Thursday

M3 on Washenga!

"Dada Dinah, kuna kisa kimoja kimetokea nikaona ni heri nikiweke hewani ili tupate kushauriana na pia kama inawezekana jamii ielimike na hili, kwa kukemea au kuwa na tahadhari nalo.

Hiki ni moja ya visa vinavyoharibu uhusiano na mapenzi ya kweli katika jamii, sio hadithi au riwaya. Kuna hawa watu wanaoitwa `washenga’ na kuna kundi jingine linaitwa `makuwadi’. Tukio hili linahusu washenga.


Kuna tofauti kubwa ya washenga ambao wanafanya jambo halali katika uchumba kwenda kwenye ndoa. Lakini lipo kundi jingine la makuwadi wao wanafanya kazi ya kuwatafutia watu wengine wanaume au wanawake kwa minajili ya starehe tu, bila kujali ni nani unayemtafutia au madhara gani yatakayotokea baadaye.


Kisa hiki kimetokea maeneo ya kwetu, na kuiva hivi karibuni. Mwanzoni nilifikiri ni hadithi tu, mpaka vurugu hii ilipotokea nikaamini ni kweli. Jamaa aliyefanya tendo hili amerejea na kimwana wake na kusababisha tafrani iliyopelekea kuumizana vibaya hutaamini.


Ilikuwa hivi, kijana mmoja alirejea toka Ulaya hivi karibuni, akaona atafute mchumba. Hakutaka ile ya kuzungukazunguka, aliona aoe moja kwa moja. Jirani yake kuna binti mmoja mrembo kwelikweli lakini wa geti kali. Akampenda, akatafuta kila mbinu wakaonana, wakakubaliana.


Hili swala likapelekwa kwa wazazi na wao wakaridhia. Kiutaratibu mkishakubaliana kuwa wachumba na mkawa katika harakati za maandalizi ya harusi wewe muoaji huwa huruhusiwi kuonana moja kwa moja na binti wa watu analindwa ile mbaya, inagawaje sasa mambo haya yanafifia.


Lakini wapo wale ambao wanafuata taratibu hizi hadi leo. Sio mbaya, ila wanadamu ndio wabaya. Jamaa huyu huko Ughaibuni alikuwa na best friend wake mcheshi saana, basi yeye akaona amtumie kama mshenga wake.


Hili ni kosa kubwa, kwani washenga ni vyema wawe watu walio-oa, kama sikosei. Tusipende kuwachukua vijana, marafiki zetu ambao ni mabachela. Mawasiliano kati ya binti na jamaa yetu huyu yakawa kupitia kwa mshenga yule na wazazi wa pande zote mbili walimuamini sana huyu jamaa.


Lakini kilichokuwa kinaendelea katikati hapa watu walikuwa hawajui. Walijua baadaye.Kukawa na visa na matukio ya kuahirisha ahirisha hii ndoa kwa muda, mara bwana harusi kafiwa,mara binti harusi anaumwa , mara hili au lile. Matukio haya yalikuwa mazito yakusababisha harusi icheleweshwe na kusogezwa mbele kila tukio linapotokea.


Siku isiyojulikana binti akayeyuka. Hutaamini, wazee wa pande zote mbili walihaha huku na kule, kwanza walimficha bwana harusi lakini baadaye ilibidi aambiwe kuwa binti ametoroka nyumbani na haijulikani alipo.


Bwana harusi akachanganyikiwa, unajua kuchanganyikiwa, huyu jamaa alichanganyikiwa, akawa hali vizuri ana mawazo, akajikuta anakonda kwa kipindi kifupi. Kwanini ilitokea hivyo, kwanini alimfanyia hivyo kwanini, ikawa kwanini…Cha ajabu huyu mshenga aliondoka naye, lakini yeye aliaga kuwa amepatwa na dharura atarejea karibuni, kwahiyo hamna mtu aliyemdhania vibaya.


Na huku alikoenda akawa anawasiliana na jamaa huku akimpa moyo kuwa asikate tama. Siku zikayoyoma jamaa akasalimu amri kuwa `hiyo siyo ridhiki’ na bahati nzuri akasafiri kidogo huko majuu. Alirudi hapa karibuni na mikakati ya kutafuta mchumba mwingine.


Wakati yupo kwenye pilikapilika za kuchuja huyu au yule,mara yule mchumba wake wa zamani akareja. Na amereja na mzigo. Na mzigo huo sio mwingine ni mimba, ujauzito. Inavyoonekana wazazi wa binti walishajua nini kinaendelea, lakini wakawa wameficha, kwani vinginevyo wangeenda polisi, kuwa binti yao kapotea, hii ni hisia yangu.


Siku moja jamaa akawafuma `live’ binti yule akiwa ameongozana na mshenga wake wakitokea kiliniki. Jamaa akashindwa kuvumilia, ikawa vurugu kweli. Jamaa anasema nia sio kumgombea yule binti ila yeye alitaka kumfundisha adabu yule mshenga ambae ni rafiki yake, kwanini alimfanyia kitendo kile, baada ya kukiri kuwa yule sasa ni mkewe.

Ni vizuri kuwa waangalifu na watu hawa, na uwe na uhakika na unayetaka kumuoa kuwa kweli anakupenda kwa dhati au ni babaisha bwege. Wenu emu-three"

No comments:

Pages