Thursday

Uchoyo/ubahili wake unanipa hofu kama tutafunga ndoa-Ushauri

"Mambo Dinah mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 27, ni mfuatiliaji mzuri wa Ushauri wako nina mpenzi yapata mwaka mmoja hivi sasa. Tumepanga tuje funga ndoa Mungu akijaalia.

Huyu mpenzi wangu sijui niseme ni mbahili, mchoyo au nimwitaje, maana kila wakati huwa analalamika hana hela hata tukitoka dinner anatanguliza kusema "yaani sasa hivi sina hela kabisa" hapo sijamuomba.

Kwa kawaida sina kawaida ya kumuomba hela yaani hata ninapokuwa nimepungukiwa au ninashida huwa namwambia anikopeshe halafu nitamrudishia baada ya muda Fulani lakini bado anasema hana hela.

Wote ni mfanyakazi na yeye anakipato kikubwa zaidi yangu. Naomba ushauri nifanye nini? nimsaidie vipi maana baadae asijekuwa mbahili hata kwa watoto wake."

Dinah anasema:Asante sana kwa ushirikiano na hongera kwa kuwa mmoja kati ya wanawake wachache wanaojitahidi kujitegemea kiuchumi. Ikiwa wewe una miaka 27, napata hisia kuwa mpenzi wako atakuwa kwenye miaka ya thelathini na kitu.


Kwa mwanaume yeyote kipindi hiki ndio pekee ambacho hudhani ni muhimu kujiweka sawa kimaisha kwa maana ya kufunga ndoa, kuwa na mahali pake pa kuishi, kuanzisha miradi ya kujiendeleza n.k. hilo moja.


Pili, inawezekana anamajukumu mengine kama ilivyo kwa sisi waafrika wote, kama wewe ni mkubwa kwenye familia yenu na umefanikiwa kupata kazi basi unachukua majukumu fulani kutoka kwa familia yako, inaweza kuwajengea wazazi, kusomesha wadogo zako n.k


Sababu ya tatu ninayoweza kuifikiria kwa haraka haraka ni Muda/wakati. Katika kipindi cha mwaka mmoja ni mapema sana kwake yeye mpenzi wako kuanza kukushirikisha kwenye kila jambo alifanyalo sio kwamba hakupendi bali hana uhakika kama yuko tayari kuweka wazi mambo yake binafsi labda kwa kuhofia kuwa utamkimbia kutokana na uwingi wa majukumu yake au utaendelea kuwa nae kwa kutegemea kupata kitu kwake na sio mapenzi ya dhati.

Pamoja na kugusia yote hayo hapo juu, inawezekana kabisa kuwa mpenzi wako ni mbahili, na hii inategemea na asili yake au jinsi alivyolelewa.


Nini cha kufanya: Kabla hatujampa hukumu ni vema tukajua ukweli wa mambo, je ni mbahili kweli? kuna jambo anafanya lakini anadhani ni mapema sana kukushirikisha? au kuna majukumu mengine ya kifamilia yanam-bana?


Ndani ya mwaka mmoja lazima utakuwa unajua kama jamaa anandugu ambao wanamtegemea ama la! Inawezekana kabisa ulidhani kuwa ni kitu ambacho hakikuhusu, lakini ni muhimu sana kujua watu wa karibu wa Mpenzi wako, sio lazima urafikiane nao au kuwafahamu kwa karibu bali kujua tu kuwa anawadogoz ake 3, anaishi na wazazi wake, kuna binamu n.k.


Ingekuwa mnaishi pamoja ingekuwa rahisi zaidi kwani mngegawana majukumu na kwa vile yeye anakipato kikubwa, angechukua jukumu la kulipia Nyumba na Bill ya umeme, wewe ukawa unashughulikia Bill ya maji, chakula na mahitaji mengine madogo madogo ya nyumbani na senti zinazobaki kwa pande zote mbili zinahifadhiwa kama akiba au inaenda kufanya jambo la maendeleo...kama mnajenga n.k.


Lakini kwa vile kila mtu anaishi kwake basi njia pekee ya kujua ukweli ni kutafuta muda mzuri wa kuzungumza nae kuhusiana na maisha yenu ya baadae kama wenza, tena ni rahisi zaidi kwa vile tayari mmepanga kufunga ndoa Mungu akijaalia. Wee anzisha maongezi haya kwa kuonyesha kuwa wewe ni "mama maendeleo" na hakikisha kila unalosema linauwingi kwa maana ya wewe na yeye.

Unaweza kuwakilisha hoja yako kwa utani Mf: mnatoka kwa ajili ya mlo wa jioni alafu yeye anasema sina hela.....cheka kisha muulize..."hivi kwanini wewe kila siku huna hela wakati wote tunafanya kazi? anaweza kukupa jibu la moja kwa moja kama kweli anamajukumu mengine au anaweza kusema "siku ikifika utajua kwanini huwa sina hela".....asipokupa jibu usijali kwani litabakia kichwani na atalifikiria jiono hiyo na usiku mzima na kukupa jibu atakapo kuwa tayari.

Au mpe kitu cheupe moja kwa moja....kwa upole na upendo lakini kwa kumaanisha, mwambie yote yalioujaza moyo wako, hali ya kujitegemea kiuchumi (kama ulivyosema hapa), mipango ya baadae, hofu yako juu ya maisha yenu na watoto hapo baadae n.k.

Maongezi hayo yatasaidia mpenzi wako kufunguka na kukuambia ukweli kama anasomesha ndugu zake, au anatunza hela kwa ajili ya kufunga ndoa, anajenga n.k. sasa ukipata ukweli kama ni mbahili au anamajukumu mengine tafadhali usisite kurudi tena hapa ili tujue namna gani tunaweza kusaidia kutokana na tatizo husika.

Kila la kheri!

No comments:

Pages