Tuesday

Nilihisi, nikahakiki, akabisha sasa nimepoteza mapenzi?-Ushauri

"Hi dada Dinah,
Mimi ni msichana wa miaka 28 nimeolewa na nina watoto waili. Tatizo langu ni kwamba nilihisi mume wangu anatoka nje ya ndoa wakati nikiwa mjamzito wa mtoto wa pili, baada ya kuona anapokea simu za ajabu ajabu na kutwa simu zake alikuwa anaziweka silent au simu zinakaa kwenye suruali tu au kwenye gari.


Siku moja usiku kama saa 4 hivi ilipigwa simu alikua anaoga cha ajabu simu ilikuwa inawaka taa tuu kwa namba hiyo ila kwa namba zingine zinaita kwa sauti ila kwa namba hiyo ndio inawaka taa tu tena bila hata vibration, mi kuona hivyo nikapokea hiyo simu na kukutana na mwanadada bila hata kujua ni mie nikasikia mambo darling, nikamwambia Darling wako anaoga una ujumbe akija nimpe?


Akakata simu mie nikachukua ile namba nikasave kwenye simu yangu na darling wake alipotoka siku mwambia kama alipigiwa simu. Mara tukiwa mezani na watoto tunakula ikapigwa simu ileile akapokea akaanza kubabaika, kidogo kaacha chakula kasema kaitwa na ndugu yake ana matatizo na mie nikamwambia ni bora twende wote maana kama ndugu yake na mie ni wangu pia akakataa na mie nikamwambia hutoki nje ya nyumba hii usiku huu bila mie nikachukua funguo zote za gari nikakaa nazo na nikamwambia ukitoa mguu hapa utajuta.


Basi akaenda chumbani kupiga simu na mie nilijua tuu nikaenda mlangoni nikawa namsikiliza eti anasema naweza kuja ila sina uhakika ila usitegemee sana. Sasa mie kwa hasira Asubuhi nikampigia huyo dem wake kwa private akapokea nilivyokuwa naongea nae akanishtukia akampa mwanaume aongee.


Jioni nikauliza hii namba ni ya nani akaniambia ni ya rafiki yake nikamuuliza mbona sijawahi kusikia kama una rafiki kama huyo nikamwambia mbona ni mwanamke akaniambia kuwa huwa wanashare na mumewe simu nikajua lazima atakuwa kamwambia kuwa nimepiga simu leo.


Nikamwambia huo ni uongo, Basi baada ya hapo nikawa na stress za ajabu mpaka nikapata na matatizo sana mpaka nikaandikiwa Bedrest na ninashukuru Mungu kanijaalia nikazaa salama salmini.


Baada ya kuona nina matatizo akaniambia kuwa huyo dem ni mke wa rafiki yake na anamtaka yeye hana mpango nae na hana tena mawasiliano nao kabisa na sitakaa nisikie simu wala nione sms toka namba hiyo.


Mara akaumbuka ilipoingia sms inamuuliza Vipi leo utakuja??? Mi nikaijibu nikasema siji then nikamwambia kuna msg yako hapa imekuja na nishakujibia, Nikamwambia kama kweli huna mpango nae mpigie simu umwambie amkomeshe na mie nikisikia kama kweli akasema ooh haina haja sijui nini akajitetea na kusema kwakua ndio nilikuwa nimetokakujifungua hata mwezi haujaisha.


Nikaachachana nae nikalala nikaogopa kujipa stress nikakosa Maziwa ya mtoto bure, Asubuhi nikapiga simu ili niongee na yule dada kwa amani yule dada lipogundua ni mimi aliniporomoshea mitusi hata kabla sijaongea nilichotaka kuongea.


Jioni nikamwambia bwana'ake(mume wangu) nikajibiwa sasa na wewe unapigiapigia simu tu watu usiowajua unategemea nini? Sikuamini kama nimejibiwa hivyo nikasema poa nimekoma. Na toka siku izo nikawa sina mapenzi na yeye nikawa namwangalia tuu, niko na watoto wangu tu ila yeye sina stori nae zaidi ya salamu na siku nyingine hata simsalimii ila naumia sana.


