Sunday

Je anaweza kumsamehe Ba'Mkuu?-Ushauri.

"Dada Dinah mie nakuja tofauti kidogo. Nimekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Kijana mmoja kwa mwaka na nusu sasa. Nampenda na pia nadhani yeye ananipenda kwani huwa ananifanyia yote ambayo mimi nahisi ni kwaajili ya mapenzi yake kwangu.


Kipindi cha mwaka tumeishi pamoja baada ya yeye kuja na idea ya kusave ili tufunge ndoa mwakani, maana yake huku tunakosihi maisha ni ghali sana. Kwa vile ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishi na mwanaume nyumba moja nikamuomba mpenzi ahamie kwangu badala ya mimi kuhamia kwake na akakubali.


Nilifanya hivyo kwa vile nilikuwa naogopa kunyanyaswa kama uhusiano wetu hautofika mbali. Namshukuru Mungu tangu tumeanza kukaa pamoja maisha yamekuwa mazuri ukiachilia migongano ya hapa na pale na kupishana kwenye baadhi ya mambo. Tumefanikiwa kusave kiasi cha kutosha kwa ajili ya kufunga ndoa kuanza maisha kama mke na mume.

Kitu cha kushangaza Mpenzi wangu hajawahi kuzungumzia wanafamilia yake, mwanzoni nilidharau tu kwa vile sikutaka kumkorofisha japokuwa kuna donge linanikaa rohoni nikitaka kujua kwanini hazungumzii familia yake wala kunitambulisha kwao kwa simu!

Huwa nafikiria vitu vingi sana juu ya mpenzi wangu huyu lakini kwa vile nampenda huwa najipa moyo maisha yetu ya ndoa ni kati yangu mimi na yeye na sio watu wengine. Siku moja nikaamua kukaa nae chini na kuuliza kama utani tu.

Mpenzi wangu alicheka alafu akaniambia, alikuwa anasubiri mpaka baada ya kufunga ndoa ndio aniambie ukweli kuhusu maisha yake lakini kwa vile nimeuliza basi atasema na lolote nitakaloamua basi ataliheshimu. Akaendelea kuwa yeye hana ndugu wala wazazi na alilelewa na baba yake mkubwa ambae alimtesa sana.

Nilimuonea huruma sana na nikatamani kumkatisha lakini pia nilitaka kujua mwisho wa story yake. Mpenzi wangu ilimbidi atoroke pale nyumbani na kudandia treni kwenda kijijini ambako kulikuwa na bibi na babu yake, alipelekwa shule na kufanikiwa kufaulu na kuendelea na Sekondari lakini baada ya tu ya kumaliza kidato cha nne Babu akafariki Dunia.

Maisha yalikuwa magumu kwani bibi hakuwa akifanya kazi na wala hakupokea msaada kutoka kwa baba mkubwa. Akaamua kuacha shule na kuanza kufanya kazi ya kulimia watu mashamba ili aweze kupata hela ya kula yeye na bibi.

Baada ya miaka michache kupita bibi nae akafariki na yeye akabaki mkiwa, hivyo akaamua kurudi Dar ili kutafuta kazi na kwa bahati nzuri alipata kazi kwenye Ubarozi fulani kama mlinzi. Akajiandikisha Chuo cha ufundi lakini masomo ya jioni na kujilipia mwenyewe. Alifanikiwa kumaliza na kufaulu, akiwa na kiu ya kwenda Chuo Kikuu aliomba Udhamini kutoka kazini kwake kwani gharama za masomo zilikuwa juu sana.

Boss wake baada ya kusikia historia ya maisha yake na kugundua kuwa hana ndugu akamdhamini akasome nje ambako ndio tumekutana. Baada ya kuniambia yote hayo nilijisikia vibaya na kujuta kwanini niliuliza, nilimuonea huruma mwanaume mzima kutoa machozi.

Nilipomuuliza kwanini hakuwa wazi tangu mwanzo? akasema hakutaka niwe nae kwa kumuonea huruma kutokana na maisha yake ya zamani bali niishi nae kwa vile nampenda.

Je! Ni sawa kama nitamshauri mpenzi wangu amsamehe baba yake mkubwa na kurudisha uhusiano?"

Dinah anasema: Nimepitia ushauri na maelezo ya wachangiaji na wamegusia vitu muhimu ambavyo natumaini umevifanyia kazi. Nakubaliana na imani yake kuwa hakutaka umuoenee huruma kutokana na hadithi ya maisha yake ya zamani ambayo inauzunisha na alitaka umpende.

Kuna watu wanajenga mahusiano na hata kufunga ndoa na kuendelea kubaki kwenye ndoa kwa vile wanawaonea huruma na sio kuwa wanawapenda. Nikirudi kwa past yake nadhani naungana na wote waliosema chunguza ili kujua ukweli na kama kuna ndugu (watoto wa baba Mkubwa'ke) basi unaweza k uanza kuzungumza nao bila kuwajulisha wewe ni nani (unaweza kujifanya ulisoma nae n.k) ili kujua ukweli wa mambo.

Kama asemayo ni kweli basi heshimu uamuzi wake wa kujiweka mbali na Mzee huyo (kama bado yupo hai) lakini jitahidi kutafuta namna ya yeye kurudisha uhusiano na watoto wa mzee huyo aliyemnyanyasa ili kuepusha watoto wao na wenu kuja kutengeneza mahusiano ya kimapenzi n.k si unajua Dunia ni ndogo hii.

Mimi binafsi sina uzoefu sana na matatizo ya kifamilia lakini nashukuru wasomaji wamekushauri vema kabisa.

Kila la kheri!

No comments:

Pages