Wednesday

Mume kanitelekeza kisa Ndugu zake, Je nina ndoa au sina Ndoa?-Ushauri

"Pole na kazi Dada Dinah,
Mimi ni Mama wa watoto wawili, nilifunga ndoa 2004. Kwenye ndoa yetu ikatokea upande wa mume wangu hawajanikubali sana. Siku zilivyosonga mbele kukawa hakuna maelewano kabisa nyumbani kati yangu na mume wangu.

Mwaka 2008 December, Mume wangu akahama nyumbani na aliniachia mtoto ambae kwa wakati huo alikuwa bado ananyonya, nilijaribu sana kumbembeleza arudi nyumbani lakini sikufanikiwa, kwa sasa anaishi Arusha.

Mwaka 2009 July mtoto wetu mdogo aliumwa sana kiasi kwamba nilichanganyikiwa, nilimueleza baba yake ambae ni mume wangu alienikimbia lakini hakuja kabisa kumuona mtoto. Toka 2008 alivyoondoka mpaka leo amesha kuja kututembelea kama mara mbili tu kwa madai kuwa Dar na Arusha ni mbali sana, hivyo hawezi kuja mara kwa mara kwani huwa anachoka.

Mara chache anatuma zawadi kidogo za watoto. Na toka aondoke ameshatuma kama laki tatu hivi na watoto wote wanasoma sasa, hajui naishije na watoto wanakula nini, yaani kwa kifupi hana habari na watoto wake.

Sasa dada naomba ushauri wako, unaona hapo kuna ndoa tena?
Mimi ninafikiria nitafute makazi yangu nihamae na watoto wangu kwani ninapokaa ni kwake yaani ni nyumba yake.

Kama watoto wakimkumbuka sana baba yao huwa nawadanganya, ila huyu mkubwa (5yrs) naona ameanza kuelewa kwani akiniuliza huwa namwabia hali halisi namuona kama ananza kuelewa na anapata uchungu sana.

In short naona kuliko niendelee kuumia moyo wangu ni better ni give up, nianze maisha mapya, nifanye juu chini nisomeshe hawa watoto na nijihesabu kuwa ni single parent.
Unanishaurije?"

Dinah anasema:Pole sana kwa yote unayokabiliana nayo, inasikitisha kuwa mumeo amefuata matakwa ya wazazi wake na hivyo kukuoa na kisha kukuacha "solemba". Kwasababu tayari mmekwisha funga ndoa na bado of course mko kwenye ndoa kwa vile hakuna Talaka iliyotolewa na kwa mujibu wa Imani za Dini, wewe kama mkewe na mama wa watoto wake unahaki zote za kubaki kwenye nyumba hiyo. Hiyo nyumba ni yenu na sio yake.

Kutokana na maelezo yako nadhani kinachomshinda kuja kuwaona watoto mara kwa mara ni mwanamke/mke mwingine anaeishi nae huko, Arusha na Dar sio mbali kiasi kwamba mtu ukatembee mara moja kila baada ya miaka miwili! Lazima kuna kitu kinamzuia kuja huko mara kwa mara bila "sababu ya msingi" hasa kama mwanamke alienae hajui kama jamaa alioa/anawatoto.

Kibinaadamu Dada mpaka sasa huna ndoa, ni kama vile jamaa amekuweka spea tairi kwamba yakimshindwa huko Arusha basi wewe upo hapo kwa ajili yake (wapo wanaume wengi tu wa Kitanzania wanafanya hivi).



Huyo mwanaume kama anajali maisha mema ya watoto wake hakika hawezi kukufukuza kwenye nyumba hiyo, lakini kwa vile sio muaminifu (amekukimbia) hivyo kumuamini kwenye masuala mengine sio kitu rahisi. Inawezekana kabisa siku moja akaamua kuiuza nyumba yenu alafu wewe na watoto kuhamishwa bila kupenda.

Sasa ili kujiondolea hofu na kuwa na uhakika wa mahali pa kuishi na watoto wako ni vema ukawahi kumtaliki mumeo (mpe Talaka), kisheria ndani ya Tanzania una haki hiyo. Ni vema ukienda Ustawi wa Jamii lakini tatizo la hawa jamaa wanakalia kesi za watu kwa muda mrefu sana. Pia TAMWA inawanasheria wazuri ila wanazile za "njoo kesho" nyingi na hivyo kucheleweza mambo.

Mimi kama Dinah nakutokana na uzoefu wangu na "Mahakama" ningekushauri uende moja kwa moja Mahakama ya Wilaya ya hapo unapoishi na kuomba kumuona Hakimu anaeshughulikia masuala ya Familia na ndoa. Ukipata nafasi ya kumuona (inategemea how busy she/he is) then muelezee matatizo yako ya kindo tangu mwanzo, maisha yalivyo hivi sasa na nia yako ya kutaka kumtaliki mumeo.

Mumeo anaandikiwa barua ya kuitwa Mahakamani ili Hakimu aweze kusikiliza upande wa pili na kupata ushahidi au sababu zilizomfanya jamaa akukimbie, baada ya hapo unaweza ukapewa nafasi ya kueleza nia yako ya kumtaliki mumeo au Hakimu anaweza kuisema moja kwa moja (kwa vile tayari umekwisha mueleza nia yako).

Kesi itaendeshwa kwa muda wa kati ya wiki 2 mpaka mwezi mmoja, inategemea kama mumeo atakuja Mahakamani na kuwa mbishi kuchukua/kubali Talaka kwa sababu zake azijuazo yeye au atataka kurudiana na wewe n.k.

Kutokana na urefu/umri wa ndoa kisheria mali zinagawanywa kwa manufaa yenu wote wawili na watoto mliozaa, lakini wewe utapendelewa zaidi kwa vile umekuwa ukilea watoto peke yako kwa muda wa miaka miwili hivyo ni wazi nyumba itakuwa yako pamoja na mali nyingine zinazowahusu ninyi kama wanandoa tangu 2004-2010.

Vilevile mumeo atalazimika kisheria (Mahakama itaamua) kuwa anatoa kiasi fulani cha pesa kila mwezi kwa ajili ya matunzo na elimu ya watoto, hata kama wewe unuwezo huo bado kisheria atalazimika kuchagia unless otherwise wewe mwenyewe ukatae.


Ikitokea umefanikiwa kuachana na mumeo kisheria, hakikisha hujengi chuki na mpe nafasi ya kuwaona watoto wake au watoto kumuona baba yako kila anapopata nafasi ya kufanya hivyo. Hakikisha watoto wanakuwa na uhusiano mzuri na baba yako.

Kumbuka tofauti zenu na chuki ya wakwe zako haziwahusu watoto waliozaliwa. Ikitokea watoto wanataka kujua kwanini baba hakai hapo nyumbani unaweza kuwaambia tu kuwa anafanya kazi mbali na siku akipata likizo atakuja kuwaona. Kamwe usiwaambie watoto kuwa baba yenu hawaenzi ndio maana hayupo hapa.....hakikisha unajenga uhusiano mzuri kati ya baba na watoto hata kama baba huyo anakuja kuwaona mara moja kila baada ya mwaka.

Talaka sio suluhisho na siku zote wanaoteseka ni watoto, lakini kutokana na unayokabiliana nayo Talaka itasaidia wewe kuwa huru kiakili na kuendelea na maisha yako kama mwanamke na vilevile kuwa na mahali penye uhakika ili kukuza watoto wenu.

Hongera kwa kuonyesha msimamo wako kama mwanamke, hongera kwa kusimama imara kwa watoto wako kama mama.

Nakutakia kila la kheri katika maisha yako na watoto wako.

No comments:

Pages