Nikakaa kimya nikawa sina mpango nae tuko tuu kama kaka na dada nikiongea nae sawa nisipoongea nae poa, Siku moja nikaamua kumtisha nikamwambia sasa nishamaliza meternity leave namaanisha kuwa mtoto ni mkubwa vya kutosha na sasa na mie naweza kutafuta mtu wa kunipooza moyo niondokane na mawazo nikae na mie na amani moyoni tuwe Ngoma droo.


Maana kama yeye kaoa na anatongoza basi na mie nimeolewa na nitatongozwa na akijaribu tu namkubali hata kama sijampenda ilimradi na mie nipoze moyo .Kumbe ilimuiingia na akajua naweza kufanya kweli akaanza kujidai anarudisha mapenzi kwa kasi kubwa mara ananiongelesha hata kama sitaki kuongeleshwa mara hivi mara vile.


Ila mie nikawa tu kama jiwe sijali ndo kwanza najidai simwoni niko Busy na simu kutwa nachat na rafiki zangu nacheka yani hata nikiwa na rafiki zake au ndugu zake mie busy na simu yangu tuu wala siwaoni.


Siku moja nilikuwa nimelala akaniamsha eti naomba kuongea na wewe nikamsikiliza akaniambia eti kuwa vile nilivyokuwa navihisi ni kweli alikuwa na mahusiano na huyo dem ila ni mahusiano tu kama rafiki yake tu wa kuongea nae tuu na kunywa tuu lakini hajawahi kufanya nae chochote hata kiss hajawahi miezi yote zaidi ya 7.


So mie nikitaka kufanya nitalipiza itakuwa ni kuwaumiza watoto tu cha kufanya tuelewane na tupendane kama zamani maana yeye hajafanya chochote cha ajabu ni kukaa tu na kuongea na huyo dada.


Nikamuuliza kama kweli kwanini ulishindwa hata kuniambia kama una rafiki wa design hiyo? Na kwanini siku aliyonitukana kama ni rafiki wa kawaida kwanini asimchukulie hatua yeyote au kwanini huyo dada anitukane kama hatembei na mume wangu??


Mi nikamsikiliza alivyomaliza nikamwambia haya nimekusikia nikaendelea kulala maana nilijionea ananizingua tuu mie nausingizi na nasubiri niamke kumnyonyesha mtoto ye ananiletea habari zake za kijinga ambazo mie zimegoma kaminika na kichwa changu.


Sasa naomba mniambie kwa story hiyo ni kweli kua hajawahi kufanya chochote au kaamua tu kuniambia hivyo kwakuwa nimemtishia na mie kutoka nje ya ndoa au kurudisha amani ndani?


Mie bado nipo vilevile kama jiwe vile simjali kwa chochote najijua mie na wanangu tuu yeye namwona kama picha ya ukutani tuu."

Jawabu: Asante sana kwa ku-share tatizo lako mahali hapa, nakupa pole kwa yote unayokabiliana nayo lakini wakati huohuo nakupa hongera kwa kusimama Imara dhidi ya emotional "abuse" kutoka kwa mumeo.

Hili ni tatizo sugu kwa wanaume wengi wa Kiafrika, mwanamke anapokuwa mjamzito au kujifungua wanadhani wamepatiwa nafasi ya kwenda kutembeza "viungo" vyao nje ya ndoa zao. Kutokana na maelezo haya ni wazi kuwa mumeo hakuwa akikuthamnini na wala hana haeshimu ndoa yake.

Hawajui kuwa Mwanamke anahitaji ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa mume mara baada ya kujifungua, sio kuanza kusumbuliwa kiakili na kihisia.


Mumeo ameongopa ili wewe usiende kufanya kama alivyofanya yeye(Mkuki kwa Nguruwe) lakini ukweli (kutokana na maelezo yako) amefanya mambo ya kimapenzi mengi tu na huyo "rafiki yake".


Kinachoshangaza nikuwa, pamoja na kukubali urafiki ulikuwepo bado hajaonyesha kuwa anajutia makosa yake kwani hajakuomba msamaha, kitu kinachonifanya mimi (Dinah) nihisi kuwa mumeo huyu anakiburi, anajivunia alichokifanya na hana mpango wa kubadili hiyo tabia yake chafu.


Naelewa kabisa uamuzi wako wa kumtenga mumeo na itachukua muda mrefu sana mpaka utakapomuamini tena, kumtamani tena, kumtaka tena na kujisikia kutaka kufanya nae mapenzi.


