Monday

Familia haimtaki, Kasaliti penzi letu,nimfanye nini?

"Unajua mapenzi ya ndoa ni kitu tofauti na mapenzi kwenye uhusiano wa kawaida. Linapotokea jambo ndani ya ndoa mnaweza mkasameheana yakaisha, lakini lipo jambo likitokea inakuwa kama kisu kimekata nyama pande mbili, kuziunganisha inakuwa sio rahisi inahitajika nguvu ya ziada.

Sijui wenzangu mtasemaje mkisikia kisa hiki `live' ambacho mhusika ndiye aliyeniletea na hatua aliyoichukua sijui wewe au mimi ungeweza kufanya hivyo.


'Rafiki yangu, hapa nilipo nimechanganyikiwa sina mbele wala nyuma. Wewe ndiye wa kwanza kukuhadithia kisa hiki kilichonikuta. Uliniuliza kuhusu hali ya shemeji yako, ukasema mbona hana raha, na unaona kama ananyong'onyea. Ni kweli, hana raha, na mimi mwenyewe namuone huruma kwa namna fulani, lakini hata hivyo nahisi adhabu anayoipata sasa bado haimtoshi kwa kitendo alichonifanyia.


Shemaji yako tumeoana kwa shida, wazazi wetu hawakukubali ndoa yetu, kwasababu hasa za utofauti wahali za kiuchumi. Mimi ni malalahoi, mwenzangu ametoke upande wa geti kali, lakini tukawa tumependana kupita kiasi. Hii ni habari ndefu kidogo.



Mapenzi yetu yalifikia kuposana, lakini posa ikagonga mwamba, sio tu kwa upande wa kikeni hata kwetu wazazi wangu walikataa wakisema familia hiyo ina nyodo, wanaijua sana. Lakini sisi hatukujali na kwakuwa tulishapendana tukasema mbele kwa mbele.


Visa vingi vilitokea, mpaka nikawekwa ndani kwa visingizio vya ajabu, siunajua tena hawa wenzetu wenye hela, wanaweza wakakusingizia kitu, ukajikuta umefungwa. Nilifungwa miezi kadha nikatoka jela, nabado mapenzi yetu yalikuwa pale pale, mwenzangu akawa amenisubiri na hatimaye wazee walisalimu amri, tukafunga ndoa.


Maisha yetu yalianza kwa shida, kwani jela iliharibu ajira yangu, na kupata kazi ikawa shida ajabu. Nikawa nabangaiza hapa na pale, na mungu akajalia nikajenga kibanda ambacho tunaishi na make wangu had sasa.



Mara nikaona mabadiliko ya ajabu kutoka kwa mke wangu, ile adabu na upendo nikaona kama vinafifia siku baada ya siku, lakini sikujali, kwasababu ya shughuli zangu. Ila, nikahisi kuna kitu, mbona safari za matembezi zimekuwa nyingi kulikoni, mara naenda kumuona shangazi mara mjomba nk. Lakini hata hivyo sikujali sana.


`Mwezi uliopita, … ' alipofika hapa aligeuza kichwa upande mwingine, nakahisi kuna msiba au vipi. Lakini nikahisi ni kitu fulani cha ajabu ambacho kimemkumba rafiki yangu.
'Mwezi uliopita siku kama ya leo nilirejea nyumbani mapema, sio kawaida yangu, huwa nashinda kwenye biashara zangu hadi usiku, na kama nitaamua kurejea nyumbani huwa namuarifu mke wangu mapema ili kama katoka aniachie ufungua mahali fulani.



Siku hii mbaya nilirejea ghafla, kwani nilihitaji pesa nikagomboe mzigo wangu wa pesa nzuri tu. Nilifika nyumbani, na kwa vile ni kwangu nilipitiliza ndani hadi chumbani , la haula, sikuamini macho yangu. Najuta kwanini nilirejea, nikaiona hiyo hali. Ogopa likukute lililonikuta.


Rafiki yangu mpendwa, ambaye tumeshibana, ambaye ndiye aliyenidhamini kwenye kesi yangu na ambaye ndiye aliyenisaidia mtaji wa biashara alikuwa …..sikuamini, `live' anafanya ufusuka na mke wangu…



Nilishikwa na butwaa, nikawa kama mtu aliyemwagiwa maji, nguvu iliniisha, na …' alipofika hapo niliona machozi yakimtoka.

Sijui kanini nilishindwa kufanya lolote, niliwaangalia weee, na wenyewe wakawa wameduwaa, wakisubiri nifanye la kufanya, lakini cha ajabu, niligeuka nakurejea kwenye biashara zangu, hadi jioni. Jioni nilifanya kitu cha ajabu ambacho sijawahi kukifanya, nilikunya kupita kiasi. Niliporejea nililala kama gogo, naikawa ndio tabia yangu hadi leo.



Unajua mpaka leo sijampiga mke wangu na wala sijasema chochote na huyo rafiki yangu, ila ndio wananiogopa kama nyoka. Rafiki yangu ananikwepa na kila akiniona anashituka kama kaona kitu gani sijui, mpaka watu wameshaanza kuhisi kitu.


Mke wangu ameisha/konda kwa mawazo, sijamsema, sijamfanya lolote na ninajifanya kama vile hakuna kitu kilichotokea.


Sasa rafiki yangu, sio kwamba nimepanga iwe hivyo, sio kwamba sikutaka kuchukua hatua yoyote, lakini nichukue hatua gani? nimuache?au nimfanyeje? ukumbuke kwao ni kama walimtelekeza, baada ya kung'ang'ania kuolewa na mimi.

Nimeshindwa la kufanya na siku zinaenda, na hata hamu ya kufanya mapenzi naye sina kabisa…nina mwezi sijui ladha ya mapenzi. SIJUI NIFANYEJE…


Dada Dinah, hata mimi nilishikwa na kigugumizi na sikumshauri chochote kwani mke wangu alifika na mazungumzo yaliishia hapo. Nikaona niliwasilishe hili swala kwako ili kama unaushauri, au kama wanakijiwe chako wanaweza wakashauri, ili nikikutana naye niweze kumpa hayo maoni.


Hayo ni mapenzi ya kusalitiana, je msamaha unaweza ukasaidia? Kifanyike kitu gani ili hali irejee, je upendo utaendelea kuwepo
emu-three"

No comments:

Pages