Tuesday

Bado nampenda Mume wangu lakini Dini imetutenganisha-Ushauri!

"Dinah mdogo wangu hujambo? Nawasalimia wanaGlob wote, nami naleta shida yangu ili nisikie wanajamii wa Dinahicious itanishaurije. Mimi ni mmama mkubwa tu, ni Muislamu na niliolewa na Bwana ambae alikuwa Mkristo nikiwa na umri wa miaka 23. Alikuwa ni mwanaume wangu wa kwanza tukiwa wanafunzi wa Chuo.

Uhusiano wetu uliendelea vizuri na baadae tukapata mtoto mmoja, Mpenzi wangu alikubali kufunga ndoa ya udanganyifu ya Kiislamu ili wazazi wangu wamkubali hivyo alislimishwa na tukafunga ndoa, baada ya siku tatu akaungama na kurudi Kundini.

Tuliendelea kuwa pamoja kwa miaka kadhaa kama mume na mke na tulipofikisha miaka mitano alidai tuende tukabariki ndoa yetu Kanisani lakini mimi sikuwa tayari kwa hilo hivyo akatafuta mwanamke mwingine kama nyumba ndogo na akasema kuwa anaoa.

Mimi sikumkatalia lakini nilimuambia kuwa nitaondoka nyumbani kwake, hapo tayari alikuwa ameanza ratiba ya kulala huko mara tatu kwa wiki, iliniuma sana Dinah. Lakini nilivumilia hali hiyo kama mwaka na kila nikimuambia kuwa naondoka kwake wala hakuwa akionyesha kujali yaani hata kusema usiondoke hasemi.

Ilipofika siku maudhi yamezidi, nikatafuta nyumba nikapanga, kabla sijahamia nikamueleza kuw animepta nyumba na nitaondoka nyumbani kwake kama kawaida hakupinga wala kuonyesha kujali basi mimi nikaondoka na kuanza maisha mapya huko nilikopanga. Baada ya muda mfupi nikaenda masomoni na niliporudi nilikuta tayari amefunga ndoa ya Kanisani na yule Mdada.

Mimi na yeye hatuna maswasiliano ya mara kwa mara lakini tunapowasiliana huwa anadai kuwa hana amani na inamuuma sana na itaendelea kumuuma mpaka anaingia kaburini. Kuna wakati maneno yake hunigusa sana hasa ukizingatia bado nina hisia nae.

Kwa sasa sijaolewa lakini akanibariki kwani kuna watu wawili-watatu wamejitokeza kutaka kunioa lakini mimi bado sijaamua kuolewa tena. Moyoni nahisi ingekuwa inawezekana kumrudisha Mume wangu ili tumkuze kijana wetu basi ningefanya hivyo, Ila nitakuwa tayari kama atakubali kurudi kuwa Muislam.

Da Dinah nimeileta hii ili nisikie ushauri wako pamoja na wachangiaji wengine. Je nimshauri aingie Uislam ili turudiane kwani nahisi bado nampenda au nikaze tu Moyo ili niolewe na mmoja kati ya hao wengine wanaotaka kunioa?

Naomba ushauri wenu tafadhali, natanguliza shukrani."

Dinah anasema: Mimi sijambo kabisa mdada, vipi wewe. Asante sana kwa ushirikiano wako. Dini ni Imani au mfumo wa maisha hapa Duniani ambao tunaufuata baada ya kukuta wazazi wetu wanauabudu lakini ukweli unabaki palepale kuwa wewe unapozaliwa na wazazi wenye kuamini Imani fulani haina maana na wewe ukiwa mtu mzima mwenye uwezo wa kufanya maamuzi juu ya maisha yako bila kutegemea wazazi uendelee kuiamini Imani hiyo.

