Thursday

Niache Mpenzi kwa ajili ya Ndugu?-Ushauri.


"Dada Dinah,ningeomba ushauri wako.
Nimekua na mpenzi wangu kwa zaidi ya miaka miwili ingawa alikua anaishi kwao lakini alikua akija kwangu na hata kushinda au kulala siku zingine. Sasa hivi majuzi mdogo wangu wa kiume alihamia kwangu baada ya chuo chao kufungwa ghafla na hivyo tukawa tukiishi nae.


Tatizo likaanzia hapo, siku moja nikarudi nakumpa mdogo wangu hela akanunue vitu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mpenzi wangu huyu akaanza kulalamika sana mpaka sasa bado hatujapata mwafaka.


Zaidi anadai kua kuwa atasitisha kuja kwangu kwani inaonekana amekua akikwaza ndugu zangu na pia anadai kua huyu mdogo wangu ham-respect na pia anaona kama yeye anamzibia uhuru wa kukaa nami kama ndugu yake.


Nilipokaa na mdogo wangu kumwuliza yeye alikana kabisa katu katu kwamba hana tatizo nae na pia anamheshimu sana kama shemeji yake. Niliporudi na kumueleza huyu mpenzi wangu akaruka akasema ni mnafiki na wala hamaanishi hivyo.


Cha ajabu nimemwambia niwakutanishe yeye na mdogo wangu amekataa akisema hawezi kukaa na kubisha na shemeji yake yeye atakachokifanya ni kutokuja kwangu. JE HAPO MIMI NIFANYEJE KWANI NIKO NJIA PANDA,nafikiria niachane nae au la kwani simwelewi anataka nini?

Jana nikawa nimempa hatima kua kama hawezi kuishi na ndugu zangu kwa upendo kama anaonipa mimi basi sioni sababu ya kuwa nae akanitumia msg kua NITAFUTE ATAKAE WEZA WAPENDA NDUGU ZANGU.Nimekua njia panda kwani kiukweli nilikua na malengo makubwa nae ila naona nashindwa. Je nifanyeje? Iteitei"

Jawabu: Pole kwa kuwekwa njia panda. Ningependa kufafanua kidogo tu hapa kabla sijaendelea. Hata siku moja Mpenzi wako hawezi kupenda ndugu zako kama anavyokupenda wewe! Husitegemee mpenzi wako kuwapenda ndugu zako, kwani halazimiki kufanya hivyo.


Yeye kukupenda wewe haina maana kuwa aipende familia yako nzima, ikitokea wanaelewana na wakampenda na yeye akawapenda kama ndugu zako (sio kama akupendavyo wewe) mshukuru Mungu, vinginevyo anapaswa kuwaheshimu (na wao wamheshimu pia) na sio kuwapenda. Kupenda ni hisia, hailazimishwi.


Ndugu wakati mwingine huwa wakorofi, baadhi huwa wanaamini kuwa unamaliza pesa kwa mwanamke na sio kwao kama ndugu zako. Wanasahau kuwa wewe sasa ni mtu mzima unastahili kuwa na maamuzi yako na kuendesha aina ya maisha utakayo au niseme kuwa na maisha yako.


Wewe umekuwa na mpenzi wako kwa muda wa miaka miwili na uhusiano wenu ni mzuri na wakaribu kiasi kwamba Binti huja kushinda na kulala kwako mara kwa mara. Katika hali halisi huyu binti alikwisha jiona yeye ndio mwanamke kwenye nyumba yako au hapo kwako, lazima alikuwa akijipa majukumu fulani kama "mwanamke" na jukumu moja wapo ni kufanya manunuzi kwa ajili ya matumizi hapo nyumbani.....huenda wewe ulikuwa hujui au hukutilia maanani kama mwanaume.


Sasa baada ya mdogo wako kuja hapo kwako, wewe ukahamisha jukumu moja la kufanya manunuzi kwa ajili ya matumizi hapo nyumbani ambalo labda kwake yeye mpenzi wako lilikuwa jukumu muhimu sana kama mwanamke wako au mwanamke ndani ya nyumba. Hakika hapo ndipo alipokwazika na kumempotezea kujiamini kwake.