Inawezekana kila ukiwa nae karibu au anapokufanyia jambo/mambo fulani picha ya yeye kumfanyia yule mwanamke mwingine inaweza kukujia na kuua "mood", yaani hata kama ulikuwa na hamu inakuishia ghafla.


Nini cha kufanya-Kama tangu umejifungua hujafanya mapenzi na mumeo itakuwa vema akienda kuangaliwa kama yuko salama kutoka VVU, lakini kama ulikuwa ukifanya mapenzi wakati unahisi kuwa "anatereza" nje basi ni vema kama wewe, yeye na mtoto mkaenda kuangaliwa damu ili mjue kama mko salama kutoka VVU.


Pamoja na kuwa mumeo anaonyesha mapenzi kuliko mlivyokutana hapo mwanzo, hakikisha hu-give in mpaka aombe msamaha na kuahidi kutorudia tena kosa alilolifanya (msamaha maana yake ni mabadiliko kwa vitendo), hivyo hiyo itakuwa nafasi yake pekee ya kubadilika.


Kamwe usimwambie ukweli kuwa ulikuwa unamtishia kuwa utaenda kulalwa nje ya ndoa yako, iache kama ilivyo.......najua siku moja atataka umhakikishie kama kweli ulikuwa na mpango huo au hata kama tayari umelala na mwanaume mwingine (hapo alipo linamuuma kweli kweli sema hana jinsi ya kuliweka wazi......hakuna mwanaume anapenda kutombewa mwanamke wake, hasa yule mwenye tabia hiyo.


Akitaka kujua muambie ukweli kuwa hukufanya lakini ulikuwa ukisukumwa kufanya hivyo kutokana na tabia yake ya kwenda nje ya ndoa yenu...kwa maana nyingine ni kuwa, huwezi ku-cheat ikiwa yeye hato-cheat, aki-cheat anakuhamasiha na wewe kufanya hivyo. Hii itakuwa adhabu tosha kwake japokuwa wewe unajua moyoni huwezi ukafanya hivyo bali ulikuwa ukimtishia tu.

Kitu kingingine ambacho ni muhimu sana ni kuwekeana Sheria, ni mume wako, mnapokuwa pamoja inamaana mnaunda ushirika fulani ambao unapaswa kufuata Sheria fulani na ni mwiko kabisa kuzivunja.

Kwa Mf-Simu yake ni yako, rafiki zako awafahamu na wewe uwafahamu wake, Namba zote ziwe-saved kwa majina unayoyajua kutokana na ulivyotambulishwa, kama kuna shughuli za kifamilia wote 2 mnashiriki, hakuna safari za usiku unless mnatoka wote, kuambizana kwa uwazi kama kuna kitu kimepungua kwenye uhusiano wenu na kupeana mikakati ya kukirudisha, kuwa na muda wenu kama wapenzi na sio kama baba na mama, kutumia kinga dhidi ya VVU mpaka utakapo hisi kumuamini tena (kama utaamua kufanya mapenzi na mumeo).


Kumbuka kwenye ndoa yenu kuna watu wadogo wawili hivyo ni muhimu kuwafikiria watoto wenu zaidi na maisha yao ya baadae kuliko kujifikiria ninyi zaidi. Hawa watoto wanahitaji mapenzi yenu nyote wawili, baba na mama mliopendana hapo mwanzo na kufunga ndoa.....hivyo ni vema kuonyesha mapenzi mbele ya watoto wenu na tofauti zenu kuziweka pembeni machoni mwao.


Ukiona unashindwa ku-recover kutokana na "Emotional abuse" basi unaweza kwenda kupata msaada kwa wataalamu, kama nilivyosema itakuchukua muda mrefu lakini kutokana na ushirikiano wa mumeo (kubadili tabia) utakuwa sawa na kufurahia ndoa yako.

Wewe ni mwanamke tofauti kabisa na wale tuliowazoea hapa Bongo akina "ndio bwana", ni mfano wa kuingwa na wanawake wengine, kisa chako kinaonyesha kuwa huitaji mwanume bali unamtaka mwanaume.........Safi sana.

Mimi na wachangiaji wengine tunakutakia kila la kheri.

No comments:

Pages