Monday

Mume hana uzazi, naombwa kumimbisha-Ushauri

"Mimi ni bosi nimeanzisha Kampuni yangu hivi karibuni. Kwenye Kampuni yangu nimeajiri wanawake wengi kuliko wanaume. Sifa ya kampuni yangu ni nidhamu na kweli wafanyakazi wote wanajiheshimu, kosa likitokea linaamuliwa kihekima.


Mimi ni mume wa mtu na ninaiheshimu sana ndoa yangu na hakuna kitu kinachoniuma kama kutoka nje ya ndoa, haya nayasikia mitaani na kwenye vyombo vya Habari. Watu wanasema tembea uone, Ishi na watu ujifunze na lisemwalo lipo kama halipo hujaliona tu bali linakuja.


Siku moja nikiwa Ofisini nikichambua CVs za wafanyakazi wangu na utendaji wao, hodi ilisikika mlangoni. Sio kawaida mida kama hiyo ya jioni kwa wafanyakazi kuja ofisini kwangu wengi wanakuwa wakifunga mahesabu yao tayari kuondoka.


"Bosi samahani sana, kama huna muda nitakuja siku nyingine, lakini hili tatizo nililo nalo halihitaji muda, kwani nimehangaika nikaona mtu pekee ninayeweza kumuamini ni wewe" alisema huyo mbisha hodi na alikuwa bado anaogopa huku akiwa kainama chini. "Ok, kaa hapo kwenye kiti nasema shida yako" Nilimwambia, huku nikijiuliza kichwani ni shida gani? kwani katika wafanyakazi ninaowaheshimu ni pamoja na huyu dada, umri wake ni miaka 34.


"Bosi naomba chonde chonde, hiki ninachokuambia kiwe mimi na wewe na naomba saana unikubalie, kwani usiponikubalia sidhani kama nitaweza kufanya kazi hapa tena, je nitakuangaliaje machoni, je nitaiwaka wapi sura yangu. Naomba usinielewe vibaya, mimi tangu nizaliwe sijawahi kutenda dhambi, sijawahi…" Alinyamaza nakuanza kulia.


Hali hii kidogo ilinishangaza, nakunifanya niache kazi yote niliyokuwa nikiifanya, nilimwangalia kwa makini huyu dada na kujaribu kufikiria tatizo analoweza kudiriki kuja kuniambia nikashindwa kuelewa.


"Naomba ujisikie amani, kwani nakuheshimu na moja ya kazi zangu ingawaje mimi ni bosi wenu, lakini pia ni kama mzazi, kaka, hata ukisema mume au vyovyote ilimradi haivunji hadhi, heshima ya kila mmoja wetu au sio? sasa ongea kama unaongea na mtu unayejisikia huru kuongea nae".


"Sikuhakikishii moja kwa moja kuwa ninaweza kulitatua tatizo lako, lakini nikilisikia kama lipo ndani ya uwezo wangu nitalitatua. lakini kama nikishidwa nitakuambia na halitatoka nje ya mimi na wewe kama unataka iwe hivyo, sasa uwe huru’’ nilitulia na kumwangalia.

"Bosi naogopa sana, na tangu tulizungumze mimi na mume wangu, nimekuwa sina raha, sio kwasababu limetusibu bali ni hizo njia za kulitatua ni nzito na sizipendi kama asivyozipenda mume wangu, lakini yeye sasa ameng’angania kuwa tufanye"


Akaanza kuelezea tatizo hilo, kuwa wao wameoana siku nyingi karibu ya miaka 16 sasa, katika mihangaiko yao wamechuma na wana hali nzuri kimaisha, kwani wana nyumba zaidi ya nne walizopangisha , wana magari ya biashara nk. Yeye alikuja kufanya kazi kwangu kwasababu alihitaji kupata ujuzi wa kuweza kufungua kampuni yao baadaye, alishanieleza hili kabla. Tatizo linalowakabili, tangu waoane hawajawahi kupata mtoto.


Awali walidhani mke ndiye mwenye matatizo, na jamii ilijaribu kuingilia kati ikashindwa kutokana na mapenzi waliyokuwa nayo. Baada ya miaka kwenda, waliamua kwenda kuwaona Wataalamu ili wajue tatizo ni nini.

Kila hospitali waliyokwenda waliambiwa kuwa "mume" ndiye mwenye matatizo. Na kweli katika kukumbuka, wakati wapo kwenye fungate walipata ajali, na mume wake aliumia maeneo ya mgongo, na kiunoni. Alitibiwa akapona na majombozi yalikuwa kama kawaida, lakini kumbe ile ajali iliharibu na mengine.


Binti yule aliendelea "hivi karibuni mume wangu amesema anahitaji mtoto, lakini hataki wa kurithi anataka azaliwe na mimi na anataka isijulikane kuwa anatatizo. Kwahiyo wazo lake ni mimi nimtafute mume anayefanana nae, mwenye heshima na anayejua kutunza siri na ambaye hataweza kwa vyovyote kuleta fujo hatiamaye" alimiliza kwa uchungu.


"Masharti yake mengine ni kuwa, yeye hataki kumjua huyo mume nitakayetembea naye na asijue nini kinachoendelea. Pili huyo mume akubali na ajue kuwa yeye ameridhia, kwa masharti kuwa iwe siri, pia mke wa huyo mume asijue", alimaliza binti yule.


Jasho lilinitoka, nikatamani kumfukuza huyu dada, lakini niliheshimu wadhifa wangu na kweli nilibadilika kwani yule dada aliponiona nilivyobadilika alianza kutetemeka kwa woga. Nilichoweza kumwambia ni kuwa anipe muda nifikirie kwanza mimi sio Mungu kuwa natoa watoto. Pili nitahakikishaje aliyoyasema ni kweli? tatu, hilo linavunja miiko ya ndoa yangu.


Alivyoondoka pale nilimuonea huruma, kwani nahisi alijuta kuniambia. licha ya kumpa matumaini ya kuwa asijali azidi kuja kazini, na nitajitahidi kusaidiana naye kulitafutia ufumbuzi.

Je dada Dinah na wengine mwasemaje, naomba busara zenu!
emu-three"

No comments:

Pages