Thursday

Ex analazimisha nirudieane nae, nimekataa anatishia maisha yangu-Ushauri

"Habari dada Dinah! pole sana kwa kazi nzito uliyonayo ya kutusaidia kwa mawazo na kutuelimisha. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 32 ni mwajiriwa wa Shirika moja hapa Dar.Nilipo kuwa Kidato cha 2, nilikuwa na mahusiano ya kimapenzi na dada mmoja, kwa ukweli nilimpenda sana.

Tulivyohitimu Kidato cha 4 kwa bahati mbaya mwenzangu hakuchaguliwa na mimi kuchaguliwa kwenda Kidato cha Tano, Wazazi wake waliamua arudie Kidato cha 3 Shule 1 ya Sekondari ambayo ilikuwa Wilayani na wakati huohuo mimi nilitakiwa kwenda kuendelea na masomo shule 1 huko Dar!

Kifupi ilikuwa siku ya majonzi kwetu kutengana kwani ndio ilikuwa mara yetu ya kwanza kuwa mbalimbali. Nashukuru Mungu nifanikiwa kumaliza Kidato cha 6 na mpenzi wangu alifanikiwa kumaliza Kidato cha 4! Mimi nilijiunga na Chuo Kikuu nae akaamua kwenda kujiunga na Chuo cha Ualimu.

Matatizo ya uhusiano wetu yalianza pale ambapo mwenzi wangu alimaliza na kupangiwa kituo cha kazi huko mkoa wa Tabora! kwani kwa kipindi chote ambacho tulikuwa mbalimbali tulizoea kupigiana simu angalau mara 3 kwa siku na hamna siku kupita hatujapigiana simu!

Baada ya yeye kupata hiyo ajira akawa hapigi simu hadi mimi nimpigie, nilikuwa naumia sana natabia ile mpya, siku 1 nikamwambia ukweli kwanini mimi ndio nimpigie simu na nisipopiga ndio siku hiyo hatuwasiliani? Akanijibu tena kwa ukali kuwa yeye kapelekwa huko(Tabora) kufanya kazi na wala sio kunipigia simu mimi.

Kwa kifupi yupo busy! Niliumia mno na jibu lile lakini kwa kuwa nilimpenda nilimuomba radhi kama swali lile limemuudhi, tukaongea mambo mengine tu. Baada ya miezi michache kupita, ghafla simu yake ikawa haipatikani.

Niliteseka sana ikabidi nimtafute dada yake ambaye yeye hakunificha aliniambia wazi kuwa mdogo wake(yaani mpenzi wangu) amefunga ndoa na anadai kaniacha mimi kwa kuwa sina future!

Nilihisi kuchananyikiwa nikawa kama siamini nachokisikia! Nilikubaliana na hali halisi japo iliniathiri kimasomo na ilinichukua zaidi ya miezi 6 kumsahau! Nashukuru nilimaliza Chuo na baada ya muda mfupi nilipata kazi nje ya nchi. Kitendo cha kuondoka Tz kilinisaidia kwa 90% kumsahau kabisa mwanamke yule na nimekaa huko miaka 4 nikachoka nikaamua kurudi Tz.

Niliporudi Tz nilianza kufanya kazi hapa nilipo(ilikuwa mwaka jana mwezi wa 8)!Mwezi February mwaka huu, asubuhi moja nikiwa kazini nilipokea simu kutoka kwa yule dada(Ex~girlfriend wangu) akadai kwa muda ule yuko Dar kaja kwangu kwani anamazumgumzo ya kina nami(kumbuka ni zaidi ya miaka 5 hatujaonana wala kuwasiliana).

Tukakubaliana, tukaongea mengi mojawapo ndio lililonileta kwenu ndugu zangu mnishauri, nalo ni:-Anadai kuwa kuolewa kule alilazimishwa na alikuwa hampendi yule mwanaume hata kidogo. Kwa kuwa alikuwa ananipenda mimi ndio maana ameamua kumwacha yule mumewe na kunifuata mimi!

