Sunday

Mume wangu kaoa M'ke mwingine,kumtaliki ni sahihi?-Ushauri.

"Hi Dinah habari za leo?
Nashukuru kwa maelekezo yako , ni mimi nilieuliza jinsi ja kupost mada. Jina langu kapuni.

Dinah nimekua mpenzi na msomaji wa blog yako, kwa kweli inamambo mengi kwa upande wangu nahisi inatoa elimu, na mara nyengine kuburudisha. Hua nasoma blog nyingi ila ni chache zimekua zikinivutia mada zake. Udumu mdogo wangu katika hili.

Mimi nijiite ni mama mzee tu nina umri wa miaka 40,nilianza mahusiano ya kimapenzi nikiwa na umri wa miaka 22,nikiwa katika mazingira ya kishule nikimaanisha chuo kikuu nje ya nchi, kabla ya hapo sikua nataka kusikia hayo mambo kwa kutegemea tutakae anza ngono ndio awe Mume wangu.

Nili bahatika kukutana na huyo kijana kwa bahati sijui niite mbaya , tulikua ni dini tofauti (mie muislamu yeye mkristo)kabla ya kuanza ngono, nilimueleza kuwa mie niko serious, sasa ikifikia hatua tukaona ni bora tuoane utakua tayari kubadili dini alikubali.

Hapo sikusita tukaendeleza kungonoka kwa miaka kadhaa tukiwa masomoni. Baadae tulirudi TZ , tukabahatika kupata mtoto, binti nzuri kabisa na tulifunga ndoa ya kiisilamu, kwa maana kua aligeresha wazee ili tupate ridhaa yao tuwe pamoja.

Baada ya muda mfupi tu wa hiyo ndoa , alinitaka nami niende kanisani tukafunge tena, nimi nilimshauri kama ni hivyo tuende bomani itakua ndio neutral, lakini aligoma kwa wakati huo, tulikua tunaishi kwenye nyumba ambayo ilikua chini ya mamlaka yangu, alihama na kuniambia huko aendako, nitaenda pale nitakapokubali kufunga ndoa ya kanisani.

Niliacha aende kwa wakati huo. Siku moja nilienda kumtembelea huko alikohamia, wakati nagonga nikasikia redio inalia mara redio ikawa kimya, baadae nilipofungua nikakuta mwanamke ametoka humo ndani. Mie niliamua kuondoka nikarudi kwangu.

Baadae jioni mume wangu alikuja kwangu na nikamuomba msamaha kwa kua sikumwambia kua naenda na kwa kuwa ameamua kuwa na yule labda nae atakua ameondoka, baadae yeye aliomba msamaha na kuniambia anataka kuwa nami ili tumlee mtoto.

Na aliniahidi anamuacha huyo msichana, na akaniruhusu kuhamia kwake, mie bila kusita nilihamia. Baada ya miezi mitatu akaenda shule ya miaka minne nje ya mkoa wa DSM. Alikua anakuja kila mwisho wa mwezi lakini kadiri miaka ilikua ikienda nikawa nahisi upendo wake kwangu ulikua unapungua, kwa maana kua alikua akija ingawa ni siku mbili lakini hashindi nyumbani kwa kutumia visingizio niko na huyu na yule (marafiki).

Hatimae alimaliza akarudi nyumbani,nikaanza kubaini simu za usiku hata saa tano,sita anapigiwa , MSG, baada ya uchunguzi niligungua ni yule mwanamke wa miaka ile na kwa MSg tayari wakawa wanaitana mke/mme. Kwa wakati huo yule mwamamke hakua nchini.

Nilipomuuliza mume wangu hii ni heshima gani ya ndoa, yeye alisema eti yule mwanamke hayupo nchini ninaogopa nini, na baadae nikabaini kadi ya benki ya yule mwanamke anayo huyu baba (mume wangu). nikamwambia hongera kwa kuaminiwa.

Kwa kweli nyumba nilizidi kuiona mbaya, nikimlaumu kwa hilo, mara nyengine aliniambia nikamshitaki kwa wakubwa. Siku moja nilichukua hatua ya kushitaki kwa kaka yake, lakini kaka yake alichonijibu sikuamini,ila nikahisi,hawanifurahii kwenye ukoo wao kwa sababu ya dini.

Shemeji aliniambia eti mimi nitafute watu wengine, ukweli sikutafuta mtu na hapo nilimwambia huyu baba (mume wangu) kama mie ninatafuta nyumba nikipata nitahama kwake kwani inaonekana ameshanichoka nahata heshima hana na ametegesha ili nijifukuze mwenyewe ili yeye asipate lawama.

Nilikua namuambia kua wanaume waliowengi wenye heshima hua wanamahusiano nje lakini wanaficha kwa wake zao, alinyamaza. Baadae akanitangazia kuanzia mwezi fulani nitaanza kulala mitara, na kweli ulipofika huo mwezi akaanza kulala huko siku nyengine.

