Sunday

Familia haimtaki, kasaliti penzi letu-Jawabu

Asante M3 kwa kuleta mkasa huu hapa ili watu wachangie na vilevile kujifunza. Naomba ufikishe pole zangu kwa mhusika.

Huu bwana alipatwa na mshituko siku ya tukio na bado yuko kwenye mshituko ambao unaweza kuendelea kuwepo kwa muda mrefu zaidi kama ataendelea kunywa pombe kuzima/funika maumivu badala ya kukabiliana nayo ili kumaliza maumivu ya hisia zake.

Wanadamu tunatofautiana sana linapokuja suala la maamuzi hasa baada ya kushuhudia mtu “kakunja” mkeo , huyu bwana alimuamini mke wake kwa asilimia zote hasa ukizingatia milima na mabonde waliyopitia mpaka kufunga ndoa.
Kinachonisikitisha ni kuwa mke wake hajaomba msamaha, huenda na yeye bado haamini kuwa amebambwa “live” au hapati nafasi ya kufanya hivyo kwa vile wakati wote jamaa kalewa(mpatie anuani yangu ya barua pepe nijaribu kumuweka sawa).


Akumbuke tu kuwa mtu anapoamua kusaliti penzi mara. zote huwa anasaliti penzi na mmoja kati ya watu ambao wako karibu sana na yeye iwe ni rafiki wa mke/mume, jirani, mfanyakazi mwenzie, msaidizi wa kazi nyumbani n.k (kama umepitia moja ya makala zangu kuhusu kuteleza utanielewa). Hivyo suala la kusikitika kwa kusema “rafiki yangu mpenzi aliyenipa mtaji” aliondoe tena huyo ndio mbaya zaidi!


Ninachokiona hapa kutokana na maelezo yake ni kwamba, wewe(mume) huenda ulikuwa ukifanya kazi sana ili uweze kumtimizia mke wako mahitaji yake ili asije akashawishika na watu wenye mapesa(ukizingatia kuwa ametoka kwenye familia fulani).

Inawezekana kabisa kuwa ulikuwa umejisahau na kuweka nguvu zako zote na muda wako wote kwenye kutafuta pesa ukidhani kuwa kukidhi mahitaji ya mkeo kwa kuwa na Senti ndio kuonyesha mapenzi kusahau kuwa wanawake wengine mapenzi ya mwili ni muhimu zaidi kuliko pesa......ikiwa alikupenda na umasikini wako ni wazi kuwa pesa isingekuwa kishawishi kwa mkeo huyo.


Kitu muhimu unachopaswa kukifanya hivi sasa ni kutengana na mkeo kwa muda (kukaa mbali nae), kisha acha kunywa pombe (ulevi)hatua hii ya mwanzo itakusaidia kukabiliana na maumivu yako na wakati huohuo kujua hisia zako zimesimama wapi katika hali halisi.


Hatua ya pili ni kuzungumzia tukio hilo kwa uwazi kwa watu wa karibu na wewe ambao unajua kwa uhakika kuwa watakusikiliza, kukuelewa na kukusaidia kwa kukupa matumaini na ushauri mzuri utakaokufanya ajue hisia zako zilipo juu ya mke wako na nini unadhani kinaweza kuwa kumesababisha mkewe kutoka nje ya ndoa yenu.


Epuka watu wanaotoa ushauri wa haraka kama vile kumuita mkeo majina machafu, kukuambia umuache na ushauri mwingine ambao wewe unajua hautokusaidia.


Hatua ya tatu ni kukutana na wataalamu waliobobea kwenye masuala ya Ndoa na mahusiano ya kimapenzi ana kwa ana ili uweze kupata msaada mzuri zaidi utakaokusaidia kufanya maamuzi ya busara.

Mtaalamu yeyote wa masuala haya kitu cha kwanza kukuuliza kitakuwa je unampenda mkeo? Pili utaulizwa...kitu gani unadhani /hisi kinaweza kuwa ni sababu ya mkeo kutoka nje ya ndoa?


Ikiwa utahisi kuwa bado anampenda mkeo na kupata jibu nini hasa kinaweza kuwa sababu ya mkeo kuchomoka nje basi mtaalamu huyo atapaswa kuandaa siku ili wewe na mkeo mkutane na mpewe darasa kama “pea” na hapo kila moja wenu ataulizwa maswali kadhaa ili kuwasaidia nyote wawili kutambua hisia zenu kimapenzi. Baada ya hapo mtapewa muda ili muweze kuzungumza, yaani kuwasiliana sio kuzozana na kubishana.

Inawezekana kabisa baada ya hapo ukawa hayuko tayari kurudisha uhusiano kwa wakati huo, hiyo ni ruksa kabisa kwani itakuchukua muda kusamehe na kusahau . Lakini kuzungumzia hisia zenu mbele ya mtu ambae anaelewa masuala haya itawasaidia sana.


Hatua ya nne ni wewe na mkeo kuwasiliana, kuzungumza kwa uwazi kabisa kwa kutumia maswali yangu yafuatayo:-

1)-Uhusiano wenu tangu mmefunga ndoa mpaka ulipomfumania ulikuwaje? Kuna kitu chochote kipepungua/badilika?

2)-Kitu gani kiliwafanya mpendane na muamue kufunga ndoa? Je bado hicho kitu mnacho?

3)-Mnataka nini kutoka kwenye uhusiano wenu na je wewe unataka nini kutoka kwa mpenzi wako?

4)-Unahisi nini kila unapomfikiria au kumuona mpenzi wako hivi sasa?

5)-Unamchango gani au unanafasi gani kwenye uhusiano wenu?

6)-Vitu gani huwa mnafanya pamoja kama wapenzi?

7)-Mara ngapi mnafanya mapenzi kwa wiki na je mnatosheka?

8)-Je unadhani mpenzi wako anahitaji ku-improve? Nini hasa kiwe “improved”?

9)-Ikiwa unapewa nasafi ya kumuwekea mwenza wako mipaka ni mipaka gani utamuwekea?

10)-Ni wazi kuwa hamuaminiani kwa asilimia zote kutokana na tukio, je unadhani utaweza kumuamini tena mwenza wako ?

Haya maswali huwa nayatumia ninapofanya 1-2-1 na pea yenye matatizo ili kurudisha uhusiano wao ulipokuwa na kuwapa mbinu nyingine(kutokana na majibu yao) ili kuboresha uhusiano wao na kuzuia makosa kutokea tena......D'hicious inaamini ktk kuboresha mahusiano na sio kuvunja.

Kila la kheri.

No comments:

Pages