Monday

Mke asikiliza wambea na sasa tunaishi ki Juma na Roza

"Habari za kazi Dada Dinah na heri ya mwaka mpya.
Mimi Naitwa Emmi nipo Iringa nimekuwa mpenzi sana wa blog yako hasa kwa ushauri na maoni mbalimbali yatolewayo humu.

Mimi nina mke nimeoa miaka mitatu iliyopita na tumejaaliwa mtoto mmoja wa miaka miwili sasa. Shida yangu sister ni kwamba mke wangu anapenda sana kusikiliza maneno ya mitaani. Mimi ni mnywaji wa pombe kiasi lakini yeye hanywi na aliniruhusu kunywa isipokuwa nisizidishe kiwango na hilo nalizingati sana.


Sasa yeye akiambiwa tu umbea kuwa mmeo ana wanawake wengine basi akirudi kutoka huko atokako hunijia kama Mbogo na hataki kusikia cha mtu, yaani ananitukana sana lakini mimi kwa sababu nampenda na pia kujali sana uwepo wa mwanangu huwa simlipizi kwa kutusi zaidi ya kukaa kimya.


Ila kuna wakati nilimwambia aachane na hao wambea kwani watambomolea nyumba yake lakini anabisha. Kwa sasa imefikia hatua hataki kukaa na mimi na anatafuta kila sababu ili nimfukuze ila mimi ni kimya nasubiri uamuzi wake.


Jamani nipeni ushauri juu ya huyu mwanamke, je nimuache au niendelee kukaa kimya huku yeye akiendelea na matusi yake ndani ya nyumba? Kwani kwa sasa tunaishi kama kaka na dada yaani kila mtu ana chumba chake, nafikiri umenielewa.
Nitashukuru sana kwa ushauri wenu Wadau.
ahasante!!! Manuel"

Dinah anasema: Manuel asante sana na heri ya Mwaka mpya! Unajua ndoa inajengwa na watu wawili ambao ni mume na mke. Huyo Mke asingesikiliza maneno ya watu na angekuamini kama ungekuwa unakunywa pombe na yeye akiwa pembeni.


Lakini kwa vile huwa hayupo unapokwenda kulewa anahaki zote za kuwa mkali nakukubali anachoambiwa na Mashoga zake ambao baadhi huenda ni walevi nahuenda huwa unafanya nao utani au wao wanakutania wewe kupita kiasi na pengine umewahi kuwtaongoza bila wewe kujua kutokana na pombe na hivyo kuhisi kuwa unaweza ukawa na mwanamke wa nje na hivyo kupeleka habazi ambazo hazina uhakika kwa mkeo.

Unajua tena Mji wa Iringa ni mdogo na usikute watu wanajuana na wanajua unanywea bar gani na huko bar huwa unakaa na kina nani......kama marafiki zako hawajaoa au wameoa lakini sio waaminifu kwa wake zao ni wazi baadhi ya watu wanaweza kuhisi kuwa hata wewe unafanya kama wanavyofanya watu wote unaokunywa nao Pombe hapo kilabuni/baa.

Ni kweli marafiki zake (Wambea) wanaweza kutunga na kum-feed maneno mkeo ili kuharibu ndoa yenu nahivyo wao kuwa huru kutoka na wewe....yote yanawezekana.

Tatizo hapo sio mameno ya wambea, tatizo hapo ni kuwa Mkeo anahisi upweke ndani ya ndoa yenu, ni wazi kuwa humpi muda wa kutosha kwa vile muda mwingi unautumia ukiwa kazini na kilabuni. Unaporudi nyumbani unakuwa na kilevi kichwani hivyo sio wewe kwa asilimia zote....sijui unanielewa hapa?!!

Sasa kutokana na upweke huo ambao unaweza kumfanya afikirie mengi mabaya na hata kuzaa wivu mkali ndio unaomfanya asikilize na kuamini kila anachoambiwa na marafiki zake kwa vile wako pale kwa ajili yake na wanaonyesha kumjali, kumsikiliza na kumpa ushauri.....hata kama ushauri ni wa kubomboa bado atawaamini kwa vile Saikoloji yake inaamini kuwa "wanamjali, wanamsikiliza na kumthamini" zaidi kuliko wewe.

