mpenzi “wao” yeye pia ni “Victim” wa utaratibu wa maisha ktk jamii yetu ya kibongo.


Hakuna mwenye kosa kati yao hao wanandugu wawili na huyo binti, nafikiri jamii iliyokuwa ikiwazunguuka ndio inapaswa kulaumiwa kwani kama kungekuwa na “uhuru” wa jina kutambulishana kwa wazazi kama “marafiki wa karibu” ambao huenda pengine wana hisia za kimapenzi lakini hawako tayari kujihusisha na mwanya gono(inawezekana kabisa).


Hivyo basi kama jamii ya Kibongo ingeachia kidogo ili vijana waweze kurafikiana na badala ya kuwatisha unawaeleza ukweli wa mambo hali ambayo ingesaidia kwa kiasi kikubwa kwa familia ya binti na Mdogo wake kijana muathirika kufahamu ukaribu wa wawili hao na hivyo wasingeruhusu kaka mtu kuchukua jumla.


Kaka mtu anachopaswa kufanya ni kuwaacha wapendanao hao waendelee namapenzi yao kwa ni wao ndio walioanza kupendana na penzi lao lilikuwa asilia ulikinganisha na yeye, pengine huyo mwanamke hana mapenzi na huyo aliyemleta mjini (kaka mtu) lakini alikubali tu kwa vile hakutaka kuolewa kama mke wa pili na Mzee Kijashimo kama alivyotishiwa na Familia yake.


Kwa kifupi basi napenda kusema kuwa haya ndio matokeo ya kuficha ficha pale tunapokuwa na mafariki wa jinsia tofauti ktk umri wa ukuaji. Unajua kile kipindi cha ukuaji kila mmoja wetu huwa na hisia za kuwa na mtu wa karibu ambae mara nyingi huwa tunarafikiana kwa muda mrefu na kupendana bila kujihusisha na ngono.


Lakini tatizo linakuja kwa wazazi, ndugu na jamii kuhisi kuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya “matusi”. Badala ya kuwasaidia na kuwalezea nini cha kufanya kukabiliana na masumbufu ya ukuaji na kuwa huru kumuona rafiki yako wa jinsia nyingine unapigwa marufuku kama sio kuhamishwa na shule kabisa.


Naelewa kuwa jamii, wazazi na ndugu wanajaribu kulinda binti/kijana wao na kuzuia wasiharibu maisha yao ya badae kwa kutiana mimba ktk umri mdogo lakini hapo hapo itambulike kuwa kuna umuhimu wa kujua nani anarafikiana na mtoto wako na urafiki wao ni namna gani hasa.


Ushauri wangu ni kwa Kaka kujipa muda na kufurahia maisha yake badala ya kuhofia lini atapata “jiko” na wapi hasa linapatikana. Akumbuke kuwa Mapenzi hayalazimishwi na vilevile kila linachotokea ktk maisha yetu huwa kuna sababu kwanini hasa kimetokea.


Huyo binti hata kama ungefunga nae ndoa asingekuwa akikupenda kama alivyokuwa akimpenda Yule aliyeujaza moyo wake na kwa vyovyote vila lazima angenda tafuta mapenzi ambayo yasingekuwepo hapo ndani na hivyo ndoa yenu ingeharibika.


Napenda kuwashauri ninyi marafiki zake kumuacha jamaa aishi vile apendavyo kwani kutokana na maisha ya sasa kufunga ndoa ni uamuzi wa mtu pale anapokutana na Yule atakae ujaza moyo wake kwa mapenzi, ila kasumba ya kukimbilia kijijini unapohisi umri wa kuoa umefika sio haki kwako wewe muaji na Yule muolewaji kwani ndoa yenu ita-base kwenye “wajibu” na kila kitu maishani mwenu kitakuwa wajibu na sio mapenzi.

Kila la kheri.

Thursday

Miaka 5 na Mume wa Mtu-Ushuhuda

MIAKA MITANO NA MUME WA MTU - USHUHUDAPole da dinah kwa kazi ngumu ya kuelimisha jamii. Nakumbuka mada hiyo hapo juu niliitoa mwaka jana ila nashukuru kuna walionipa ushauri mzuri nikaweza kufanikiwa japo kuna walioniponda.


Dada yangu nimeamua kusalimu amri nimeshaachana na mume wa watu na kuamua kukaa kutulia kuhangaika na maisha yangu huku nikimwomba Mungu anisamehe sana. Ila nahitaji ushauri nini cha kufanya kwa sababu jamaa kakataa kuwaweka wazi kwa ndugu zake na hata mkewe kuwa hayuko na mimi.


Tena anasema walivojua tunauhusiano ndo watakavojua tumeachana sasa kinanishinda kitu kimoja coz mkewe ananitumia sms za matusi kila kukicha, mara anapiga simu nashindwa la kufanya sipokei wala kujibu Je nifanyeje ili huyu mwanamke asiendelee kunisumbua na ajue its over me na husbad wake? Naomba ushauri wako dada pamoja na wachangiaji wote.
Niwatakie siku njema"

Jawabu:Asante sana kwa kurudi tena na kutuma "feedback". Miaka mitano sio "kitoto" yeye huyo mwanaume mwenye tabia chafu haamini kabisa kuwa wewe kama mwanamke unaejiamini umesimama na kumwambia sasa imetosha na kila mtu achukue ustaarabu wake.


Sio wanawake wengiwa Kibongo wenye kujiamini kama ulivyoamua kuwa wewe hasa ukizingatia mume huyo wa mtu alikuwa akikuangalia ktk hjaliz zote hasa kiuchumi. Hali ya yeye kukufanyia kila kitu ali-relax nakujua kuwa "imetoka" yaani huwezi kuacha maraha anayokupa na mapesa na ndio maana hataki kabisa kuliweka wazi hilo kwa ndugu na jamaa zake. Chukulia kuwa hilo ni tatizo lake na anapaswa kurekebisha mambo na mkewe ili apate kile alichokuwa akikifuata kwako.

Huyo mwanamke anahasira sana na wewe, kama ambavyo mwanamke yeyote angeweza kujisikia baada ya kuibiwa mumewe. Tofauti ni kuwa mwanamke huyu badala ya kufanyia kazi suala zima la kwanini hasa mumewe alitoka na wewe kwa kipindi kirefu hivyo na kujaribu kujirekebisha na kuimarisha ndoa yake anapoteza muda kukutukana wewe....again chukulia kuwa hilo ni tatizo lake kwani wewe umekwisha nawa mikono na huusiki na lolote linalotokea kwenye uhusiano wao hivi sasa.

Kutokupokea wala kujibu ni uamuzi mzuri sana, sasa ilikuondoa usumbufu wa huyo mwanamke badilisha nambari yako ya simu na hakikisha hakuna mtu kutoka pande hiyo anaijua nambari mpya hiyo.

Kuwa na siku nzuri.

Pages