Monday

Nifanyeje? Tuna VVU Binti wa kazi adai Mimba ni ya Mume wangu?

"Hodi wenyewe, mama nanihii upo?’ ilikuwa sauti ya mama mmoja alikuja kuchota maji. Mimi nilikauka kimya, siunajua tena siku ya Jumatatu unatakiwa uwe kazini lakini kwa vile bado nipo kijiweni, sikupenda majirani wajue hili.

Mama watoto alikimbilia nje na kumkaribisha huyu mgeni ambaye hakutaka kuingia ndani zaidi ya kuchota maji na kuondoka. Yule mama alimuuliza mama watoto wangu kama anataka mfanyakazi, niliguna moyoni, nikijua nini jibu atakalopata.‘Kwa hivi sasa sihitaji, inagwaje kweli ni muhimu ningekuwa naye, kwasababu nashindwa kufanya shughuli nyingine au kutoka kwa vile sina mtu wa kumkabidhi majukumu’ mama watoto alimijibu.

‘Sawa, lakini huyo ni mtoto mzuri kitabia, ingawaje hawa watoto wa nyumbani unaweza ukawaamini sana lakini wakafanya jambo ambalo hutazamii. Yaani mimi hapa nilipo natamani duniani inimeze kwa tukio lililotokea kwangu, kisa cha mfanyakazi wa nyumbani’ Huyo mama akaamua kukaa kwenye ngazi za nyumba yangu ili aweze kumhadithia mke wangu.

Nilikuwa dirishani kwahiyo maongezi yao nilikuwa nikiyasikia vizuri, na kwa vile Yule mama hakujua kuwa nipo aliongea kiundani mambo yake, kama unavyowajua akina mama wakiamua kuongelea swala Fulani kwa mtu anayemuamini.‘Ndiye unayetaka kuniletea mama?’ mke wangu aling’aka.

"Hapana sio huyo, huyo wangu namuandaa aende kwao kalikoroga mwenyewe’ Yule mama alisema , na kabla mke wangu hajamuuliza vizuri alianza kuhadithia kisa ambacho kilinifanya nishituke na kuamua kukiweka hapa ili wale wenye nia njema wachangie na huenda iwe fundisho kwa wenye wafanyakazi wa nyumbani.

Binti huyu niliye naye nilimchukua akiwa mdogo, alipomaliza darasa la saba. Tuliishi nae kama binti yetu, na kwa vile alikuwa na adabu , mchapakazi mzuri niliamua kumsomesha Sekondari hadi kidato cha nne. Hakufaulu, lakini tulikuwa na malengo ya kumsomesha zaidi.

Lengo hilo lilikwama kwasababu mume wangu kibarua chake kiliota majani, ikawa mimi ndiye mhudumiaji wa familia. Kama unavyojua kipato changu ni kidogo nisingeweza kumsomesha na kuilisha familia, kwahiyo tukakubaliana kuwa asubiri hadi mume wangu atakapopata kazi.

Siunajua maeneo ya huku kwetu kama unafanyakazi ili uwahi kazini inabidi uondoke saa kumi na moja alifajiri na kurudi nyumbani ni kuanzia saa mbili za usiku. Hili halikuwa tatizo kwasababu mume wangu alikuwa katika mkumbo huo kabla hawajampunguza kazini kwao.

Na pia yupo huyo binti ambaye tulimchukua kama mfanyakazi wa nyumbani na bado tunaendelea kumlipa licha ya kujitolea kumsomesha na kumpa huduma zote kama mtoto wetu. Lakini kama walivyosema wahenga, kuku wa kienyeji hafugiki, na kweli kwa hili sidhani kama nitahitaji mfanyakazi wa nyumbani tena.

Wakati mwingine nawashangaa sana hawa waume zetu, sijui akili zao zikoje. Unajua ninakuhadithia hili sio kwasababu nimjinga wa kutoa siri za mume wangu nje. Hapana, lakini lilotokea inabidi nimhadithie mtu ninayemuamini ili anipe ushauri.

Naujua ushauri nasaha nimeshaupitia, lakini huu sasa ni mkali zaidi. Wiki kama mbili zilizopita nimepata kalikizo kadogo nikaona nishirikiane na familia kujifanyia miradi midogo midogo na hapo ndipo nilipogundua kubwa kuliko.

Mfanyakazi wangu huyu wa nyumbani ni mjamzito nilipomuombana aniambie ni nani aliyempa hiyo Mimba, alikataa katakata, hadi nilipomwambia na mrejesha kwao kijijini ndio akanitajia. (Nitamrejesha kwao ingawaje hataki lakini kwa hali ilivyo sitaweza kusihi naye tena).

Nilishindwa kuamini kuwa Mume wangu ndio mwenye mzigo huo yaani hadi sasa siamini mbaya zaidi nilipomuuliza Mume wangu nae alikataa kakataa kabisa sasa sijui nimuamini nani? hili linawezekana kweli?.

Isingekuwa mimi na mume wangu tumeathirika na VVU ningefungasha virago vyangu ili kumuachia nafasi, manaake kaona simfai mpaka anatembea na Msichana wa kazi, lakini kutokana na tatizo letu tunahitajiana hasa kwenye kumlea mwanetu ambae pia aligunduliwa kuwa ameambukizwa.

Tuliamua kupima baada ya mtoto wetu kuwa anaumwa mara kwa mara, alipopimwa akaonekana ana Virusi vya UKIMWI hivyo na sisi tukalizimika kupima na majibu yakawa hayo kwamba wote tunavyo.

Sio siri kuwa mimi na mume wangu na mtoto tumeathirika, sasa sikutegemea kuwa mwenzangu anaweza kukosa imani na kudiriki kutembea na mfanyakazi wetu ilihali anajua kuwa anamtataizo haya ya kiafya.

Mume mume wangu kakataa katakata na kusema huyu binti kaumua kumpakazia ili asiondoke hapa nyumbani. Je nifanyeje ili kuupata ukweli? Japokuwa namuamini sana mume wangu na tangu tuoane naye hajawahi kunisaliti au kunidanganya. Sasa mimi nachanganyikiwa sijui nishike wapi? Nisaidie ushauri, nifanyeje?" Akamaliza huyo Mgeni mchota maji.


Kwa haraka haraka Mke wangu akamuambia Mgeni wake kuwa afuate Sheria, kwamba amshitaki na huko kwenye vyombo vya Sheria atapata ukweli na ushauri huo ulimfanya Yule mama ainuke na kwa hasira akaaga huku akisema‘Nini?, nimshitaki mume wangu?kwaheri" aliaga mama huyo!

Je ingetokea kuwa huyu mama kaja kwakokutaka ushauri ungemsaidiaje? Ungemshauri vipi?
Asanteni.
M3.

No comments:

Pages