Mimi nilimwambia ukweli kuwa; KWANZA ndoa ya Kikristo haina Talaka, PILI siwezi kuwa nae kutokana na ukatili alionifanyia! Wadau naomba ushauri wenu kwani sasa hivi imekuwa kero kwangu. Yaani mwanamke amekuwa akipiga simu na kutoa vitisho kuwa kama sitomkubalia basi atakunywa sumu nakuandika Waraka kuwa mimi ndio nimesababisha hivyo. Ili mimi nishikwe na Polisi na kutumikia kifungo kwa rest of my life.

Kwa ukweli mimi siwezi kurudiana nae hivyo naomba mnielekeze njia gani nizitumie ili niondokane na kero hizo! Kingine ni kuwa toka niachane na mwanamke huyu nimetokea kuwa chukia sana wanawake, sina hamu tena ya kuwa na mwanamke na ni mwaka 5 sasa sijawa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamke!

Je hali hii ikiendelea ndio kusema sitooa tena na ukizingatia umri unaenda? Naombena msaada wenu ndugu zangu na akhsanten sana.
Collns H.M
Dar "

Dinah anasema:Kabla hatujapoteza muda, hebu chepuka kwenye kituo Cha polisi na ripoti vitisho kutoka kwa huyo Ex na waeleze sababu ya Mwanamke huyo kukupa vitisho hivyo, kisheria Polisi wanatakiwa kukulinda wewe kutokana na vitisho vya mwanamke huyo.

Kama anakufuata-fuata Ofisini au nyumbani kwako yeye atapewa barua kwa mujimu wa Mahakama kuwa haruhusiwi kukatiza karibu na wewe na akionekana eneo hilo (unapofanya kazi/ishi) polisi wanahaki ya kumuondoa kwa nguvu.


Sasa ikitokea kajiua atakuwa kajiua kwa matatizo yake mwenyewe na wewe utakuwa salama kwani Polisi watakuwa na maelezo yako yote. Hakikisha unapata copy (nakala) ya maelezo yako, jina na cheo cha Polisi aliechukua maelezo yako, muda (siku, tarehe na mwaka), na jina la kituo just incase polisi huyo atahamishwa au kupoteza ushahidi.

**********************************************************

Baada ya kutendwa na kuumizwa na mtu uliemuamini na kumpenda imekuwa ngumu kwako kuamini wanawake, sidhani kama unatuchukia wanawake wote bali hutuamini. Kuna hali fulani ya uoga wa mwanamke mwingine kurudia kilichofanywa na Binti uliempenda.

Kwa kawaida huwa nashauri mtu ajipe muda (kaa mbali na uhusiano wa kimapenzi) mpaka utakapo pona kabisa kihisia, kupona huko kunaweza kuchukua muda mrefu kuanzia miezi sita mpaka miaka saba. Urefu wa uponaji kihisia unategemea zaidi na muda wa uhusiano wenu.

Kama uhusiano...kwa Mfano: ulikuwa wa miaka miwili na zaidi kupona kwake huchukua muda mrefu pia. Kutokana na maelezo yako inaonyesha ulikuwa umepona lakini baada ya huyu mwanamama kuanza kukufuata fuata katonesha kidonda hivyo kukurudisha nyuma.

Hali hiyo ya "kuchukia" wanawake ikiendelea hakika hutoweza kuoa au tuseme kuishi na mwanamke unless other wise uamue kufunga ndoa na mwanamke ili kutimiza wajibu kitu ambacho ni hatari sana.

Ili kuepuka hilo wewe mwenyewe unatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kukaa mbali na huyo binti "machafuzi" ili uweze kuendelea na maisha yako mapya, hilo moja.

Pili, unatakiwa kurudisha imani juu ya wanawake, kwani si wanawake wote tunatabia chafu. Kuthibitisha hilo angalia wanawake wote kwenye familia yako je wanatabia kama ya Ex wako? Hapana! sasa hiyo inamaana kuwa kosa la mwanamke mmoja halibebwi na wanawake wote Duniani. Kurudisha kwako imani juu ya wanawake ndio njia pekee ya wewe kuwa karibu na viumbe hao na hivyo kudondokea mmoja kimapenzi.

Ni matumaini yangu maelezo ya wachangiaji yamesaidia kwa kiasi kikubwa kufanya uamuzi wa busara ili uendelee kuishi kwa amani na hatimae kupenda tena.

Kila la kheri!

No comments:

Pages