Wewe kama mwanaume ulitakiwa kugundua hilo (alipokasirika) na kumrudishia jukumu hilo yeye, kwamba endelea kumpa pesa za manunuzi ya vitu yeye na sio Mgeni (mdogo wako). Huyu mpenzi wako aliposema kuwa anasitisha kuja hapo kwako kwa vile Mdogo wako hamheshimu na vilevile kuwapa uhuru ninyi kama ndugu, alitegemea wewe kuwa upande wake kama mpenzi wake.


Sio kwa kumuunga mkono na kwenda kumsakama mdogo wako bali kwa kumhakikishia kuwa unampenda na hakuna mtu atakaeingilia na kuharibu penzi lenu. Avumilie kwa sasa kwani mdogo wako yuko hapo kwa muda tu.


Kwasababu hukumuelewa (wanawake wengine husema hivi kumbe wanamaanisha vile), ndio maana amekataa kukutana na kupatanishwa, alichotaka huyu ni kuhakikishiwa nafasi yake kwako kama mpenzi na kurudishiwa jukumu ambalo labda alikuwa kalizoea kama mwanamke wako.

Uwepo wa mdogo wako hapo nyumbani inakuwa ni tishio kwake hasa kama hawakuwahi kukutana kabla, kwani baadhi ya wanawake hudhani kuwa ndugu wanaweza kuwa-feed wapenzi wao maneno ili watimuliwe.......sasa kwa vile Dogo ni mwanaume huenda hata muda mwingi unatumia nae kuliko kufanya hivyo na mpenzi wako hali inayoweza kumfanya ajishitukie....(asijiamini).


Nilichokiona hapa ni kuwa ninyi wawili mnapendana na wote hamjui mnataka nini kutoka kwenye uhusiano wenu na hivyo mnabaki kupigana mikwara, yeye hataki kuja kwako tena ili kukupa uhuru na ndugu yako.


Wewe unataka aishi na ndugu zako kwa upendo kama anaokupa wewe na akishindwa huoni sababu ya kuwa nae(sasa uko nae kwa ajili ya ndugu zako au kwa vile unampenda?)......kumbuka yeye hajatamka kuachana na wewe.....lakini kutokana na mkwara wako kakupa jibu zuri kabisa kuwa ukatafute mtu atakaependa ndugu zako kitu ambacho hakiwezekani!


Kuishi na ndugu na kuwapa upendo kama anaokupa wewe ni kitu ambacho hakiwezekani (rejea maelezo yangu ya awali), lakini kuishi nao kwa heshima ili kuboresha amani inawezekana.


Kosa-Ulishindwa kung'amua kuwa umemnyang'anya mpenzi wako jukumu ambalo lilikuwa muhimu, pia ulishindwa ku-handle the issue kama mwanaume na badala yake ukatoa lawama huku na kuzipeleka kwa Mdogo wako alafu tena kwa mpenzi wako na mbaya zaidi ukaegemea upande wa mdogo wako badala ya mpenzi wako ambae pengine angekuwa mkeo (una mipango mingi nae).


Nini cha kufanya-Mtafute Mpenzi wako, Omba msamaha kutokana na uamuzi wako(kama mwelevu na yeye pia atakuomba msamaha kwani alikosa pia kwa kusema vitu indirect) na kaeni chini mzungumzie hili suala kwa uwazi zaidi.


Kama kutakuwa na tatizo lolote au mpenzi wako anahisi kutojiamini mbele ya ndugu zako basi mhakikishie mapenzi yako juu yake, ni kiasi gani umeji-commite kwake na ungependa penzi lenu liende wapi kama ni uchumba alafu ndoa.....kama hivyo ndivyo basi ungependa yeye na ndugu zako kuheshimiana (sio kupendana).


Siku nyingine maneno maneno yakitokea usiende kuuliza upande wapili kabla hujapata ushahidi, "handle" kiutu uzima kwa kufanya uchunguzi, pata ushahidi kisha zungumza nao kwa nyakati tofauti na kuwapa onyo.


Hakuna sababu ya kumuacha Mpenzi wako kwani inaonyesha kuwa anakupenda, ila hajiamini. Kama na wewe unampenda na unamtaka basi mtafute, muelezane, msameheane, muonyeshane mapenzi na mrudiane.


Kila la kheri.

No comments:

Pages