Nilikata tamaa na hiyo ndoa Niliamua kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja , kutafuta shule, na kutafuta nyumba, kwa bahati mungu alijibu sala zangu zote, nilibahatika kupata shule nje ya nchi na nikapata nyumba.

Nilipomuambia nimepata nyumba , nitaondoka kwako hakuleta hata ile lugha ya kusema usiondoke mke wangu, nilihama mwaka juzi mwishoni na baada ya muda mfupi nikaenda shule nje ya nchi ambapo niko hadi sasa. Mwaka jana wakati nikiwa likizo nimekuta ndio anafunga ndoa ya kanisani, na hakuniambia kama ameamua kuoa ilihali tunandoa ya kiisilamu.

Nilichoamua dada ni kua nikiaenda likizo hii nimtake tuende mahakamani ili tuvunje hio ndoa na nibadilishe document, Naomba ushauri kwa hilo, niko right????

Pamoja na hayo, jambo jengine ni kua , mtoto nilienae ni mmoja, ningetamani nipate mwengine, umri ni 40kuna jibaba moja lilionesha interest ya kuzaa nami, ila hofu yangu ni mume wa mtu ana watoto wawili anasema ananipenda ila ndio hinyo, kusubiri hadi nipate asie na mke pia kwa umri wangu sio rahisi sana (inachukua muda) naogopa kuingia kwenye menopolse kabla sijajaribu tena kuzaa.

Naomba mnishauri mwenzenu, niamuaje hapo? ili nikija huo mwezi wa 12 niwe na maamuzi kama nijaribu na huyo mume wa mtu au nifanyeje?

Nawakilisha

Pole kwa maelezo mengi unajua hua ninatension ya maisha yangu ndio maana nikianza kuyaeleza hua naeka mdorongo huo, sikutegemea kua na ndoa ya aina hio

Kila la kheri".

Jawabu: Asante kwa ku-share sehemu ya maisha yako ya kimapenzi na ndoa mahai hapa. Shukurani za dhati kabisa kwa wote waliotoa michango juu ya hili.

Nisingependa kuegemea sana kwenye kitu amabacho kimepita lakini hata hivyo nitagusia kidogo tu kuwa kosa kubwa lililofanyika ni kufunga ndoa kwa "kuzuga" ndugu na jamaa wako kitu ambacho Mumeo pia alikitaka kwa kufunga ndoa ya "kuzuga" kanisani.

Unajua kila mtu huwa anazingatia vitu fulani muhimu ktk maisha yake ya kimapenzi na hatimae ndoa, na hujitahidi kwa kila wawezalo ili kuhakikisha vile vitu muhimu vinakuwepo kabla hawajaamua kuendelea mbele na masuala mengine kwenye uhusiano husika.

Kwako wewe na mume wako (kutokana na maelezo yako) pamoja na mambo mengine Dini na kuridhisha familia zenu vilikuwa ni vitu muhimu zaidi hivyo basi hilo lingezingatia yote yaliyotokea yasingetokea ( hatuwezi kubadilisha kilichokwisha fanyika)......


Uamuzi wako wa kumtaliki mumeo ni sahihi kabisa ila fanya hivyo kisheria ili kutopoteza haki zako kama mke. Jaribu kutembelea Mahaka yako ya Wilaya ya mahali ulipo na omba kuonana na Hakimu, mara nyingi inachukua wiki moja mpaka miezi 3 inategemea na uzito wa Kesi yenu.


Mahakama kupitia Hakimu ndio itatoa "samansi" ili mume wako aende mahakamani, usimfuate wewe kama wewe (nje ya sheria) kwani inaweza ikakusumbua na vilevile kufanya kesi kuwa ndefu, zingatia kuwa utakuwa nyumbani kwa likizo tu sio kwamba unaishi huko hivyo muda ni muhimu.


Hilo la wewe kutamani/taka kuzaa tena kabla hujafikia "kikomo cha hedhi" limetulia lakini usijifikirie wewe zaidi bali yule mtoto atakae zaliwa na yule ulienae hivi sasa. Fikiria maisha yao ya baadae na mahusiano yao na baba zao.


Hilo baba lenye kuonyesha "interest" kuzaa na wewe wakati tayari anamke na watoto halija kaa vema kwani atakuwa anacheza nje ya ndoa yake kitu ambacho wewe machungu yake unayajua, sasa kwa kujali hisia za mwanamke mwenzio na kuepuka huyo mwanamke mwenzio kutopata maumivu uliyopitia wewe (mume wako alipoibiwa na mwanamke mwingine na hatimae kufunga ndoa) jiepushe na huyo jamaa.


Miaka 40 sio uzee (uzee ni muonekano wa ngozi yako na unavyojiweka wewe sio namba), nina hakika kabisa kuna vijana wengi tu ambao hawajaoa au wale "Wajane" (wanaume wanaitwaje vile?...)na wako huru kabisa kuanzisha uhusiano mzuri na wewe na hatimae kujizalia mtoto au watoto zaidi.

Kila la kheri dada....

No comments:

Pages