Mfumo huu wa maisha unatusaidia sisi kuwa karibu zaidi na Mungu ambae wote tunaamini kuwa anatulinda, kutusaidia na kutuepusha na mabaya yote hapa chini ya Jua (Duniani), lakini linapokuja suala la mapenzi Dini huwa haina nafasi kwa sababu hujui ni mtu gani utamdondokea kimapenzi na yeye akakupenda jinsi umpendavyo!

Itakuwa ni mara chache sana kukutana na mwanaume mwenye Imani kama yako na mkapendana kwa dhati unless mnajumuika pamoja kwenye shughuli za kiDini au wazazi wake na wake wawaunganishe AGAIN itakuwa bahati sana kwako wewe kumpenda huyo uliyetafutiwa ili kufunga ndoa.

Sina uhakika na jinsi ndoa za Kiislamu zinavyofuatiliwa ili kuidhinisha "Talaka" ukiachilia ile ya "kisheria za kijadi" ambayo wenza hujulikana wameachana ikiwa hawajakutana kimili kwa muda fulani.

Nina uhakika na ndoa ya Kikristo kuwa haina Talaka, japokuwa siku hizi kuna sheria inayomruhusu mtu yeyote kumtakili mwenza wake Kisheria ili kuepuka usumbufu na unyanyasaji ambao unatokana na umilikishi (mume wangu, mke wangu) vinginevyo ndoa hiyo itaendelea kujulikana kuwa ni wanadoa waliotangana na kila mmoja hatoruhusiwa kufunga ndoa tena mpaka mweza wake afariki Dunia huko aliko.

Ndoa ya Kiislam uliyofunga haikuwa halali kwani wote mlikuwa mnajua kuwa mnafanya hivyo ili wazazi wako wamkubali, lakini kama kuna uthibitisho kuwa mlifunga ndoa basi hata ndoa yake aliyofunga Kanisani ni batili kitu ambacho kinaweza kurahisisha mambo kama wote wawili mtakubaliana kuhusiana na Imani zenu za Dini.

Kutokana na maelezo yako inaonyesha kuwa Imani zenu za Dini ni muhimu zaidi kuliko uhusiano wenu wa kimapenzi na kama ukweli ndio huo basi itakuwa ngumu sana kwa ninyi wawili kuishi pamoja kwani wote hamtaki kubadilisha Mfumo wa maisha yenu kiimani.

Natambua unampenda mzazi mwenzio na ofcoz anakuwa wazi sana kwako na comfortable kuongea na wewe mambo mengi kwa vile mmekuwa pamoja kwa muda mrefu na anatambua kabisa kuwa wewe ni mwanamke unaemuelewa vizuri kuliko Mkewe wa kanisani. Pia inawezekana anataka kuwa na uhusiano mzuri na wewe kwa faida ya mtoto wenu.

Kama kweli unampenda na unataka kurudiana nae basi utafanya lolote ili kurudiana na "mumeo", tunapozungumzia kufanya lolote ni pamoja na kubadili Dini na kufuata Imani anayoiamini yeye.

Wapenzi huwa radhi kubadili Dini, wengine hata Kukana wazazi wao kwa ajili ya wapenzi wao, sasa kama kweli wewe unampenda Jamaa na una uhakika anakupenda kwanini usifanye atakacho ili kuwa nae?

Ndoa yake ya Kanisani sio batili kama unauthibitisho wa aina yeyote kama vile cheti cha ndoa n.k...hivyo isikutishe kabisa. Huyo mwanamke aliefunga nae ndoa ameingilia ndoa yako na hakika huyo ni mume wako wa kudumu kama utaamua kuafiki na kubariki ndoa hiyo Kanisani.

Lakini kama Dini yako ni muhimu zaidi na labda hutaki kuwaudhi wazazi wako ambao mimi naamini kabisa kuwa hawahusiki na maisha yako ya kimapenzi basi kubali kuolewa na hao wanaume wengine waliojitokeza.

Natumaini sehemu ya maelezo yangu na michango ya watu wengine yamesaidia ktk kufanya uamuzi wa busara.

Kila la kheri!

No comments:

Pages