Ninachokiona hapa sio "umbea" bali ukosefu wa mawasiliano na wewe kushindwa kuzingatia nguzo muhimu iitwayo "Maelewano" Mf: wewe ni mnywaji ili asikunyime kile unachokipenda kutokana na pombe amekubali kuwa endelea kunywa lakini sio sana.....mkeo ame-complimise hapo!

Je! wewe umekubali kitu gani ambacho labda wewe hukipendi lakini kwa vile ni mkeo mpenzi na hutaki kumnyima raha ya kufanya jambo alitakalo ukakubali aendelee kufanya jambo hilo....SIDHANI!


Unatakiwa kumshukuru Mkeo kwa kukuamini na kukuruhusu uendelee kunywa pombe lakini usizidishe. Mkeo sio tu anakupenda bali pia anajali afya yako kwani sote tunajua Pombe sio nzuri kwa afya zetu.

Sasa kwa vile ameruhusu uendelee kunywa haina maana uende kilabuni kila siku na badala yake unaweza kunywa ukiwa nyumbani na hivyo yeye kupata muda wa kuwa na wewe. Unaweza kabisa kufurahia Bia ukiwa na familia yako sio washikaji kila siku.....wewe ni mume na baba hivyo jaribu kuzingatia majukumu yako kama Mwanaume wa kisasa.

Ukimya wako ndio unamfanya mwanamke huyo kuzidiwa na hasira na ndio maana hatakaki hata kuwa karibu na wewe, sio hivyo tu inawezekana anaamini kuwa umetoka nje ya ndoa na hataki kupata maamubukizo ya HIV (kitu ambacho hata mimi nampongeza) incase ulitereza nje kiukweli.

Nini cha kufanya: Watu wengi hukimbilia Talaka, lakini tukumbuke kuwa Talaka sio suluhisho la matatizo na mkikimbilia Talaka ni wazi hutomkomoa yeye mkeo au rafiki zake bali mtoto mliemleta hapa Duniani. Mtoto wenu ndio ataumia japokuwa ni ngumu sana kwa ninyi wazazi wake kuona maumivu yake Kiakili, Kimwili, Kisaikolojia na Kihisia.

Tafuta muda mzuri, ukiwa umetulia kiakili na zungumza na mkeo, Omba msamaha kwa kutokuonyesha kuwa unajali (hii itamlainisha na kumfanya akusikilize vema), mhakikishie ni kiasi gani unampenda na ni muhimu kiasi gani kwenye maisha yako.

Mwambie kuwa yote anayosikia kutoka kwa rafiki zake sio kweli na ili kumthibitishia hilo basi uko tayari kwenda kuangalia afya yako (vipimoo vya HIV)...majibu yakitoka safi ni wazi itampa amani moyoni na hivyo kuanza kulala kitanda kimoja na mume wake (wewe Manuel).

Weka wazi yote yalioujaza moyo wako kutokana na tabia ya mkeo ambayo ni wazi imesababishwa na unywaji wako wa Pombe.

Kumbuka Ndoa inajengwa na Nguzo 3, (1) Zote ambazo ni kwa mujibu wa Imani za Dini zenu, alafu kuna zile mbili za kidunia/kabila (inategemea unatoka wapi) ambazo ni (2) Uhusiano wa kimapenzi (3) Uhusiano wa kingono.

Uhusiano wa kimapenzi nao una Nguzo tano muhimu ambazo ni Heshimiana, Thaminiana, Shirikiana, Sikilizana/Elewana/kubaliana na mwasiliano (kuna topic inazungumzia kwa kirefu )sasa wote wawili mnatakiwa kuzingatia hayo ili kuimarisha uhusiano wenu wa kimapenzi.

Pia ongeza muda unaotumia kuwa na mkeo, badala ya kuzungumzia masuala kuhusu maisha na mtoto hakikisha mnazungumza kuhusu ninyi wawili kama wapenzi kitu ambacho kitawasaidia kuw akaribu zaidi na hata kuboresha uhusiano wenu wa kingono.

Punguza unywaji wa pombe kwa maelewano kuwa nae apunguze marafiki wasiokuwa na mpango, badili utaratibu wako wa kwenda kunywa pombe kilabuni na badala yake nunua chupa/kopo za pombe na kunywa huku mkeoyuko pembeni.

Kila la kheri!

No comments:

Pages